Katibu Mkuu wa chama cha Mapinduzi (CCM) Balozi Dkt. Emmanuel John Nchimbi ametoa wito kwa viongozi na makada wa chama hicho kuwa hawapaswi kujisahau kwa kuwa wao ni chama tawala ambacho kimepewa mamlaka ya kuongoza serikali zote mbili za Tanzania (Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Mapinduzi Zanzibar) hivyo wana jukumu la ulezi na kuhakikisha ustawi wa nchi unapewa kipaumbele
Balozi Dkt. Nchimbi amezungumza hayo Machi 24.2024 alipokutana na wajumbe wa mabaraza ya wazee wa CCM wilaya na mikoa kichama, Unguja Zanzibar ambapo amesema CCM inaamini kuwa uwepo wa serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) Zanzibar kunapelekea utulivu wa nchi
Amesema anaamini waliofanya maamuzi ya kuwa na serikali ya aina hiyo walifanya maamuzi ya busara yaliyozingatia maslahi ya watu kabla ya maslahi ya vyama vya siasa
Aidha, Balozi Dkt. Nchimbi amesema siku zote anapata kigugumizi kumuelewa mtu anayetoka hadharani na kudai kuwa anataka kujitoa kwenye serikali hiyo (SUK) kwa kuwa anaamini usalama, umoja na utulivu wa watu ni jambo linalopaswa kupewa kipaumbele zaidi na kwamba masuala mengine hayana maana kama masuala ya amani na utulivu hayajazingatiwa
Kufuatia hilo ametoa wito kwa viongozi na wanachama wa chama hicho (CCM) kutojifananisha na vyama vingine na kutojibizana kwa kuwa wao ni walezi wa nchi
Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar Dkt. Mohammed Saidi Mohammed (Dimwa) akizungumza kwenye hadhara hiyo amesema mabaraza ya wazee ya CCM ya ngazi mbalimbali yana wajibu wa kusimamia na kudumisha utamaduni, umoja wa kitaifa, uzalendo na malezi bora, sambamba na hilo pia wana jukumu la kushauri njia bora za kufanikisha ushindi wa CCM katika chaguzi mbalimbali.