Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Nape: Mikutano ya hadhara ni demokrasia

NAPE Mojaa.jpeg Nape Nnauye, Waziri wa Habari

Wed, 19 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye akisema mikutano ya hadhara ya vyama vya siasa ina afya na demokrasia kwa Taifa, wachambuzi wa masuala ya siasa wamekubaliana na hoja hiyo wakisema mikutano hiyo ni sawa na kioo kwa watawala kujitizama.

Nape aliyewahi kuwa katibu wa itikadi na uenezi wa CCM, ametoa kauli hiyo ikiwa ni zaidi ya miaka sita tangu Serikali ilipopiga marufuku mikutano hiyo, ikiache ile ya wabunge na madiwani katika maeneo yao.

Serikali ilizuia mikutano hiyo baada ya kumalizika kwa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2015 ikisema siasa hufanywa wakati wa uchaguzi na baada ya hapo huruhusu shughuli nyingine za maendeleo kuendelea.

Hatua hiyo ilizua malalamiko kutoka kwa vyama vya siasa na wadau wa demokrasia wasema Katiba na Sheria ya Vyama vya Siasa imekiukwa na kuitaka Serikali iondoe zuio hilo, jambo ambalo halikutekelezwa hadi sasa.

Kufuatia kelele za mara kwa mara Desemba 15 mwaka jana, Rais Samia akifungua mkutano wa wadau wa demokrasia ya vyama vingi nchini, miongoni mwa aliyoyaeleza ni suala mikutano hiyo na uwezekano wa kuiruhusu baada ya kupata maoni ya wadau.

Aliwataka wadau wajadili na kuja na mapendekezo ya namna bora ya kufanya mikutano hiyo akisema “vyama mna haki ya kikatiba kufanya mikutano, kunadi sera zenu lakini mnaivunja wenyewe, hakuna atakayekubali anaongoza nchi anatoa kibali mfanye mkutano mnapita kuvunja magari ya watu na kufanya vurugu.”

Jana, akiwa kwenye mahojiano katika kipindi cha ‘Joto Kali la Asubuhi’ kinachorushwa na E-TV, Nape alisema anaamini mikutano vya vyama vya siasa ingeiimarisha CCM zaidi kuliko hali ilivyo kwani ukiwa unaongoza bila kuwa na mtu anayekusema ni rahisi kujisahau kwa sababu ni binadamu.

“Wakiwa watu wanawasemasema… ‘mara hili jambo sio sawa, mara kodi… ohh hivi’, mnarudi ndani mnakaa.

“Yapo mambo CCM tumeyabadilisha kwa kuwasikiliza jamaa wanavyopiga kelele, wanapiga kelele mnawabishia, lakini mkirudi ndani mnasema hili linafikirisha lifanyiwe kazi,” alisema.

Nape alisema hayo alipokuwa akizungumzia mwenendo wa hali ya siasa wa sasa ukilinganishwa na wakati akiwa katibu wa itikadi na uenezi.

Akizungumzia kauli hiyo ya Nape Mkurugenzi wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Bob Wangwe alisema ingawa mwanasiasa huyo amechelewa kutoa kauli hiyo, lakini alichokisema kipo sahihi kwa kuwa mikutano ya hadhara ipo kikatiba na si hisani.

“Amezungumza ukweli kabisa…Serikali inayotaka kujitizama haiwezi kutumia kioo chake isipokuwa kioo kingine ambacho ni wapinzani,” alisema Wangwe.

Anachokisema Wangwe kinaungwa mkono na Dk Onesmo Kyauke, mwanasheria aliyesema zuio la mikutano ya hadhara halipo kisheria bali lilitolewa kisiasa na kwamba ifike wakati Serikali iheshimu Katiba kwa kuruhusu mchakato huo kuendelea kama miaka ya nyuma.

“Mikutano ya hadhara ni muhimu kwa sababu inasaidia kuimrisha vyama ili kuendelea kuwa hai hasa kwa kupata wanachama wapya na kuendesha vikao vya kikatiba na chaguzi,” alisema

Katibu Mkuu wa ACT-Wazalendo, Ado Shaibu alisema, “nakubalina na mawazo ya Nape kuhusu mikutano ya hadhara kwa sababu ndiyo nyenzo ya watawala kupata changamoto kutoka kwa vyama vya upinzani.”

Ado anaungwa mkono na Naibu Katibu Mkuu wa Chadema-Zanzibar, Salum Mwalimu aliyesema mikutano ya hadhara inaleta ustawi wa demokrasia na uhuru wa wananchi kutoa maoni kuhusu mwenendo wa Serikali.

Katibu Mkuu wa CUF, Hamad Masoud Hamad alisema mikutano ya hadhara ni sehemu ambayo vyama vya siasa kupata wanachama wapya na kunadi sera zao.

Kwa upande wake Katibu Mkuu wa Baraza Kuu la Waislamu Tanzania (Bakwata), Nuhu Mruma alisema mikutano ya hadhara ni jambo muhimu kwa sababu watu wanatoa maoni yao na kusikiliza sera za vyama husika.

“Kikubwa watu wafuate utaratibu na sheria zilizowekwa kuhusu mchakato huu. Kama kuna sehemu kuna madhaifu au changamoto basi zirekebishwe ili iendelee,” alisema Mruma.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live