Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mzimu wa Lowassa waitesa Chadema

86845 Pic+lowasa Mzimu wa Lowassa waitesa Chadema

Mon, 2 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Chadema imepanga kufanya uchaguzi wa viongozi wake kitaifa Desemba 18 mwaka huu.

Hata hivyo, uchaguzi huo unaweza kuwa tofauti na chaguzi za miaka ya nyuma kutokana na mazingira ya kisiasa yalivyo sasa.

Kurejea CCM kwa aliyekuwa mgombea wao, Edward Lowassa ambaye uchaguzi wa mwaka 2015, alipata kura 6,072,848 sawa na asilimia 39.97 ni jambo ambalo linaonekana kuutikisa uchaguzi ujao wa Chadema.

Kutokana na hilo, wadau wa siasa wamesema Chadema imekuwa na hofu na ni ngumu kuwaamini waliohamia kutoka CCM na kuwapa uongozi.

Kuanguka kwa wagombea uenyekiti wa Kanda, Frederick Sumaye (Pwani) na Cecil Mwambe (Kusini) kunaweza kuwa na ujumbe kwa watu ambao walihamia Chadema wakitokea CCM wakati wa joto la uchaguzi la mwaka 2015.

Sumaye na Mwambe ambao waliangushwa katika chaguzi hizo za kanda, wamechukua pia fomu za kugombea nafasi ya mwenyekiti wa Chadema kupambana na Freeman Mbowe, ambaye ameongoza chama hicho tangu 2004.

Kurejea kwa viongozi kadhaa wa upinzani katika chama tawala ndani ya miaka miwili iliyopita wakiwamo wabunge, madiwani, mameya na wanachama wa kawaida kumevifanya vyama vya upinzani kuwaangalia kwa jicho la mashaka waliojiunga na upinzani wakati wa uchaguzi wa 2015.

Hofu hiyo ya upinzani inaweza kuwa imeongezeka zaidi kutokana na kurejea CCM kwa Edward Lowassa, mtu ambaye aliapa ‘kutowasaliti’ wapiga kura wake milioni sita waliompigia kura 2015.

Lowassa ambaye amewahi kuwa waziri mkuu kuanzia mwaka 2005 mpaka 2008, alihamia Chadema mwaka 2015 na kufuatwa na viongozi makada kadhaa wa CCM wakiwemo waliowahi kuwa wabunge, mawaziri na viongozi wa mikoa wa chama hicho.

Hata hivyo, wimbi lililoanza miaka miwili iliyopita la viongozi kadhaa hasa wabunge na madiwani wa upinzani kurejea CCM lilimkumba pia Lowassa, ambaye miezi michache iliyopita alikuwa ameapa kutorejea chama tawala.

Hata hivyo, Machi Mosi mwaka huu Lowassa alirejea CCM jambo ambalo kwa namna moja au nyingine limefanya viongozi waliohamia naye kwenda Chadema kuangaliwa kwa jicho la mashaka.

Wachambuzi wa masuala ya siasa nchini wanasema sasa imedhihirika mzimu wa Lowassa unakisumbua chama hicho kufuatia kushindwa kwa makada wa zamani wa CCM, Sumaye na Mwambe.

Akizungumza na Mwananchi jana, mchambuzi wa masuala ya siasa, Profesa Gaudence Mpangala amesema kuondoka kwa Lowassa kumechangia Chadema kupoteza imani na wanachama wake waliotokea CCM.

“Kuondoka kwa Lowassa kumeiathiri Chadema, aliaminiwa na kupewa nafasi kubwa, sasa uamuzi wake wa kuondoka huenda umewafanya wanachama wake kukosa imani na watu waliohamia kutoka CCM,” alisema Profesa Mpangala.

Wakati mchakato wa uchaguzi ukiendelea ndani ya Chadema, kwenye mitandao ya kijamii imeibuka mijadala ya makada wa chama hicho wakipanga safu za uongozi na kutaja makada wakongwe ambao hawakuwahi kuwa CCM.

“Kwa Chadema inaonekana hao `wahamiaji’ walikwenda kuisoma Chadema kwa manufaa ya CCM ndiyo yakatokea yale mambo ya hamahama, sasa ni kama wanachama wameshtuka na wanajaribu kukabiliana na hilo,” alisema Profesa Mpangala.

