Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwenyekiti UVCCM awataka vijana kutokuogopa kusema ukweli, kuwakosoa viongozi

22280 Uvccm+pic TanzaniaWeb

Mon, 15 Oct 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa UVCCM, Kheri James amewataka vijana kutosita kusema ukweli pamoja na kuwakosoa viongozi wao pale wanapopotoka ili kuenzi misingi ya ukweli ya Mwalimu Julius Nyerere.

Akizungumza wakati UVCMM walipotembelea nyumba ya Mwalimu Nyerere, Msasani jijini Dar es Salaam leo ikiwa ni sehemu ya kumbukizi ya kifo cha mwasisi huyo wa taifa, alisema kwa sasa vijana wengi wamekuwa wakisita kusema ukweli kwa viongozi wao.

"Kama kuna jambo limepungua katika jamii yetu ya sasa ni utamaduni wakuambiana ukweli, kuvumilia ukweli na kupokea ukweli."

"Tunatumia kumbukizi hii ya Mwalimu kuwasisitiza vijana kote nchini kutumia turufu ya ukweli katika kueleza, kukosoa na kusimamia maslahi ya nchi yetu,"  alisema.

James alisema endapo vijana watakaa kimya taifa litapoteza mwelekeo kwa kiasi kikubwa, jambo ambalo ni ishara ya kutojali misingi mizuri ya waasisi wa taifa hili.

"Pale ambapo alikosea Mwalimu hakusita kusema bayana kwamba kweli nimekosea. Ni viongozi wangapi katika nchi yetu, ndani ya chama chetu tupo tayari kuomba radhi tunapokosea. Hii ni kazi kubwa tunayotakiwa kuifanya," alisema.

Alisema UVCCM iko tayari kusimamia heshima ya nchi na kutoruhusu viashiria vyovyote vya uvunjifu wa amani na heshima iliyoasisiwa na Mwalimu Nyerere kwani kufanya hivyo ni uzalendo kwa taifa.

"Tumeanza ukurasa mpya ambao hatutokubali mtu yoyote kwa cheo chake, nafasi yake  kuvunja heshima ya nchi eti kwa msingi wa uhuru wa kujieleza au demokrasia," alisema.

Chanzo: mwananchi.co.tz