Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nchimbi akabidhiwa mikoba, aanza na watatu Chadema

NchimbizAA8tYc.jpeg Nchimbi akabidhiwa mikoba, aanza na watatu Chadema

Tue, 23 Jan 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Katibu Mkuu wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Balozi Dk Emmanuel Nchimbi amesema chama hicho hakiwezi kukimbia mazungumzo na vyama vya upinzani kwa kuwa hakiogopi mabadiliko.

Dk Nchimbi alisema hayo jana alipohutubia wanaCCM waliojitokeza kumpokea alipowasili kwa mara ya kwanza kwenye Ofisi za Makao Makuu ya chama jijini Dodoma.

Dk Nchimbi aliwasili jijini hapa jana na kupokelewa na wanaCCM katika uwanja wa ndege.

"CCM haiwezi kususa mazungumzo na vyama vya upinzani, CCM hakiogopi mageuzi. Kuna mageuzi mengi yamefanyika ukiwamo kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi," alisema.

Alisema CCM ilikubali mageuzi ya kuanzishwa kwa mfumo wa vyama vingi vya siasa na asilimia 20 ya Watanzania ndio walikubali mfumo huo huku asilimia 80 wakikataa. "CCM haikukimbia mageuzi hayo, iliamua kukubaliana na wachache asilimia 20 na kufanya mageuzi ya kisiasa kwa kutungwa sheria iliyoanzisha vyama vingi mwaka 1992," alisema Dk Nchimbi.

Alisema matatizo mengi yanatatuliwa kwa mazungumzo na si vinginevyo, huku akitoa mfano wa tatizo la uhaba wa sukari kuwa Rais Samia Suluhu Hassan ameshachukua hatua kwa kutoa vibali kwa wafanyabiashara kuagiza sukari nje ya nchi.

“Jukumu la kujenga amani ya nchi ni letu sote, nawaomba ndugu zangu wa vyama vya upinzani washiriki jukumu hilo na kuzungumza pamoja kunapokuwa na matatizo," alisema.

Dk Nchimbi alisema atazungumza na viongozi wa vyama vya upinzani kuhusu jukumu la kuijenga nchi pamoja kwa kuwa ni marafiki zake.

Kuhusu wajibu wa wanaCCM, Dk Nchimbi alisema kwa mujibu wa Katiba ya chama, kila mmoja ana wajibu wa kukitangaza chama hicho.

Dk Nchimbi ambaye jana alikabidhiwa rasmi ofisi ya katibu mkuu na aliyekuwa akishika nafasi hiyo, Daniel Chongolo, alimpongeza kwa kazi kubwa ya kukijenga aliyoifanya.

Alisema Chongolo ameondoka na kukiacha chama kikiwa imara tofauti na kilivyokuwa nyuma.

Pia, Dk Nchimbi alisema anawakabidhi zawadi wanaCCM wa Dodoma ya viongozi watatu wa Chadema waliohamia CCM akiwemo aliyekuwa mbunge wa viti maalumu, Upendo Peneza aliyesema CCM ndiyo kwenye maendeleo.

“Sijaingia CCM kwa ajili ya mwanamke mwenzangu Rais Samia Suluhu Hassan, nimeingia CCM kutokana na maendeleo anayoyafanya ikiwemo kuleta maridhiano kwa vitendo.

“Wanamtukana lakini hajibizani na zaidi ya yote anafanya kwa vitendo aliyoyaahidi," alisema Peneza.

Alisema wakati anaingia kwenye siasa zaidi ya miaka 15 iliyopita, baba yake mzazi alimshauri ajiunge na CCM.

"Sikukubaliana na wazo la baba nikamwambia najiunga Chadema, naye alinipa baraka zake na fedha za kunisaidia. Leo (jana) nimeamua kujiunga CCM kwa kuwa ndio chama chenye mwelekeo wa maendeleo," alisema Peneza.

Alisema ajenda ya maandamano ya Chadema kuhusu miswada ya sheria ya uchaguzi iliyowasilishwa bungeni haina mashiko kwa sababu Kamati ya Bunge ya Utawala, Katiba na Sheria bado inafanyia kazi maoni yaliyotolewa.

Kwa upande aliyekuwa mwenyekiti wa Baraza la Umoja wa Vijana la Chadema Mkoa wa Manyara, Benson Andrew alisema maendeleo yanayofanywa na Serikali ya CCM chini ya Rais Samia ndiyo yamemfanya ajiunge CCM.

Alisema aliingia Chadema akiwa na miaka 12 na amekuwa mwanachama kwa zaidi ya miaka 14 hadi alipoamua kujiondoa jana.

Kiongozi mwingine wa Chadema, Onesfory Mbuya alisema amevutiwa na R nne za Rais Samia ambazo ni maridhiano, kuvumiliana, kujenga na mabadiliko.

Alisema suala la maridhiano ndio kimemvutia zaidi na kuamua kujiunga na CCM kuunga mkono juhudi zinazofanywa na Rais Samia. Alisema aliingia Chadema mwaka 2004 na aliwahi kushika nafasi kadhaa za uongozi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live