Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NEC yamwita Lissu

8c0b74fbe6a31e13eeeb72d32fc94d36 NEC yamwita Lissu

Mon, 28 Sep 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imemtaka mgombea urais kupitia Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA),Tundu Lissu afi ke kutoa ushahidi katika Kamati ya Kitaifa ya Maadili.

Ushahidi huo unahusu kauli aliyoitoa mjini Musoma kuwa Rais Dk John Magufuli amekutana na wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo yote jijini Dodoma, kupanga mkakati wa kuhujumu uchaguzi, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 28 mwaka huu.

Mkurugenzi wa Uchaguzi wa NEC, Dk Willson Mahera jana aliwaeleza waandishi wa habari jijini Arusha kuwa Lissu anatakiwa afike kesho Septemba 29 mwaka huu kuthibitisha kauli hiyo, vinginevyo taratibu na kanuni za uchaguzi zitachukuliwa dhidi yake.

Dk Mahera alisema Septemba 26 mwaka huu Lissu akiwa Musoma katika mikutano ya kampeni, alisema Rais Magufuli Septemba 25 mwaka huu na Septemba 26 mwaka huu, aliitisha kikao Dodoma na kukutana na wasimamizi wa uchaguzi wa majimbo yote.

Alisema mbali ya hilo, Septemba 25 mwaka huu, Lissu alisambaza taarifa mitandaoni zikisema Rais Magufuli alifanya kikao na Mkurugenzi wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi na wasimamizi wa uchaguzi mjini Dodoma.

Mahera alisema siku zilizotajwa na Lissu, alikuwa katika ziara za kikazi kukagua na kuratibu maandalizi ya uchaguzi katika majimbo ya Mkoa wa Manyara, Arusha na Kilimanjaro na mikoa mingine alikopita amekutana na na wasimamizi wa uchaguzi katika maeneo yao ya kazi. Alisema hali hiyo inadhihirisha wazi kuwa taarifa zilizotolewa na Lissu, zina lengo baya kwa nchi na halitakubalika.

Dk Mahera alisema NEC inawasihi wagombea wa vyama vyote kufuata sheria, kanuni na taratibu za nchi ili kulinda amani ya nchi katika kipindi cha kampeni kilichobaki kwa kujali muda wa kampeni, ratiba ya kampeni na kuepuka matusi, tuhuma zisizo na ushahidi zenye lengo la kuwadanganya Watanzania ili kupata kura za huruma.

Alisema NEC imekumbana na changamoto kutoka kwa baadhi ya wagombea wa kiti cha urais za kutoheshimu sheria, taratibu na maadili ya uchaguzi ikiwemo baadhi yao kutumia maneno ya kukashifu wagombea na tume yenyewe, pia kutoa taarifa zisizo za kweli zenye lengo la kuleta taharuki miongoni mwa Watanzania.

Aliwaonya baadhi ya wagombea katika kampeni, kujiona tayari wameshashinda na kuwaaminisha Watanzania kuwa wasipotangazwa, waingie barabarani kuvunja amani, kwani ni kosa kubwa kuvunja sheria na kuvuruga amani ya nchi na hilo halitavumiliwa, kwani sheria kali itachukuliwa dhidi yao.

Alisema NEC ndio yenye mamlaka kisheria ya kutangaza matokeo ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani siku ya uchaguzi. Alisema tume inawaonya wagombea kutopotosha Watanzania na kuwajengea taswira kuwa wamekwishashinda na kwamba Tume ya Taifa ya Uchaguzi itawaibia kura.

Dk Mahera alisema tabia hiyo ni mbaya, yenye lengo la kuvuruga amani ya nchi. Aliwataka waandishi wa habari kutokubali kuingia katika mtego huo wa baadhi ya wagombea wa kuwataka kutangaza matokeo kinyume na taratibu na sheria ili wasije kuchukuliwa hatua za kisheria.

Alisema kitendo cha baadhi ya wagombea urais kuikashifu NEC kwamba itaiba kura ni kitendo cha kuidhalilisha, chenye lengo la kuitisha tume ili isifanye kazi zake kwa uhuru na hilo halitakubalika. Dk Mahera aliwaasa Watanzania kuwapuuza wagombea wa aina hiyo.

Chanzo: habarileo.co.tz