Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

NCCR-Mageuzi kutoa ratiba uteuzi wiki ijayo

MBAT.webp NCCR-Mageuzi kutoa ratiba uteuzi wiki ijayo

Fri, 5 Jun 2020 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

CHAMA cha NCCR-Mageuzi, kimesema kitatoa ratiba ya uteuzi wa wagombea urais, wabunge, madiwani pamoja na wawakilishi, mwanzoni mwa wiki ijayo huku kikiitaka Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC), kutenda haki katika uchaguzi mkuu 2020.

Pia, chama hicho kimefungua milango kwa chama chochote cha siasa nchini, ambacho kipo tayari kushirikiana ili kuiondoa Serikali ya Chama cha Mapinduzi madarakani.

Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia, alibainisha hayo jana wakati alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari, jijini Dodoma.

Mbatia alisema, tayari ameshamwagiza Katibu Mkuu wa chama hicho kutoa ratiba ya uteuzi wa wagombea ndani ya chama mapema wiki ijayo.

“Nitoe wito kwa vijana na wale wote wenye sifa, kujitokeza kugombea nafasi mbalimbali, katika uchaguzi huu, nafasi za urais Tanzania bara na Zanzibar, ubunge, wawakilishi pamoja na zile za udiwani,” alifafanua Mbatia.

Alisema, katika uchaguzi mkuu mwaka huu, chama hicho kipo tayari kushirikiana na vyama vingine vya siasa kwa maslahi ya taifa. “Sisi tupo tayari kushirikiana na chama chochote kile cha siasa kwa maslahi ya mama Tanzania, kwani hata salamu yetu inasema kwa pamoja tutashinda,” alisema Mbatia.

Alisema, katika uchaguzi mkuu 2020, ajenda yao ni Katiba mpya kwa kuwa ndiyo kauli ya umma wote.

“Ajenda yetu katika uchaguzi huu ni katiba mpya ni haki yetu kauli hii inatokana na umma wote lazima tutaendelea kuipigania kwa mslahi ya taifa letu,” alisema.

AkizungumziaTume ya Taifa ya Uchaguzi nchini, alisema inatakiwa kuzingatia taratibu za kisheria na kikanuni na uamuzi yanatolewa kwa usawa na haki.

“Uchaguzi mkuu wa mwaka huu, mwezi Oktoba, tunataka kuliingiza taifa hili katika historia mpya kwa Tume ya Uchaguzi kutenda haki na usawa,” alisema.

Aliwapongeza watu waliojiunga na chama hicho hivi karibuni, wakiwamo wabunge na viongozi wengine wakubwa.

Akizungumzia mlipuko wa virusi vya corona, Mbatia alisema wanaendelea kuwatahadharisha wananchi kuendelea kuchukua hatua ili kujikinga.

“Corona bado ipo, tuendele kuchukua tahadhari na kuondoa hofu mimi ni mtaalam wa majanga lazima tuhakikishe kuwa hofu yetu inaondoka kwa kuwa inachangia katika kushusha kinga ya mwili kwa kiwango kikubwa sana,” alisema.

Alisema NCCR-Mageuzi, kinalaani vikali mauaji ya kikatili ya raia mweusi wa marekani George Floyd, akiwa mikononi mwa polisi hali iliyosababisha maandamo makubwa.

“Sisi kama taifa tuna kitu cha kujifunza, pia jeshi letu la polisi lina kitu cha kujifunza, maandamano haya yameathiri uchumi wa Marekani ambao unatugusa na sisi pia hapa,” alisema.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live