Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nape arudi kumnadi Chiza kwa mara ya pili

10289 Pic+nape TanzaniaWeb

Mon, 6 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Kakonko. Mbunge wa Mtama mkoani Lindi, Nape Nnauye amerejea Buyungu mkoani Kigoma kwa mara ya pili kumnadi mgombea ubunge wa CCM, Christopher Chiza anayetaka kulitwaa jimbo hilo lililokuwa chini ya Chadema.

Nape ambaye ni katibu wa itikadi na uenezi wa zamani wa CCM mara ya kwanza alikuwapo jimboni hapo wakati wa uzinduzi wa kampeni Julai 26, akiwa amefuatana na katibu mkuu, Dk Bashiru Ally na katibu mkuu mstaafu Yusuph Makamba.

Makada wengine waliokwenda Buyungu kumnadi Chiza ni mbunge wa zamani wa Moshi Vijijini pia aliwahi kushika nafasi kadhaa za uwaziri, Dk Cyril Chami na aliyekuwa mbunge wa Ukonga kupitia Chadema, Mwita Waitara ambaye amekihama chama hicho na kujiunga CCM.

Safari hii Nape amerejea Buyungu akiwa na mbunge wa Korogwe Mjini mkoani Tanga, Mary Chatanda. Nape ambaye ni maarufu kwa usemi wake wa ‘bao la mkono’, juzi wakati akimnadi Chiza alisema amerudi na mkakati wa ushindi kwa mgombea huyo wa CCM.

Akizungumza katika mkutano wa kampeni uliofanyika Kijiji cha Kasuga, alisema takwimu za tathmini ya maendeleo ya kampeni jimboni Buyungu zinaonyesha kuwa CCM inaongoza kwa mvuto miongoni kwa wapiga kura na kwamba huenda chama hicho kikashinda kwa zaidi ya asilimia 70.

Nape alisema Serikali inayosimamia ilani ya uchaguzi ya CCM ndiyo inayotekeleza miradi yote inayokwenda kwa wananchi na usimamizi wa karibu katika kusukuma maendeleo unafanywa na wabunge na madiwani wa CCM, hivyo kuwataka wapinzani waeleze wapi wamefanya katika kupeleka miradi ya maendeleo kwa wananchi wakieleza gharama na chanzo cha fedha kilichotumika kugharamia miradi hiyo.

Nape alisema katika kipindi ambacho Chiza alikuwa mbunge ipo miradi mingi ya maendeleo ya wananchi iliyotekelezwa ikiwemo miradi ambayo imetekelezwa nje ya bajeti ya Serikali.

Mbunge Mary Chatanda alisema anashangazwa na viongozi wa upinzani na wagombea wao kupiga kelele za kuleta maendeleo wakati tayari kazi kubwa imefanywa na Serikali ya CCM chini ya Chiza.

Akiomba kura kwa wananchi wa Kijiji cha Nyakayenzi, Chiza aliwataka kumchagua kwa ajili ya kusimamia maendeleo yao kwani Serikali imepitisha miradi mikubwa ambayo inahitaji msimamizi makini.

Aliitaja baadhi ya miradi hiyo ni uboreshaji wa barabara za wilaya kwa kiwango cha changarawe iliyotengewa Sh621 milioni na ujenzi wa madarasa kwa ajili ya shule za msingi na sekondari iliyotengewa Sh264 milioni.

Chanzo: mwananchi.co.tz