Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwili kiongozi Chadema aliyeuawa wawasili nyumbani

97510 Pic+chadema Mwili kiongozi Chadema aliyeuawa wawasili nyumbani

Sat, 29 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Manyoni. Vilio na simanzi vimetawala wakati mwili wa mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Manyoni, Alex Magubi ukiwasili  nyumbani kwake mtaa wa Majengo Mjini Manyoni ukiwa umebebwa na vijana wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania huku wakiimba nyimbo mbalimbali.

"Tumechoka kuuawa, tutajilinda wenyewe, tumechoka kuuawa, tutajilinda wenyewe," wamesikika wakiimba vijana hao waliovalia sare za chama hicho.

Magubi ambaye ni mkazi wa Majengo mjini Manyoni mkoani Singida mwili wake ulikutwa umepigwa na kitu chenye ncha kali Februari 25, 2020.

Baada ya mwili kuwasili itafanyika ibada, baadaye kuelekea makaburini kwa maziko.

Februari 27, 2020 Kamanda wa Polisi mkoani Singida, Sweetbert Njewike amesema Magubi ambaye kituo chake cha kazi kilikuwa Mwembeni mjini Manyoni bado haijafahamika siku ya tukio, aliondoka muda gani.

Kamanda Njewike amesema mwili wa marehemu uliokotwa mbugani mbali na barabara, ukiwa umechomwa chomwa sehemu mbalimbali za mwili ikiwemo kichwani na miguuni.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
“Wakati mwili wa Alex ukiokotwa mbugani, pikipiki yake iliokotwa kanda ya barabara iendayo Dodoma. Baada ya mwili kukaguliwa alikutwa na vitu vyote isipokuwa simu. Chanzo cha mauaji hayo bado hakijafahamika, upelelezi unaendelea,” amesema.

Amesema hadi sasa hakuna mtu anayeshikiliwa kuhusiana na mauaji hayo ya kikatili na wameanzisha msako mkali.

“Tunaomba mwananchi yeyote mwenye taarifa sahihi juu ya tukio hilo atoe kwenye kituo chochote cha polisi kilicho karibu au mamlaka zingine ili watu\mtu aliyehusika aweze kukamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria,” amesema.

Kuhusu marehemu kuwa kiongozi wa Chadema wilayani Manyoni, Njewike amesema hilo wamelisikia lakini walipofanya utafiti imebainika kuwa alikuwa ni dereva wa bodaboda tu na sio kiongozi wa Chadema.

Wakati Kamanda Njewike akisema kuwa Magubi hakuwa kiongozi wa Chadema, Mwenyekiti CCM Halmashauri ya Itigi, Alli Minja akizungumza na Mwananchi amesema marehemu alikuwa mwenyekiti Chadema Wilaya ya Manyoni.

“Binafsi nasikitika kwamba sitohudhuria mazishi yake kutokana na kukosa usafiri. Alex alikuwa Chadema wa aina yake,” amesema na kuongeza;

“Alikuwa na utamaduni wa kuhudhuria vikao vya mabaraza ya madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni na kwetu huku Itigi. Kwenye suala la miradi ya maendeleo, ulikuwa huwezi kujua kama ni wa upinzani. Alikuwa anatoa ushirikiano wa hali ya juu. Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi,” amesema Minja.

Chanzo: mwananchi.co.tz