Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NEC yaongeza vituo vya kupigia, majimbo bado

45159 Pic+nec NEC yaongeza vituo vya kupigia, majimbo bado

Wed, 6 Mar 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imeongeza vituo vya kupigia kura kutoka 36,549 vya mwaka 2015 hadi 37,407 ikiwa ni maandalizi ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Licha ya kuongezeka kwa vituo hivyo, Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk Athumani Kihamia alisema bado hawajafikiria kuongeza majimbo.

“Majimbo hayahusiani na uboreshaji, yanahusiana tu na uchaguzi, ndiyo maana hatujazungumzia hiyo. Wakati ukifika tutajua.”

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam katika ufunguzi wa mkutano wa mabadiliko ya kanuni za uboreshaji wa Daftari la Kudumu la Wapigakura la 2008, Mwenyekiti wa NEC, Jaji Semistocles Kaijage alisema lengo la kuongeza vituo ni kuondoa kero zilizojitokeza kwenye uchaguzi mkuu uliopita.

Pia alisema vituo 6,208 vimebadilishwa majina na 817 vimehamishwa kutoka kijiji/mtaa mmoja kwenda mwingine.

“Vituo 19 vimeongezwa kutoka kata moja kwenda nyingine. Matokeo ya uhakiki wa vituo vya kupigia kura kwa Tanzania Zanzibar yanaonyesha vituo vimeongezeka kutoka 380 hadi vituo 407,” alisema Jaji Kaijage.

Hata hivyo, katibu mkuu wa CCK, Renatus Muabhi alihoji ongezeko la vituo akisema limekuja kabla ya daftari kuboreshwa, “vituo vya kupigia kura tunategemea viwe vingi, lakini huwezi kuongeza kabla ya kujua namba halisi unayofanya marekebisho. Sasa unapoongeza kutoka 36,000 hadi 37,000 umejuaje? Ni nini kilichokupa uhakika kwamba hivyo vituo vitakidhi idadi ya wapigakura?” alihoji Muabhi.

Katibu wa Itikadi na Uenezi wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu alihoji kuhusu kanuni inayowataka kupeleka ripoti zao NEC, “kipo kifungu humu kinasema waangalizi wa uchaguzi hawapaswi kutoa taarifa kwa umma mpaka ifikishwe kwa Tume iwe ‘approved’ ndipo itoke kwa umma. Sasa eneo hilo unalifanya zoezi la uchaguzi liwe kizani.”

Katibu mkuu wa Chadema, Dk Vincent Mashinji alisema wasimamizi wa uchaguzi hawapaswi kuwa watumishi wa umma kwa kuwa wana masilahi na mwajiri wao.

Katibu mkuu wa ADC, Don Mnyamani alisema kisheria daftari lilitakiwa kuboreshwa mara mbili ndani ya miaka mitano njambo ambalo Dk Kihamia alisema bado hawajachelewa.

“Daftari hilo lilipaswa kuboreshwa miezi 36 baada ya mwaka 2015 na kabla ya uchaguzi wa 2020. Kwa sasa ukitokea uchaguzi mdogo watu wengi hawatapiga kura kwa kuwa majina yao hayamo,” alisema.

Mkurugenzi wa uchaguzi, Athumani Kihamia alikanusha akisema bado hawajachelewa.

Hata hivyo Mwenyekiti wa NEC Jaji Kaijage akijibu malalamiko hayo alikanusha tume kuhodhi taarifa za waangalizi na kuziwasilisha kwenye tume hiyo hakumaanishi kuwa zitakubaliwa au kukataliwa.

Kuhusu watumishi wa umma, Jaji Kaijage alisema kanuni hizo zimetungwa kutokana na sheria mama ya uchaguzi ambayo ni sheria ya Uchaguzi ya Taifa sura ya 343.

Naye Mkurugenzi wa Uchaguzi, Kihamia alisema tume haijachelewa kufanya uhakiki wa Daftari la Kudumu la wapiga kura.

“Ili useme tumechelewa lazima ile tarehe ya uchaguzi iwe imefika halafu hatujafanya. Kwa hiyo hata ingekuwa bado miezi minne, bado hatiujachelewa. Kwa hiyo hizo ni hisia tu,”



Chanzo: mwananchi.co.tz