Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NEC yarudisha wengine 25 kugombea udiwani

5de4708e141fe178ac51bc222272690b NEC yarudisha wengine 25 kugombea udiwani

Mon, 14 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imezifanyia kazi rufaa 50 zikiwemo nne za wagombea ubunge waliopinga kutenguliwa uteuzi wao katika Jimbo la Babati Mjini.

Kwa NEC kuzikataa rufaa hizo, wahusika wataendelea kutokuwa kwenye orodha ya wagombea katika jimbo hilo.

Aidha, NEC juzi imechambua na kufanya uamuzi kuhusu rufaa 46 za wagombea udiwani; imezikubali rufaa 25 na kuwarejesha wagombea katika orodha ya kugombea.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk Wilson Mahera alibainisha hayo katika taarifa iliyotolewa Dar es Salaam jana.

Taarifa ilieleza kuwa, NEC imekataa rufaa 12 za wagombea udiwani ambao hawakuteuliwa. "Pia, tume imekataa rufaa tisa za kupinga wagombea wa udiwani walioteuliwa,"ilieleza taarifa hiyo na kuongeza: "Tume itaendelea kutoa matokeo baada ya usajili na uchambuzi wa rufaa kila siku na wahusika wa rufaa hizo watajulishwa kwa barua juu ya uamuzi wa tume."

Kwa kuzingatia taarifa hiyo, hadi sasa NEC imefanya jumla ya rufaa za wagombea ubunge zilizofanyiwa uamuzi kufikia 117 na zile wa wagombea wa udiwani kufikia 195.

Tume imepokea rufaa 557 kutoka kwa wagombea ubunge na udiwani kuhusu uteuzi wa wagombea wa nafasi hizo katika Uchaguzi Mkuu wa Mwaka 2020 wa rais, wabunge na madiwani unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28, mwaka huu.

Rufaa hizo zimewasilishwa chini ya Kifungu cha 40(6) cha Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, Sura ya 343 kikisomwa pamoja na Kifungu cha 44(5) cha Sheria ya Uchaguzi ya Serikali za Mitaa, Sura 292 kinachotoa fursa kwa wagombea ubunge na udiwani kukata rufaa wanapokuwa hawajaridhisha na uamuzi wa wasimamizi wa uchaguzi kutokana na pingamizi zilizowasilishwa.

Pia, chini ya Kanuni ya 32 (3) ya Kanuni za Uchaguzi wa Rais na Wabunge za Mwaka 2020, ikisomwa na Kanuni ya 30 (3) ya Kanuni ya Uchaguzi wa Serikali za Mitaa (madiwani) za mwaka 2020.

Chanzo: habarileo.co.tz