Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwenyekiti UVCCM anaweza kusamehewa, lakini ukweli ni upi?

12527 Uvccm+pic TanzaniaWeb

Sat, 18 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Je, ni kweli kwamba Serikali ya CCM hupendelea maeneo ambayo chama hicho kina ufuasi mkubwa kwa kuyapatia fedha nyingi za maendeleo ukilinganisha na yale yanayoongozwa na upinzani?

Hili ndilo swali ambalo limekuwa likijadiliwa katika majukwaa mbalimbali huku kukiwa na wimbi la viongozi wa upinzani wakihamia CCM kwa kile wanachokitaja kama kuiunga mkono Serikali na kuhakikisha maeneo yao yanafikiriwa kwa ajili ya maendeleo.

Mjadala kuhusu upendeleo unaofanywa na CCM ulichochewa na kauli ya Mwenyekiti wa Jumuiya ya Vijana ya chama hicho (UVCCM), Kheri James ambaye alisema ni CCM pekee ndiyo inayoamua wapi pa kupeleka maendeleo na kwamba hakuna mwananchi atakayefanya lolote.

Licha ya kuomba msamaha kwa kauli hiyo, James alikuwa tayari ameshayamwaga maji ambayo kuyazoa si rahisi. Akiwa katika kampeni za kumnadi mgombea wa udiwani kwa tiketi ya CCM katika Kata ya Bugara mkoani Manyara, James alisema CCM haiwezi kupeleka maendeleo kwenye maeneo ambayo wakazi wake huchagua upinzani badala ya chama tawala.

Aomba radhi

Katika tamko lake la kuomba radhi, hata hivyo, James hakusema anaomba radhi kwa kosa gani. Pia, alishindwa kusema kwamba kauli yake ilikuwa ni ya uongo na aliupotosha umma. Badala yake alifanya hivyo kutokana na simu alizopokea za kumkosoa na kumuonya kwa kauli yake hiyo tata.

Ikiwa hao waliomuonya James walifanya hivyo kwa kuwa alidanganya au kwa kuvujisha siri, haijajulikana. Kinachojulikana, ni tamko la kuomba msamaha lilikuja ndani ya siku tatu baada ya Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, Humphrey Polepole kuikana kauli ya James kwenye mkutano na waandishi wa habari, kwamba kauli hiyo haiakisi msimamo wa chama.

Polepole alisema CCM ni muumini mkubwa wa imani kwamba maendeleo hayana chama, kauli ambayo hutolewa mara nyingi na Rais John Magufuli.

Hata hivyo, Polepole hakubainisha kama kuna hatua zozote zinaweza kuchukuliwa dhidi ya James kutokana na kauli yake.

Hadi sasa, hakuna anayejua ni kauli ipi ya kushika, msamaha wa James au ya Polepole. Ndiyo kisa, Hamad Hamis, mtumiaji wa Twitter aliandika:

“Mwambie (James) kwamba tumeusikia msamaha wake,”. “Na tutafuatilia maeneo yote (ya nchi) yaliyopo chini ya CCM, tukilinganisha viwango vyao vya maendeleo na yale ambayo (CCM) haiongozi.”

Pamoja na hayo, utaratibu ambao CCM imekuwa ikiutumia katika kupeleka maendeleo majimboni umekuwa ni jambo la mjadala siku zote.

CCM yenyewe imekanusha zaidi ya mara moja kama inafanya matumizi ya kitaifa ya Serikali katika hali ya kibaguzi ambapo hupendelea maeneo ambayo inatawala na kuyaacha yale yaliyopo chini ya upinzani.

Suala kwamba Serikali ya Tanzania inafanya matumizi makubwa ya kitaifa kwenye maeneo yenye ufuasi mkubwa kwa CCM lilikuwa ndio msingi wa utafiti uliopewa jina la ‘Siasa za Matumizi ya Serikali Tanzania, 1999-2007.’

Ingawa hakuna ripoti mpya, taarifa za utafiti wa mwaka 1998-2007 katika wilaya 114 nchini, uligundua kwamba Serikali ilikuwa inapeleka kiwango kikubwa cha matumizi ya kibajeti kwenye zile wilaya zilizoipigia chama hicho kura nyingi tofauti na maeneo yaliyo chini ya upinzani.

Utafiti huo ambao ulichapishwa katika jarida la African Studies Review mwaka 2011 ulitumia mabadiliko ya mfumo wa kikodi ambao ulishuhudiwa kupigwa marufuku kwa tozo ya maendeleo ya serikali za mtaa katika mwaka 2003-2004.

Licha ya kuwa kodi hii ilikuwa ndio chanzo kikuu cha mapato ya mamlaka ya serikali za mitaa, Serikali ya awamu ya tatu iliipiga marufuku kodi hiyo kufuatia malalamiko kwamba utekelezaji wake haukuwa sawa na kwamba walipa kodi hawakuwa wakiona manufaa ya kodi hiyo katika uboreshwaji wa huduma za kijamii.

