Siku moja baada ya mkutano wa Halmashauri Kuu ya Chama cha NCCR-Mageuzi kutangaza kuwasimamisha Mwenyekiti wa Chama hicho, James Mbatia na makamu makamu mwenyekiti wake upande wa Bara,Angelina Mtahiwa, Kamati Kuu ya Halmashauri Kuu Taifa ya Chama hicho imekutana na kutoa maazimio manne ikiwamo kuwasimamisha nafasi za uongozi Makamu mwenyekiti Zanzibar Ambar Hamid, mweka hazina, Suzan Masele na naibu Katibu Mkuu Zanzibar, Amer Mshindan.
Juzi Jumamosi, Kikao hicho cha Halmashauri Kuu kilichokutana katika ukumbi wa Jeshi la Wokovu uliopo Kurasini kilitangaza kumsimamisha Mbatia na Makamu wake upande wa Bara, Angelina Mtahiwa.
Jana Jumapili Mei 22, 2022 Kamati Kuu ya chama hicho ilikutana katika ukumbi wa Msimbazi Center na kutoa maazimio manne.
Akisoma maazimio hayo Mwenyekiti wa Baraza la Wadahamini la Chama hicho, Mohamed Tibanyendela amesema wamewasimamisha Makamu mwenyekiti Zanzibar, mweka hazina, na naibu Katibu Mkuu Zanzibar hadi pale Halmashauri Kuu itakapokutana.
Tibanyendela amesema maazimio mengine ni kutotambua mkutano wa Halmashauri Kuu uliofanyika Mei 21 kutokana na kutokuwepo kwa mujibu wa katiba.
"Tayari tulishamwandikia barua Msajili wa Vyama vya Siasa wa kusogezwa mbele kwa mkutano huo hadi mwezi Agosti mwaka huu" amesema Tibanyelenda.
Pia, amesema Kamati Kuu imelaani Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa kuingilia migogoro ya chama na tayari wameshamuandikia barua pamoja na Mamlaka yake ya uteuzi.
Azimio jingine ni kutoitambua bodi ya wadhamini iliyoteuliwa kwani bodi ipo kihalali na inaendelea kufanya kazi kwa mujibu wa sheria.
Mwenyekiti wa NCCR, James Mbatia alisema Chama hicho ndio muasisi wa mageuzi Tanzania hivyo wanaamini katika muafaka wa kitaifa.
Amesema mambo yaliyotokea ni changamoto ndogo sana zilizotokea kwenye Chama hivyo wanaamini watasimamia.
"Haya yaliyotokea ni mgongano wa kimaslahi, tutaendelea kuimarika na ninaomba vyama vyote tusimamie demokrasia yetu," amesema Mbatia
Jana Jumapili mchana Jeshi la Polisi lilizingira ofisi za makao makuu ya Chama cha NCCR-Mageuzi zilizoko Ilala kuhakikisha hakuna shughuli zozote zinazofanyika katika ofisi hizo.