Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NEC yawarejesha wengine 19 kugombea ubunge, 26 udiwani

Eb909771a94698155eaf9bcebc566c9c NEC yawarejesha wengine 19 kugombea ubunge, 26 udiwani

Thu, 10 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekubali rufaa za wagombea ubunge 19 na kuwarejesha katika orodha ya wagombea. Pia, tume hiyo imekubali rufaa 26 na kuwarejesha wagombea husika katika orodha ya wagombea udiwani.

Taarifa iliyotolewa Dodoma jana na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk Wilson Mahera ilisema NEC iliketi juzi na kupitia, kuchambua na kufanya uamuzi wa rufaa 67, ambapo 22 ni za wagombea ubunge na 45 za wagombea udiwani.

Mahera alieleza kuwa Tume hiyo imekubali rufaa 19 za wagombea ubunge na kuwarejesha katika orodha ya wagombea.

Rufaa hizo ni kutoka majimbo ya Tunduru Kaskazini, Nyasa na Songea Mjini mkoani Ruvuma, Mbeya Vijijini mkoa wa Mbeya, Karagwe mkoani Kagera, Ulanga mkoa wa Morogoro, Chemba mkoa wa Dodoma, Tanga na Muheza mkoani Tanga, Kibamba, Ubungo na Kigamboni mkoani Dar es Salaam, Same Mashariki mkoa wa Kilimanjaro, Buhigwe mkoa wa Kigoma, Mufindi Kusini mkoa wa Iringa na Tabora Kaskazini mkoa wa Tabora.

Kuhusu wagombea udiwani, Mahera alisema alisema Tume hiyo imekubali rufaa 26 na kuwarejesha wagombea husika katika orodha ya wagombea udiwani.

Alitaja rufaa hizo 26 zilizokubaliwa, majina ya Kata na majimbo kwenye mabano kuwa ni: Kingolwira, Kilakala, Mindu, Uwanja wa Taifa, Tungi, Kiwanja Cha Ndege na Mbuyuni (Morogoro Mjini), Bugene na Igurwa (Karagwe Mjini), Kihanga na Ndama (Karagwe), Bwera (Chato), Mzingani na Magaoni (Tanga), Central (Tanga Mjini), Bukindo, Muriti, Namagondo na Kakukuru (Ukerewe), Kitangiri, Ilemela, Buzuruga (Ilemela), Kerege (Bagamoyo) na Chemchem(Kondoa Mjini).

“Tume imekataa rufaa 3 za kupinga wagombea ubunge walioteuliwa. Rufaa hizo ni kutoka majimbo ya Kalambo, Kigamboni na Muheza” alisema Mahera.

Pia, Mahera alisema Tume hiyo imekataa rufaa 3 za kupinga madiwani walioteuliwa. Rufaa hizo ni kutoka Kata za Ipwani (Mbarali), Ilemela (Ilemela) na Kichangani (Ulanga).

Alisema pia Tume hiyo imekataa rufaa 16 za wagombea udiwani ambao hawakuteuliwa. Mahera alifafanua kuwa jumla ya rufaa za wagombea ubunge, zilizofanyiwa uamuzi na Tume hadi sasa ni 111 na za wagombea udiwani ni 45.

“Tume itaendelea kutoa matokeo baada ya usajili na uchambuzi wa rufaa hizo. Wahusika wa rufaa hizo wameanza kujulishwa kwa barua juu ya uamuzi wa Tume” alisema.

Kwa uamuzi huo wa Tume kukubali rufaa zingine 19 za ubunge, sasa jumla ya rufaa zote za wagombea ubunge zilizokubaliwa ni 47, ambapo awamu ya kwanza Tume ilikubali rufaa 15 na awamu ya pili ilikubali na kuwarejesha wagombea ubunge 13

Chanzo: habarileo.co.tz