Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwiba mwingine mchungu kwa wabunge wa upinzani Tanzania

81859 Pic+upinzani Mwiba mwingine mchungu kwa wabunge wa upinzani Tanzania

Mon, 28 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Zuio la mikutano ya hadhara limeendelea kuwa mwiba kwa wabunge wa vyama vya upinzani katika majimbo kadhaa, huku wenzao wakionekana kuendesha shughuli zao bila matatizo.

Rais John Magufuli alipiga marufuku mikutano ya hadhara na maandamano mwaka 2016, isipokuwa kwa viongozi waliochaguliwa ambao wameruhusiwa kuendesha mikutano katika maeneo yao.

Zuio la Rais pia halikuhusu mikutano ya ndani ya vyama, lakini wanasiasa wa upinzani wamekuwa wakilalamikia kuzuiwa kwa sababu tofauti ambazo hawaridhiki nazo.

Zuio hilo limekuwa likilalamikiwa kila mara na wapinzani, lakini Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Simon Sirro aliwahi kuiambia Mwananchi kuwa hajawahi kupokea barua ya malalamiko hayo.

Jana, polisi wilayani Iringa Mjini ilizuia mkutano ambao Mchungaji Peter Msigwa (Chadema) alipanga kufanya katika Uwanja wa Mwembetogwa.

Sababu za kuzuiwa ni barua ya taarifa ya Chadema kutoweka wazi dhumuni la mkutano na kuwepo kwa taarifa za kiintelijensia kuhusu kundi la watu kupanga njama za kufanya vurugu mkutanoni.

Pia Soma

Advertisement
Pamoja na polisi kusema hawajui madhumuni ya mkutano huo, wamesema sababu ya tatu ni dalili za kuanza mapema kampeni za uchaguzi wa serikali za mitaa pamoja na kutokuwapo kwa askari wa kusimamia mkutano wake.

Lakini Msigwa ambaye ni mbunge wa Iringa Mjini alisema hoja za polisi hazina mashiko.

“Ni mikutano mingi sana nimezuiliwa ambayo sina kumbukumbu ya idadi yake. Wananizuia kwa sababu ukweli wanaufahamu na hawataki wananchi wapate taarifa hizo,” alisema.

“Lakini wananchi kwa sasa wanahitaji kuelezwa ukweli ili kufanya uamuzi badala ya kushawishiwa kwa kofia na tisheti.”

Sababu kama hizo na nyinginezo zimekuwa zikitumiwa na polisi kuzuia mikutano maeneo mengine.

Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe alizuiwa na polisi kufanya ziara jimboni kwake kwa maelezo kuwa mkuu wa wilaya hiyo alikuwa na ziara ya kukagua shughuli za maendeleo.

Katika hatua nyingine, polisi walivamia mkutano wake wa ndani jimboni Septemba 30 wakidai kuwepo na taarifa za kiintelijensia za kuhatarisha amani.

Hayo pia yamemkuta mbunge wa Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ambaye ameiambia Mwananchi kuwa tangu Januari hajapata kibali cha kufanya mikutano na ameshazuiwa mara kadhaa, moja ya sababu ikiwa ni taarifa za kiintelijensia za kuhatarisha amani wakati wa mikutano yake.

Katika wiki za karibuni, Mwananchi imeshuhudia wabunge wa CCM wakifanya mikutano. Miongoni mwao ni Haroon Pirmohamed (Mbarali), Abdallah Chikota (Nanyamba) na Dk Charles Tizeba (Buchosa).

Wengine ni Pauline Gekul (Babati Mjini), Emmanuel Papian (Kiteto) na Hawa Ghasia wa Mtwara Vijijini.

Baadhi ya walioongea na Mwananchi kuhusu hali hiyo, walishauri wabunge kutafuta haki yao mahakamani.

“Mikutano ya hadhara inatambuliwa kisheria na kikatiba. Mahakama ndiyo itatoa tafsiri na kuweka vigezo ili kuondoa changamoto ya sababu ambazo polisi inaweza kutoa wakati wowote,” alisema wakili wa kujitegemea, Dk Onesmo Kyauke.

“Pili Msajili anatakiwa atoe tamko kwa Jeshi la Polisi kuhusu athari hizo. Wazungumze ili kuona tatizo liko wapi maana vyama visipofanya siasa vinakosa uhai hivyo ni tishio la kufutwa kisheria.”

Tayari mbunge wa Ubungo (Chadema), Saed Kubenea amesema atamwandikia barua Msajili na Spika wa Bunge ili kupata ufafanuzi kuhusu zuio la kufanya shughuli zake za kijimbo.

Pia Mbilinyi, maarufu kwa jina la Sugu, aliandika barua mara mbili kwa mkuu wa polisi wa wilaya, kisha akawasiliana na kamanda wa polisi wa mkoa bila kupata msaada kabla ya kuwasiliana na IGP Sirro,

“Siku moja nilikutana na RPC na IGP Sirro uwanja wa ndege wa Songwe. IGP akatoa agizo kwa RPC mbele yangu (kuruhusu mikutano). RPC akatii,” alisema Sugu.

“Baadaye RCP akaniambia amemuagiza OCD kuniruhusu, lakini bado kukawa na ugumu. OCD anasema hajapewa agizo lolote. Hali hiyo iliendelea na imefika hatua si RPC wala OCD anayepokea simu wala hawajibu meseji zangu.”

Chanzo: mwananchi.co.tz