Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwenyekiti mwingine akana kuhama Chadema

17516 Mwenyekiti+pic TanzaniaWeb

Mon, 17 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Hai. Wiki moja baada ya wenyeviti 20 wa vijiji wa Chadema katika Jimbo la Hai mkoani Kilimanjaro kuripotiwa kuhamia  CCM, mmoja wa ameibuka na kukanusha madai hayo.

 

Akizungumza na MCL Digital leo Jumamosi Septemba 15, 2018 mwenyekiti huyo wa kijiji cha Warindoo, Emmanuel Muro  amesema taarifa hizo hazina ukweli wowote.

 

Mbunge wa Hai ni Freeman Mbowe ambaye pia ni mwenyekiti wa Chadema na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni.

 

Muro amesema alishangazwa kuona orodha ya jina lake kati ya wenyeviti 20 alioorodheshwa kuwa wamejiuzulu.

“Nilishapeleka malalamiko yangu polisi na sehemu nyingine husika lakini naona inapigwa danadana tu, ukweli ni kuwa sijajiuzulu.

“Sijawahi kuandika barua ya aina yoyote ile kuhusiana na kujivua uenyekiti nilishangaa kiukweli kuona jina langu kwenye magazeti na kwenye mitandao kwamba nimejiuzulu hakuna kitu kama hicho,” amesema.

Septemba 11, 2018 mwenyekiti mwingine wa kijiji cha Uraa, Seth Munisi ambaye jina lake lilikuwa katika orodha ya waliojiuzulu alikanusha.

Taarifa ya wenyeviti hao kuhama Chadema ilithibitishwa  Septemba 6, 2018 na mkurugenzi wa Halmashauri ya Hai, Yohana Sintoe aliyedai kupokea barua zao za kujiuzulu.

Katibu wa CCM mkoani Kilimanjaro,  Jonathan Mabihya amesema ni jambo la kushangaza wenyeviti hao kuandika barua za kujiuzulu kisha kuzikana na kubainisha kuwa huenda wametishwa na vyama vyao.

"Itakuwa wametishwa na vyama vyao vya awali kwa sababu wenzetu wanatumia ubabe zaidi. Kama wao wametishwa wakane barua zao za kujiuzulu. Kama katibu wa mkoa nawaambia waende mahakamani kufungua mashtaka,” amesema Mabihya.

Naye katibu wa Chadema mkoani hapa, Basil Lema amesema: “Kama kweli walihama kwa mioyo yao iweje sasa hivi wakane  barua zao. Ni wazi kuwa walilazimishwa kwa mitutu ya bunduki.  Huku wako salama iweje wajiondoe.”

Chanzo: mwananchi.co.tz