Waziri wa Fedha, Mwigulu Nchemba amechombeza kuelekea 2025 akisema wanaojadili mwaka huo ambao ni wa Uchaguzi Mkuu wanaona kiwango cha mvua na mafuriko na mengine ambayo hajayataja kwenye hotuba yake.
"Mama apewe maua yake," amesema Mwigulu katika hotuba yake bungeni mjini Dodoma dakika chache kabla ya wabunge kuipigia kura bajeti ya Serikali ya mwaka wa fedha 2023/2024. Huku akishangiliwa kwa nguvu, Mwigulu amesema Rais ana vitu ambavyo si kila mtu anaweza kuvifanya.
"Mama ni mama, mpeni maua yake, wanaojadili 2025 na kiwango cha mvua nilichowatajia na mafuriko na mengine ambayo sikuyataja, sio kila mtu anaweza kufanya," amesema. Amesema mengine anayofanya siyo ya kutoa fedha, anasimamia watu wapate haki yao. "Anasaidia kuunganisha nchi, uwekezaji na mengine mengi siwezi kuyataja yamefanyika," amesema Mwigulu akisisitiza kuwa ni vyema kumheshimu na kuunga mkono yale yanayofanywa na viongozi. "Tuwalipe uungwana viongozi wetu, tuwe tunajikita kwenye hoja, tuache hoja za kuvuka mipaka ambazo zinaweza kuligawa taifa letu," amesema Mwigulu. Waziri huyo wa fedha alihitimisha hotuba yake kwa kuwaomba wabunge wapokee salamu za Rais. "Amesema yuko nanyi bega kwa bega, mkitoka hapa mpeleke salamu kwa wananchi," amesema Mwigulu.