Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nape anapojipambanua kwa deni la taifa

Napepic Nape Nnauye, Mbunge wa Jimbo Mtama

Thu, 11 Nov 2021 Chanzo: mwananchidigital

Novemba 2017, Nape Nnauye, mbunge wa Mtama (CCM) alikuwa mbogo bungeni akihoji kuhusu nidhamu ya Serikali katika ukopaji. Miaka minne baadaye (Novemba 2021) Nape anaendelea kushikilia hoja hiyo.

Nape, anataka Serikali iliyopita, chini ya Dk John Magufuli ichunguzwe ili taifa lipewe taarifa sahihi kuhusu kiasi kilichokopwa na matumizi yake. Alichokijengea ukosoaji ni jinsi Serikali iliyopita ilivyozingirwa na usiri.

Upande wa pili, anaisifu Serikali ya sasa chini ya Rais Samia Suluhu Hassan, kwamba imeonyesha wajibu kupitia mkopo wa Sh1.3 trilioni kutoka Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF).

Turejee bungeni Novemba 2017, wakati wa mjadala wa Mpango wa Maendeleo ya Taifa kwa mwaka 2017-2018, Nape alizungumzia kasoro ya Serikali kutoishirikisha sekta binafsi katika miradi inayoweza kujiendesha kibiashara, badala ya kuendelea kukopa, kitu ambacho alionya kwamba kitakuja kusababisha athari kubwa kwa nchi.

Jambo la kwanza Nape alisema kuwa Serikali inakopa fedha nyingi kwa ajili ya miradi mikubwa ambayo ukamilikaji wake unachukua muda mrefu, wakati mikopo husika marejesho yake yanafanyika ndani ya muda mfupi. Kutokana na hali hiyo, alitahadharisha kwamba marejesho yataathiri miradi mingine.

Nape alisema kwa vile miradi itachelewa kukamilika, wakati wa marejesho ya mikopo itabidi kuchukua fedha kwenye miradi ya huduma kama elimu, afya na kadhalika ili kuwalipa wadeni wa nchi. Katika hili Nape alisema anatilia shaka uzalendo wa wachumi ambao walikuwa wakimshauri Dk Magufuli.

Upande wa pili, Nape alionya kuwa nchi inapiga hatua kwenda kuwa isiyokopesheka ikiwa itakopa kwa ajili ya miradi miwili tu; wa kwanza ni ujenzi wa reli ya kisasa (standard gauge) dola 15 bilioni (Sh33.8 trilioni) na wa ufuaji umeme wa Stiegler’s Gorge megawati 2,100 dola 5 bilioni (Sh11.27), jumla dola 20 bilioni (Sh45 trilioni).

Nape alisema taarifa za Mpango mpya zinaeleza Deni la Taifa limefikia dola 26 bilioni (Sh58.6 bilioni) sawa na asilimia 32 ya uhimilivu wa deni. Kwamba ili Tanzania ifikie kikomo cha kukopeshwa, deni lake linapaswa kufikia dola 45 bilioni (Sh101.4 trilioni).

Kutokana na hoja hiyo ya Nape, endapo Serikali itaongeza mkopo kwa miradi miwili tu ya standard gauge na Stiegler’s Gorge, deni litafikia dola 46 bilioni (Sh103.7 trilioni), yaani ongezeko la Sh2.3 trilioni kutoka kwenye kiwango chake cha mwisho cha kukopa.

Tuje Novemba 2021

Wakati wa mjadala wa hoja ya Mpango wa Maendeleo ya Serikali 2022-2023, Nape amehoji ukuaji wa deni la taifa ambalo limefikia Sh78 trilioni. Anataka ukaguzi maalumu ufanyike.

Nape alipozungumza kwa mara ya kwanza Novemba 2017, hakuwa na maajabu yoyote, maana wabunge wengi huzungumza mambo ya msingi. Hoja yake ya Novemba 2021, ni kielelezo cha jinsi anavyosimamia agenda.

Kuzungumza mara ya kwanza bungeni inawezekana ni upepo tu unapita. Kurejea tena na tena ni kipimo tosha kwamba mtoa hoja ana agenda anayoisimamia. Na hivyo ndivyo Bunge linavyotaka.

Hoja nzuri ni ile yenye mwendelezo. Inatolewa leo na inafuatiliwa mpaka kupata matokeo yake. Kujenga hoja halafu unaiacha njiani bila kujua nini kitatokea, ni kielelezo cha namna mtoa hoja asivyo na agenda.

Tatizo kubwa linalolitesa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ni wabunge kukosa agenda. Wapo bungeni lakini huoni wanachokisimamia. Hawaanzishi mjadala wala hawasimamii agenda yoyote.

Bunge linahitaji wabunge wengi ambao watakuwa na agenda zao, ama kwa ajili ya masilahi ya nchi moja kwa moja au zenye kulenga majimbo na maeneo yao ya uwakilishi. Hivyo ndivyo italeta maana ya kuisimamia serikali.

Bunge linatakiwa lipate wabunge wengi ambao kwa kuwatazama mmoja-mmoja au kwa makundi, unafahamu wana agenda gani wanaisimamia. Kazi ya ubunge ina thamani kubwa na inatakiwa mwenye kuipata aitendee haki.

Mbunge anatakiwa kuiona kesho ya nchi au jimbo lake kama agenda yake itafanikiwa. Kwa hiyo anaweka mkazo kuhakikisha kwa jua na mvua, agenda yake inapata kusikika na kuungwa mkono na wengine.

Bunge lina siasa nyingi, kama husimamii agenda yako kikamilifu, utakuwa kila mara unayumba, unamaliza miaka mitano, unaulizwa ulifanya nini, unaishia kutaja orodha ya maswali uliyouliza bungeni na michango uliyotoa. Hata hivyo, hakuna agenda mahsusi uliyosimamia. Nape anasimamia agenda ya deni la taifa.

Chanzo: mwananchidigital