Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Ndejembi: Mbuyu wa siasa za CCM ulioacha kishindo

34509 Pic+ndegembi Tanzania Web Photo

Wed, 2 Jan 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Imekuwa ni vilio na huzuni huku wengi wakipigwa na mshangao. Lakini maandiko yanasema siku za kuishi kwa mwanadamu ni miaka 70 na ikiwa ana nguvu ni miaka 80 lakini huyu alishapita.

Mwishoni mwa Desemba 29, 2019 Gwiji wa siasa nchini Pancras Ndejembi alimaliza kazi yake duniani.

Ndejembi alidumu katika uenyekiti wa CCM wa mkoa wa Dodoma kwa miaka 25 (1982 -2007). Katika kipindi kwa miaka 10 alikuwa mwenyekiti wa wenyeviti wa CCM wa mikoa, cheo ambacho kimefutwa karibuni.

Wengi na hasa wapenda siasa wanamfahamu mzee huyo aliyejulikana kwa misimamo ya uwazi na ukweli mna katika vipindi vya uchaguzi ndani ya chama alitumika kama gia kubwa ya kukwamua gari kwenye tope.

Mkongwe huyo alijizolea umaarufu na nyumbani kwake paligeuzwa sehemu ya tambiko la viongozi wa CCM waliotaka kugombea nafasi za uongozi,hata urais.

Kifo cha Ndejembi (86) kimewagusa si wana Dodoma pekee. CCM imetuma salamu za rambirambi ikimweleza namna alivyokuwa shupavu, a mpenda haki na mtetezi wa wanyonge.

Miongoni mwa wanaomfahamu vema na kufanya naye harakati za siasa tangu enzi za Tanu ni Balozi Mstaafu, Job Lusinde.

Mzee Lusinde mwenye makazi yake mita 100 kutoka makazi ya Ndejembi, anasema mtima wake hautakuwa na furaha wala amani, ila tu anamuombea pumziko jema mbele za Mungu.

“Mimi na Ndejembi tulifanya harakati nyingi kwa wakati huo tukiwa bado vijana. Miongoni mwa mambo atakayoendelea kuyakumbuka juu yake ni uvumilivu na moyo wa uzalendo, ambayo wakati wote alipenda kuwarithisha vijana.

Anasema hakuwahi kujikweza kwa mtu zaidi ya kupenda kujifunza na kubadilishana mawazo kabla ya kutekeleza tena bila ya kutumia nguvu.

“Hata siku moja hakujiona mkubwa kuliko mwingine, lakini roho ya huruma, uvumilivu wake na kujali wengine ndivyo vilimuongezea heshima, kwa ujumla alikuwa ni mwanasiasa wa damu,” alisema Lusinde.

Lusinde anasema vijana wanapaswa kujifunza kupitia kwa mkongwe huyo ikiwemo viongozi walioko madarakani na wale wanaotamani kuwa madarakani kwa kuwa jambo jema kwa kiongozi ni uvumilivu.

Waziri wa zamani wa Mawasiliano na Uchukuzi ambaye alipokea kijiti cha uenyekiti wa CCM mkoa wa Dodoma, William Kusila anasema kifo cha ndejembi ni pigo kubwa ambalo halielezeki.

Kauli kama hiyo inatolewa pia na Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, sera, bunge, kazi, ajira na wenye ulemavu Antony Mavunde kuwa Ndejembi ameacha pengo ambalo itamchukua muda kulisahau.

Anasema licha ya umri wake mkubwa Ndejembi aliendelea kuwa mwalimu wake katika siasa na alijua mambo mengi ambayo baadhi ya wanasiasa hawayajui.

“Mimi na mwenzangu Deo Ndejembi (Mkuu wa wilaya ya Kongwa) tulivuna mengi kupitia katika simulizi za babu yetu ambazo kwenye vitabu hatukuwahi kusoma wala kupata elimu kwa mtu mwingine, hakika imeniuma na inanigusa moja kwa moja,” alisema Mavunde.

Mbunge huyo anasema alipokuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM, kabla ya vikao alikuwa akifika kwa Ndejembi akiwa na wenzake na kumweleza wanachotaka kuwasilisha kwa maslahi ya vijana na aliwashauri namna bora ya kuwasilisha mawazo yao mbele ya viongozi.

Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Dodoma Godwin Mkanwa anasema kilichoanguka ni mlima. yeye anajiona mwenye deni kwani siasa zilizosimikwa na mkongwe huyo ni imara na hazijayumba.

“Ukisikia Dodoma ni ngome ya CCM basi ujue msingi mkubwa ni huyu mzee. Mimi nililelewa naye tangu nikiwa kijana. Katika maisha yake ustaafu, Ndejembi aliendelea kuulizia habari za chama na mipango inavyoendelea ikiwemo miradi ambayo aliiasisi na kwamba furaha yake ilikuwa kusikia utulivu ndani ya chama.

Misimamo yake

Mwaka 2015 Mwananchi ilifanya mahojiano na mzee huyo nyumbani kwake ambapo alitangaza hadharani kuwa alikuwa anamuunga mkono Edward Lowassa na kuwa alikuwa ni rafiki yake.

Lakini Lowassa alipohamia Chadema, walibaki na urafiki lakini alisema asingekuwa tayari kumpigia kampeni.

Lowassa alikuwa mmoja wa makada waliokuwa wanapewa nafasi kubwa ya kupitishwa kugombea urais kwa tiketi ya CCM, lakini jina lake liliondolewa mapema na kusababisha atangaze kujiunga na Chadema, ambayo ilimpa fursa hiyo, ikiungwa mkono na vyama vingine vitatu vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa).

Katika Uchaguzi Mkuu, John Magufuli aliyepitishwa na CCM alishinda kwa kupata kura milioni 8.8, akifuatiwa na Lowassa aliyepata kuta milioni 6.07.

Akizungumza katika mahojiano hayo Uzunguni Jijini Dodoma, Ndejembi alisema si yeye tu aliyeamua kumuunga mkono Lowassa, bali alikuwa na kundi kubwa la wana CCM ambalo liliona waziri huyo mkuu wa zamani anafaa kwa wakati ule.

“Chama kilikuwa na hali mbaya, kila tukishauri mambo hayakuwa yakienda sawa, kuanzia wanachama kwa wanachama lakini ikafika mpaka kwa viongozi na wanachama. Mparaganyiko ulikuwa mkubwa kiasi cha kukiyumbisha chama. Sisi tuliokuwa tukienda ofisi za chama za wilaya, mkoa na hata Taifa tulikuta tofauti kubwa. Watu hawataki hata kukuona, wanasema wakati wetu umepita na kuuliza tumekuja kufanya nini,” nikaona mtu wa kunyoosha alikuwa ni Lowasa.

Wakati huo alisema kama CCM kingeendelea na mambo hayo, hali ingekuwa mbaya zaidi na kupoteza ushindi dhidi ya wapinzani ambao kwa wakati huo walionekana wazi wamejipanga kutumia udhaifu wa CCM.

Ndejembi alimtaka Rais Magufuli atakapopokea kijiti cha uenyekiti wa CCM, aanze ‘kutumbua majipu’ ndani ya chama ambayo alisema yanakipeleka chama kubaya ili kuwepo na mageuzi na mapinduzi ndani ya chama hicho, kazi ambayo inafanyika hivi sasa na msemo wa majipu ulichukuliwa.



Chanzo: mwananchi.co.tz