Ukinzani dhidi ya kodi hiyo katika Wilaya ya Arumeru mwaka 1998 na kuchomwa moto kwa ofisi ya kodi ya Wilaya ya Kilosa, ni mifano miwili ya ukinzani dhidi ya tozo hiyo uliodhihirisha kutokuridhishwa kwa watu wengi.

Lakini, upigaji marufuku wa tozo ya maendeleo na kuchukuliwa na Serikali kuu, na mgao uliofuata uliofanywa na serikali katika mwaka 2005 kufidia mapato yaliyopotea. Hapa ndipo Serikali ilianza kupunguza mgao wa kibajeti kwa wilaya za upinzani bila kuibua malalamiko ya upendeleo.

Upigwaji marufuku wa tozo hiyo uliipa Serikali fursa kubana fidia ya mapato yaliyopotea kwa malengo ya kisiasa. Hatua hii ilimpatia Laura Weinstein, nafasi ya kuangalia “mchezo” uliokuwa ukifanyika katika ugawaji wa Bajeti kwa mwaka wa fedha wa 2004-2005. Aalichambua jumla ya pato au hasara (net gain and loss) iliyotokana na mabadiliko ya mfumo wa kodi ili kufahamu kama kulikuwa na upendeleo wowote.

Kwa CCM faida, upinzani hasara

Utafiti huo ulifichua kwamba Serikali ilipunguza matumizi yake kwenye maeneo yaliyo chini ya upinzani na yale ambayo hayakuipa CCM ushindi mkubwa wa asilimia 60 kwenda juu katika uchaguzi wa mwaka 2000. wilaya kama vile za Arusha, Ilala, Kinondoni, Temeke, Bukoba, Moshi na Mwanza zote zilishuhudia upungufu wa mapato yaliyotengwa na Serikali kuu.

Kwa upande mwingine, utafiti huo ulibaini kuwa Serikali iliongeza kiwango cha bajeti kwa wilaya zilizo karibu katika mkoa huohuo ambazo zimeiongezea CCM mgao wake wa kura baada ya uchaguzi.

Hii ilidhihirika katika maeneo ya Biharamulo mkoani Kagera na wilaya ya Arumeru mkoani Arusha ambapo wilaya hizo mbili ziliiongezea CCM ushindi kwa kuipatia kura zaidi ya asilimia 60 baada ya uchaguzi wa kwanza.

Ongezeko la asilimia moja la kura zilizopigwa, kwa mujibu wa utafiti huo, lilihusishwa na ongezeko la Sh1.51 ya pato la mtu binafsi.

Kama wastani wa idadi ya watu wanaoishi katika wilaya husika ni 270,000 hii ingepelekea ongezeko la kibajeti la Sh408, 000. Kwa ongezeko la pointi moja la kura zilizoenda kwa upinzani serikali ilikuwa inapunguza matumizi yake kwenye wilaya hiyo kwa Sh2.04 katika pato la mtu mmoja, au punguzo la wastani la kiwilaya la Sh550, 000.

Ongezeko la asilimia moja katika kura za mgombea wa urais wa CCM ilipelekea ongezeko la asilimia 1.12 katika pato la mtu binafsi katika shilingi za Kitanzania. Utafiti huo pia uligundua kuwa kadri kura za mgombea wa urais wa upinzani zilivyokuwa zikiongezeka, kiwango cha kushuka kwa bajeti katika wilaya husika ilikuwa ni kwa asilimia 1.29.

Maendeleo hayana chama

Rais Magufuli, licha ya utafiti uliofanyiwa rejea hapo juu, amesikika zaidi ya mara moja akisema Serikali huipendelea mtu wala eneo lolote. Kauli yake ya “maendeleo hayana chama” inarudiwa rudiwa na wasaidizi wake waliomo serikalini na katika chama. Alipoulizwa kuhusu matokeo ya utafiti huo, Polepole alikataa kuuzungumzia akimtaka mwandishi waonane akiwa na huo utafiti. Alipofuatwa ofisini kwake, hakupatikana.

Lakini, matokeo ya utafiti huu hayakishangazi chama kikuu cha upinzani chini, Chadema. Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano na Mambo ya Nje wa chama hicho John Mrema anaona kutokuwepo kwa usawa katika ugawaji wa fedha za maendeleo kati ya maeneo wanayoyaongoza na yale yaliyo chini ya CCM kama ni desturi na siyo bahati mbaya.

Mrema anasema kwamba hiyo ndio imekuwa hulka ya Serikali kuyatenga maeneo yanayoongozwa na Chadema na kwamba chama hicho kimekuwa kikipokea malalamiko ya mara kwa mara kuhusiana na ubaguzi uliopo katika utekelezaji wa miradi ya maendeleo.

Miongoni mwa ubaguzi huu, Mrema anabainisha, ni ule uliotokea hivi karibuni ambapo Serikali kuu ilitenga Sh180 milioni kwa ajili ya ujenzi wa madarasa katika jimbo la Buyungu, lakini Kata ya Gwarama, chini ya Chadema, haikupewa hata shilingi moja. Lakini, Kata ya Kakonko, iliyopo chini ya CCM ilipatiwa Sh90 milioni.

