Dar es Salaam. Mwenyekiti wa NCCR-Mageuzi, James Mbatia amesema chama hicho cha upinzani nchini Tanzania kitashiriki uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba, 2020.
Mbatia ambaye pia mbunge wa Vunjo ametoa kauli hiyo leo Alhamisi Februari 13, 2020 katika mkutano wa waandishi wa habari kuhusu namna chama hicho kilivyojipanga kushiriki uchaguzi huo.
Amesema wataweka wagombea wa udiwani, ubunge na urais kwa maelezo kuwa chama hicho ndio kimeasisi mageuzi nchini.
Amesema lengo la chama chochote cha siasa ni kupata mamlaka kupitia vyombo vya uamuzi ili kuwatumikia Watanzania.
“Jana tulifanya kikao tumeamua kushiriki kwenye uchaguzi huu. Tutashiriki ngazi ya urais Tanznaia Bara na Zanzibar, na pia ubunge, uwakilishi na udiwani,” amesema Mbatia.
Kwa mujibu wa Mbatia, Februari 19, 2020 watafanya kikao cha halmashauri kuu ya chama hicho kuweka mikakati ya pamoja na kutoa ratiba ya chama ya namna mchakato huo utakavyokuwa .
Pia Soma
- Samia awaonya wanachama CCM
- Makamu wa Rais Mama Samia aongoza maadhimisho miaka 43 ya kuzaliwa CCM
- CCM yatenga Sh1 milioni kumchukulia fomu Rais John Magufuli
- Mvutano wa utendaji mamlaka za Serikali washtua wajumbe wa bodi ya barabara
Kuhusu ushirikiano na vyama vingine vya upinzani Mbatia amesema, “hili suala kubwa kidogo linalohusu katiba yetu ya chama na chombo kikubwa na uamuzi ni halmashauri kuu ya NCCR-Mageuzi. Baada ya kikao tutatoa maazimio yetu kuhusu jambo hili.”