Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Naibu meya Ilala ataja sababu za kuhama CUF, madiwani waendelea kutimka

9647 Meya+pic TanzaniaWeb

Thu, 2 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Siku chache baada ya wabunge wawili wa Chadema kutangaza kujiuzulu nyadhifa zao na kuhamia CCM, madiwani wengine wawili wa chama hicho wametangaza kufuata nyayo zao.

Wiki iliyopita mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara alitangaza kujiunga na CCM na Julai 31 usiku, mbunge wa Monduli kupitia chama hicho, Peter Kalanga alitangaza kujiuzulu wadhifa huo na kutimkia CCM.

Juzi, Diwani wa Vingunguti (CUF), Omary Kumbilamoto alijiuzulu huku akitaja sababu nne zilizomfanya kuchukua uamuzi huo ikiwamo mgogoro ndani ya chama chake. Kumbilamoto pia alikuwa naibu meya wa Manispaa ya Ilala.

Hata hivyo, jana diwani wa Kizota jijini Dodoma (Chadema), Jamala Ngalya alijiuzulu na kuhamia CCM.

Sababu nne za Kumbilamoto

Kumbilamboto alitangaza uamuzi wa kujiuzulu na kutaja sababu nne ikiwamo mgogoro ndani ya CUF unaomkwaza kutekeleza majukumu yake.

Pia alisema viongozi wa CUF walishindwa kujitokeza katika kata yake kumsaidia lilipotokea janga la mafuriko mwaka huu.

Sababu nyingine ameitaja kuwa ni kupewa vitisho vya kufukuzwa uanachama kwa kile alichodai kuwa karibu na mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda.

Akifafanua sababu hizo, Kumbilamoto ambaye anamuunga mkono katibu mkuu wa CUF, Maalim Seif ameufananisha mgogoro ndani ya chama hicho na ule wa mataifa ya Palestina na Israel ambao umekosa suluhu.

“Mvutano huo umesababisha nishindwe kutimiza wajibu wangu kwa ufanisi huku napewa vitisho vya kufukuzwa uanachama kwa sababu ya kuwa karibu na viongozi wa Serikali akiwamo mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Paul Makonda,” alisema.

Alisema wakati Kata ya Vingunguti ilipokumbwa na mafuriko hakuna kiongozi wa CUF aliyekwenda kutoa msaada wala kuitembelea isipokuwa uongozi wa Serikali wa mkoa.

“Sikuletewa hata kijiko na viongozi wangu wa chama, lakini viongozi wa Serikali walinisaidia. Hata hivyo upande wangu wa chama unaniambia mimi ni msaliti kutokana na ushirikiano ninaoupata (serikalini),” alisema.

Alisema wakati wowote atafanya mkutano wa hadhara kuwaeleza wananchi wa kata hiyo chama anachokwenda kufanyia shughuli zake za kisiasa na amewaachia wana CUF chama chao.

Meya wa Ilala, Charles Kuyeko alisema, “nimesikia kama ulivyosikia wewe, lakini hajaniaga na wiki nzima nilikuwa namtafuta simpati.”

Wakati huohuo, diwani wa Kizota (Chadema), Ngalya ametangaza kujiuzulu wadhifa huo na kujiunga na CCM.

Akizungumzia uamuzi huo, Ngalya alisema anarudi nyumbani kwa kuwa waliomkata wakati wa Uchaguzi Mkuu 2015 ndani ya CCM kwa sasa hawapo madarakani.

Diwani huyo ambaye hivi karibuni alichaguliwa kuwa mnadhimu wa madiwani wa Chadema Tanzania, alisema uamuzi wake ni ‘huru’ na anaungana na timu ya Rais John Magufuli ili kuchapa kazi.

Chanzo: mwananchi.co.tz