Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nchi nne zafungua ofisi ndogo za ubalozi Dodoma

Bunge Kuarishwa (600 X 362) Nchi nne zafungua ofisi ndogo za ubalozi Dodoma

Mon, 13 May 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Serikali ya Tanzania imesema hadi sasa, nchi nne zimeshafungua ofisi ndogo za ubalozi jijini Dodoma tangu Serikali ihamishie makao makuu yake huko.

Uamuzi wa Serikali kuhamia jijini Dodoma ulitangazwa na hayati John Magufuli, Julai mwaka 2016 wakati alipopewa wadhifa wa kuwa Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) ambapo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alianza kuhamia rasmi Septemba 26, 2016.

Mchakato wa kuhamia jijini Dodoma ulifuatiwa na viongozi wengine wakuu na kuhitimishwa na Rais Magufuli Oktoba 12,2019.

Naibu Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mbarouk Nassoro Mbarouk ameyasema hayo leo Jumatatu, Mei 13, 2024 wakati akijibu swali la msingi la Mbunge wa Bahi, Ernest Nollo.

Mbunge huyo amehoji ni lini balozi mbalimbali zitahamia Dodoma kuunga mkono juhudi za Serikali kuhamia Dodoma.

Akijibu swali hilo, Mbarouk amesema Serikali kupitia Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki inaendelea kufanya jitihada za kuzishawishi balozi zote zinazowakilisha nchi zao hapa nchini kuhamia makao makuu ya nchi Dodoma.

“Tayari, Serikali imetenga eneo maalumu la kujenga ofisi za kibalozi na makazi ya waheshimiwa mabalozi na tayari hati za viwanja hivyo zimeanza kutolewa,” amesema.

Amesema Serikali inaendelea pia kuzihamasisha balozi kwa kuwafahamisha juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali za kuboresha miundombinu katika jiji la Dodoma ambayo ni muhimu kwa mabalozi hao katika utekelezaji wa majukumu yao pindi watakapohamia.

“Kutokana na juhudi hizo zipo balozi kadhaa ambazo zimeishaleta wataalamu wake ili kukagua viwanja hivyo na sasa wanaandaa michoro ya majengo watakayojenga,” amesema.

Aidha, amesema hadi sasa nchi nne zimeshafungua ofisi ndogo za ubalozi jijini Dodoma zikiwamo Ufaransa, Ujerumani, China na Uingereza pamoja na Ofisi ya Uratibu ya Umoja wa Mataifa (UN).

Chanzo: www.tanzaniaweb.live