Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NCCR yataka kampeni za kistaarabu, yakemea matusi

66038c5c8ad39f499166998730242d1b NCCR yataka kampeni za kistaarabu, yakemea matusi

Sat, 8 Aug 2020 Chanzo: habarileo.co.tz

CHAMA cha NCCR-Mageuzi kimesema kimejipanga kufanya kampeni za kistaarabu na kujitofautisha na vyama vingine vya siasa kwa kuepuka lugha za matusi, kejeli na dhihaka wakati wa kuomba kura kwa wananchi.

Mwenyekiti NCCR-Mageuzi, James Mbatia alitoa msimamo huo jijini Dar es Salaam jana wakati wa mkutano mkuu wa chama na kusisitiza kuwa watahakikisha kampeni zinaendeshwa kwa kuzingatia ilani ya uchaguzi ya chama hicho.

Mbatia alisema malengo ya chama ni kuendelea kuifanya Tanzania kuwa sehemu nzuri ya kuishi kwa kutumia ndimi zake kikamilifu kwa kuwa kina maono chanya ya kimaendeleo hivyo hakiwezi kufuata mkumbo kueneza siasa chafu

Alisema NCCR-Mageuzi ni chama cha Watanzania na siyo taasisi ya watu fulani hivyo ni lazima kuwa na ushirika wenye utulivu utakaosaidia kuwa na ushindani wenye amani wala mapigano inapokuja suala la kuhakikisha nchi inakuwa mahala salama.

"Ushirika wenye maslahi mapana kuliko ushindani usio na tija vyote ndiyo malengo yetu. Kila mmoja kwa nafasi yake watusaidie ili tuweze kusonga mbele, Watanzania wanahitaji maendeleo na kuiona Tanzania ikisonga mbele," alisema Mbatia.

Akizungumza Mwenyekiti wa Kamati ya Amani Maridhiano inayoundwa na viongozi wa dini, Shehe Alhad Mussa alisema mwenendo wa chama hicho cha siasa umeonesha kujali utu, uzalendo pamoja na kujitoa huku kikifanya siasa safi zinazowapa afya Watanzania.

Kiongozi huyo wa dini ambaye alikuwa miongoni mwa waalikwa kwenye mkutano huo wa NCCR Mageuzi, alisisitiza kuwa kufanya hivyo ni kuonesha umuhimu wa maendeleo na ni ukomavu wa kisiasa unaoonyeshwa na Mbatia na chama chake.

"Nchi hii lazima iongozwe na watu wenye uchungu na wazalendo, hatutokubali kuona inaongozwa na watu wanaoweza kutumika na mabeberu, ni lazima iongozwe na wazalendo kwa kuwa hao ndio pekee wana uchungu na nchi yao"

Aliendelea: "Tunataka kuona chama chenye mwelekeo na matendo kama NCCR-Mageuzi ambacho kinapambana kwa siasa safi, lugha nzuri ya staha, bila kufikiria umwagaji wa damu wala uvunjifu wa amani, tunataka kuona vyama vya siasa vya aina hii."

Alisema akiwa Mwenyekiti wa Kamati ya amani mkoa wa Dar es Salaam na mwanzilishi wa kamati za amani Tanzania, wanapenda kuona vyama vya siasa za kistaarabu, kuheshimu sheria, desturi, kuheshimu mamlaka mbalimbali na kusisitiza kuwa hiyo ndiyo siasa inayotakiwa.

Alisema ni lazima iongozwe na watu wenye uzalendo na si wanaotumika na mabeberu. “Kimeonesha kuwa ni chama safi chenye mWelekeo mzuri katika uongozi…Sisi kama viongozi wa dini tunapenda kuona vyama vya siasa vinavyofuata NCCR –Mageuzi.”

Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza, alisema Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa inafarijika kuona NCCR-Mageuzi kikionesha ustaarabu katika utekelezaji wa majukumu yake.

Aliviasa vyama vingine vya upinzani kuacha lugha za vitisho badala yake vifanye siasa safi wakati wote na vikiona vinaonewa vinapaswa kufuata hekima na utaratibu.

Alisema vyama vinapaswa kujiangalia kwanza wajibu wao wakati wa utekelezaji wa majukumu. Alisema anafarijika anapoona vyama vya siasa vinaelezana ukweli.

Aliwataka viongozi wa vyama vya siasa kuacha kuwa chanzo cha migogoro na viache kutoa lugha za uchochezi . Alivitaka vitumie muda uliopo kufanya kampeni za kistaarabu kuwezesha taifa kufanya uchaguzi wake kwa uhuru na uwazi.

Mkurugenzi wa Taasisi ya Mwalimu Nyerere, Joseph Butiku alisema vyama vyote vilianzishwa kwa malengo ya kuhudumia Watanzania na siyo kujihudumia vyenyewe.

"Siyo kazi yao kuvuruga, bali kulinda haki ya kila mtu na siyo kuvuruga misingi ya taifa iliyopo hivyo kila chama ni lazima kihakikishe kinatekeleza ipasavyo majukumu yao," alisema Butiku.

Butiku aliitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kuhakikisha inatekeleza majukumu yake ipasavyo kwa kusimamia sheria na taratibu zake kufanikisha uchaguzi mkuu kufanyika katika utulivu na amani.

Aidha, alimpongeza Rais John Magufuli kwa hatua mbalimbali za kupambana na rushwa katika utawala wake huku akiwataka viongozi wa dini kuombea taifa kwani rushwa inaharibu haki ya wananchi.

Butiku pia alikipongeza NCCR Mageuzi kwa kusimamia misingi mbalimbali iliyokifanya kisiharibike . Alikitaka kwa kujenga taifa linalojali haki, utu, busara, umoja na demokrasia

Mwenyekiti wa Jumuiya na Taasisi za Kiislamu Tanzania, Amiri Mussa Kundecha alimtaka Mbatia kuendelea kusimamia matakwa ya chama akizingatia misingi ya haki, amani na utulivu. Alisisitiza wanasiasa kuwezesha siasa zenye hekima nchini.

Chanzo: habarileo.co.tz