Hoja hiyo iliungwa mkono na mhadhiri wa sayansi ya siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Dk Richard Mbunda aliyesema kuwa kutokana na hali ngumu wanayopitia Chadema kuna hali ya kutoaminiana.

Alisema kinachoendelea ni jitihada za makusudi za kukilinda chama dhidi ya hujuma na kujaribu kuwaweka watu wanaoonekana wanaaaminika.

“Kuna watu wameonekana kuwa mamluki na wana ajenda ya kukivuruga chama hicho ndiyo maana viongozi wameamua kufanya jitihada za makusudi kupambana kukilinda chama dhidi ya hujuma. Huwezi kuwa na imani tena na watu wa aina hiyo maana wenzao wameonyesha mfano kwa kurudi CCM,” alisema Mbunda.

Vita ya uenyekiti yahusishwa

Hofu ndadi ya Chadema imeongezeka zaidi kwa wanachama waliohamia Chadema wakati huu wa uchaguzi mkuu, ambao Sumaye na Mwambe wamechukua fomu kutaka kupambana na Mbowe katika nafasi ya uenyekiti wa Taifa.

Kitendo cha kuanguka kwa Sumaye katika nafasi ya mwenyekiti wa Chadema-Kanda ya Pwani na Mwambe (Kusini) kunaweza kuwa na uhusiano wa moja kwa moja na hilo.

Kwa mtu kama Sumaye ambaye alitawala na kuwa kivutio kikubwa katika kampeni za urais za mwaka 2015, usingetarajia aanguke kirahisi katika uchaguzi wa kanda, tena kwa kura za hapana.

Sumaye, ambaye ni waziri mkuu aliyehudumu kwa miaka yote kumi ya utawala wa Rais wa Awamu ya Tatu, Benjamini Mkapa alipata kura 48 za ‘Hapana’ dhidi ya 28 za ‘Ndiyo’ katika uchaguzi huo ambao unaweza si tu kubadilisha taswira ya mwanasiasa huyo ila hata ya Chadema kwa ujumla.

Kuanguka kwa Mwambe ambaye alipata kura 31 dhidi ya 53 za mshindi Selemani Mathew hakuwezi kufananishwa na suala la Sumaye, ingawa naye pia anaonekana mgeni Chadema kwa sababu alihamia mwaka 2015.

Sumaye aliwatangazia wajumbe kuwa nia yake ya kuwania uenyekiti wa Chadema nafasi inayoshikiliwa na Freeman Mbowe ndiyo iliyomuadhibu, lakini ataendelea kuwa mwanachama mtiifu.

Kuna maswali mengi na mitazamo mingi tofauti. Je kitendo cha mgombea urais wa Chadema, Edward Lowassa aliyepata kura milioni sita na kuweka rekodi kwa wagombea wa vyama vya upinzani tangu mfumo wa vyama vingi uanze mwanzoni mwa miaka ya tisini, kumewafanya Chadema wasiwe na imani na wanaohamia kutoka CCM?

Kitendo cha Sumaye kuchukua fomu ya kuwania uenyekiti wa Taifa, kwa baadhi ya wanachama wa Chadema kimeonekana kama usaliti mkubwa na hasa wengi wakiamini kuwa Mbowe ambaye amekuwa mwenyekiti wa Chadema tangu mwaka 2004 anastahili kuendelea kuongoza chama hicho.

Hoja hiyo inaweza kupewa nguvu na hasa ukizingatia kuwa safu ya viongozi wote wa juu walioingia na Mbowe madarakani mwaka 2004, hakuna aliyebaki hata moja. Wote wamerudi CCM.

Lakini kitendo cha Sumaye kukataliwa na kuonekana hafai, ina maana Chadema imeamua kwenda na watu ambao wanaamini. Je Chadema haimwamini yeyote anayehamia kutoka CCM?

Walichokisema Chadema

Hata hivyo, mkurugenzi wa Mawasiliano, Itikadi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alikataa kuhusisha kuangushwa kwa Sumaye na Mwambe na historia yao ya nyuma huku akieleza huo ni uamuzi wa wapiga kura.

Chanzo: mwananchi.co.tz