Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NEC yapigilia msumari wa mwisho uchaguzi mdogo Korogwe

14162 Pic+nec TanzaniaWeb

Tue, 28 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), imepigilia msumari wa mwisho katika sakata la uchaguzi mdogo wa ubunge wa Jimbo la Korogwe Vijijini baada ya kutamka kuwa mgombea Timotheo Mzava (CCM), amepita bila kupingwa.

Akizungumza jijini Dodoma leo katika ufunguzi wa mafunzo kwa wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi wa kata na majimbo utakaofanyika Septemba 16, Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), Jaji Semistocles Kaijage amesema mbali na mgombea huyo wa ubunge, wengine waliopita bila kupingwa ni waliokuwa wagombea wa nafasi za udiwani katika kata 10.

Jaji Kaijage amesema kata zitakazoingia sasa katika kinyang’anyiro hicho cha uchaguzi ni 13 na majimbo ya Monduli, Arusha na Ukonga lililoko Jijini Dar es Salaam.

Katika hatua nyingine, mwenyekiti huyo amewataka wasimamizi wote wa uchaguzi mdogo wa majimbo na kata wanaoshiriki mafunzo hayo, kwenda kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia matakwa ya katiba, sheria na kanuni zinazosimamia uchaguzi.

Amewaonya kuacha kwenda kufanya kazi kwa mazoea ili wapunguze au kuondoa  malalamiko mengi yanayojitokeza wakati wa uchaguzi.

Amesema uchaguzi ni mchakato unaojumuisha hatua na taratibu mbalimbali zinazopaswa kufuatwa na kuzingatiwa huku akisisitiza kuwa hatua na taratibu hizo ndiyo msingi wa uchaguzi mzuri wenye ufanisi ambao hautakuwa na malalamiko au vurugu.

 “Tunakutana hapa kwa siku tatu ili kwa pamoja tubadilishane uzoefu, tujadili namna ya kufanikisha kazi hii ya uchaguzi, lakini pia namna ya kukabiliana na changamoto mbalimbali zinazoweza kujitokeza katika hatua zote za uchaguzi,” amesema Jaji Kaijage.

 

Amewataka waepuke madhara yanayotokana na ukiukaji wa sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi  na amesisitiza katika kipindi hiki ambacho uchaguzi mdogo unafanyika katika mazingira ambayo yana hamasa kubwa ya kisiasa, kutoaminiana kwasababu  hutawaliwa na mihemko ambayo ni chanzo cha uvunjifu wa amani.

 

“Ninyi meaminiwa na kuteuliwa katika nafasi hizi za usimamizi wa uchaguzi kwa kuwa mna uwezo wa kufanya kazi hii, hivyo mjiamini na kujitambua,” amesema.

Ametoa wito kwao kuhakikisha wanayaelewa vema maeneo yao ya kazi na kuhakikisha wanawatumia vizuri wasaidizi wao ili wapate matokeo mazuri yasiyoacha maswali kwa wapigakura.

“Mjue mna jukumu la kuimarisha imani ya wananchi pamoja na wadau wote wa uchaguzi. Mkafanyekazi kwa ufanisi bila kuegemea upande wowote. Kufanya kazi kwa uhuru na kwa uwazi kutawasaidia kudumisha amani katika maeneo yenu ya uchaguzi.”

 

 

Chanzo: mwananchi.co.tz