CHAMA cha NCCR-Mageuzi kimesema ajenda yao kubwa katika Uchaguzi Mkuu mwaka huu ni kutafuta muafaka wa kitaifa ili kufi kia maridhiano baina ya viongozi wa vyama vyote na kuipeleka nchi mbele.
Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati uzinduzi wa kampeni za ubunge Temeke, Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa chama hicho, Daniel Ayote alisema muafaka wa kitaifa ni msingi wa maendeleo ya uchumi wa nchi.
“Tunaomba mtuunge mkono katika ajenda zetu, tukiongozwa na ajenda kuu ya kutafuta muafaka kitaifa ili tufanye kazi kwa pamoja kwa sababu tunajenga nyumba moja,” alisema Ayote.
Alisema NCCR -Mageuzi inaunga mkono juhudi za maendeleo na kwamba kupitia uchaguzi huu kimekusudia kuunganisha na kulileta taifa pamoja kupitia muafaka wa kitaifa.
“Lazima tukubaliane kwa pamoja kuleta maendeleo hatuwezi kuendelea kutoelewana baina ya viongozi na wananchi na kufikia malengo,”alisema Ayote. Kamishna wa NCCR-Mageuzi, Mustafa Muro alisema chama hicho kinaamini katika mageuzi ya uchumi kwa kutumia nguvu kazi ya vijana.
Alisema kupitia mgombea ubunge wa Temeke, Miraji Asseid ni wazi atashirikiana vizuri na viongozi wengine hata wa vyama vingine bungeni kuleta maendeleo kwa kuwa chama hicho kinaamini katika umoja wenye tija kwa taifa.