“Huu ni mfano mmoja tu,” anasema. “Kuna maeneo mengi nchini ambapo hali kama hiyo inatokea.”

Mrema anasema hali hiyo haiwaogopeshi kama chama. “(Lakini) inatufanya tuwe na wasiwasi, kwani (huo mwenendo) unaigawa nchi katika matabaka ya kisiasa.”

Meya Chadema apingana na Mrema

Hata hivyo, Meya wa Jiji la Arusha, Calisti Lazaro anasema wazo kwamba Serikali inapendelea maeneo yanayoongozwa na CCM halipo katika jiji lake.

Kuthibitisha anachokisema, Meya huyo amasema hivi sasa jiji hilo linatekeleza miradi kadhaa ya maendeleo inayofadhiliwa na Serikali kuu kama vile ujenzi wa barabara, vituo vya afya na mingineyo.

“Tuseme kwamba kuna ubaguzi, basi sidhani kama Serikali inaweza kuufanya waziwazi,” anasema.

“Hata kama Serikali iamue kututenga (Jiji la Arusha) mapato yetu ya ndani yangetosha kutuwezesha kutekeleza miradi yetu ya maendeleo.”

Profesa wa Chuo Kikuu cha Kikatoliki cha Ruaha (RUCU), Gaudence Mpangala anakubaliana na utafiti ulionukuliwa hapo juu akifafanua kwamba suala la Serikali kupendelea maeneo yanayoongozwa na CCM ni jambo lisilopingika. Anatoa mfano wa tukio la mwaka jana tu ambapo taasisi ya Wakfu wa Mwalimu Nyerere (MNF) ilimtaka aiandalie watu mashuhuri kutoka mkoa wa Iringa ambayo ilitaka kujadiliana nao kama sehemu ya juhudi za taasisi hiyo kukuza amani na utulivu nchini.

Profesa Mpangala anakumbuka kwamba jambo kubwa lililokuwa limetawala katika mjadala huo ni kutengwa kwa kata zinazoongozwa na upinzani katika ugawaji wa miradi ya maendeleo.

“Lengo kuu la yote haya ni kuonyesha kama watu wanataka maendeleo basi waichague CCM na kwamba kama watachagua upinzani hawatayapata (hayo maendeleo).”

Ubaguzi na migogoro

Lakini, Profesa Mpangala anaonya kwamba kama tabia hiyo itaendelea bila kuingiliwa kati inaweza kusababisha kuibuka kwa migogoro ya kijamii kutokana na manung’uniko kutoka kwa jamii zinazodhani kwamba zinatengwa.

Kwa sababu ya tofauti za kipato katika maeneo mbalimbali ya nchi inaweza kuwa ngumu kutuliza hasira za wale wanaolalamikia kubaguliwa. Hii ni kwa sababu “licha ya kwamba kodi wanakusanya wananchi wote wengine wanapata mgao (na) wengine hawapati.”

Profesa Mpangala anawakumbusha wanasiasa wanaojitahidi kuhubiri amani akisema amani haiwezi kuja katika mazingira ya ubaguzi na kutengwa.

“Maendeleo ya nchi lazima yasambazwe kwa usawa nchi nzima. Msingi wa migogoro mengi ya kijamii ni kwenda kinyume na kanuni hiyo.”

Madhara mengine ya ubaguzi anayoyaona Profesa Mpangala ni kifo kwa vyama vya upinzani na hivyo kurudi kwenye mfumo wa chama kimoja. Ikifikia hapo, anaonya msomi huyo, basi taifa zima litakuwa katika hali ya mtafaruku.

“Uamuzi wa kuanzisha mfumo wa vyama vingi katika siasa zetu ulikuwa ni wa kitaifa,” anabainisha Profesa Mpangala na kwamba kuuawa kwake kutakuwa na madhara kwa taifa zima.

Misingi ifuatwe

Profesa Mpangala anasema kwamba njia pekee ya kuiepusha nchi kudhurika ni kufuata na kuheshimu sheria na taratibu za demokrasia ya vyama vingi. “CCM inahitaji kufikiria upya vitendo vyake. Inahitaji iheshimu mfumo wa vyama vingi na kuhakikisha inavitendea vyama vyote sawa kama wadau wa maendeleo.”

Wito huu unafanana na ule unaotolewa na Mrema anayesema kwamba juhudi za makusudi zinapaswa kuchukuliwa kuzuia taifa kupasuka kwani hilo likitokezea hakuna mtu atabaki salama.

Anasema kuna haja kwa serikali na chama tawala kuelewa kwamba nchi ni moja na hisia za kutengwa huzaa uasi. “Serikali lazima itumikie watu wake bila kuendekeza ubaguzi,” anashauri.

Khalifa Said ni mwandishi MCL anapatikana kwa +255 716 874 501 au [email protected]

 

Chanzo: mwananchi.co.tz