Katibu Mkuu Mstaafu wa CCM Yusufu Makamba amempinga hadharani Katibu Mstaafu mwenzake Dk Bashiru Ali kuhusu kupinga kauli ya kuupinga mwingi.
Neno kuupiga mwingi, limekuwa likitumiwa na makada wa CCM wakimsifia Rais Samia Suluhu Hassan kwa kazi anazofanya.
Novemba mwaka huu, Dk Bashiri akihutubia mkutano wa Mtandao wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (Mviwata) uliofanyika mkoani Morogoro, aliwataka wakulima kudai haki zao, huku akionyesha kukerwa na kauli ya kuupiga mwingi.
Akitoa salamu katika mkutano mkuu wa CCM jijini Dodoma leo 8, 2022 jijini Dodoma alipopewa nafasi ya kuwasalimia wajumbe wa mkutano mkuu wa CCM.
Wakati akitoa kauli hiyo, Dk Bashiru Ali alikuwa ameketi kwenye viti vilivyoandaliwa kwa Makatibu wakuu wastaafu akiwemo Wilson Mukama.
Mkongwe huyo ambaye amejiita jina la Tobo, amemweleza Dk Bashiru kuwa aachane na kauli zake kwamba Rais Samia ni jembe badala yake akubaliane na waliowengi kuwa anaupiga mwingi.
“Jana nilimwambia Bashiru, wewe kipindi cha Magufuli (Hayati John) ulimuita buldoza sasa wenzako wakimuita kaupiga mwingi nongwa iko wapi,” amesema Makamba.
Mzee Makamba ambaye jana alichaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Makatibu wakuu wastaafu, alianza kwa utani wa kusema, “kuna shemeji yangu hapa nilimwambia jana lakini tumeelewana.”
Makamba anamuita Dk Bashiru shemeji kwa sababu mke wa mzee huyo Mama January anatoka mkoa wa Kagera ambako ndiko asili ya Dk Bashiru.
Kuhusu Rais Samia amesema hakuna mwingine wa kumpinga 2025 ndani ya chama na hata kwa wanaotaka kuwania kiti hicho kutoka nje ya CCM kwani bado anaamini Mwenyekiti huyo anasifa za kuwa kiongozi.