Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwenyekiti CCM alaani mauaji kiongozi wa Chadema

97519 Pic+mauaji Mwenyekiti CCM alaani mauaji kiongozi wa Chadema

Sat, 29 Feb 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Manyoni. Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Manyoni,  Jumanne Mahanda  amevitaka vyombo vya Dola kuwasaka na kuwakamata waliohusika katika mauaji ya kiongozi wa Chadema wa wilaya hiyo, Alex Magubi.

Mahanda ametoa kauli hiyo leo Jumamosi Februari 29, 2020 katika ibada ya mazishi ya kada huyo wa Chadema mkazi wa Majengo mjini Manyoni mkoani Singida ambaye mwili wake ulikutwa umepigwa na kitu chenye ncha kali Februari 25, 2020.

Amesema alikuwa akishirikiana na Magubi kuwaletea maendeleo wakazi wa Manyoni licha ya kuwa vyama tofauti.

"Mimi ni mwana CCM na kiongozi wa wilaya lakini nimeumizwa sana na tukio hili, naomba vyombo husika vichukue nafasi yao mapema sana na mhusika ajulikane," amesema Mahanda.

Mwenyekiti huyo amesema kwa mara ya mwisho walikuwa na Magubi katika kikao cha baraza la madiwani wa halmashauri ya Manyoni wiki moja iliyopita.

Leo vilio na simanzi vilitawala wakati mwili wa Magubi ambaye ni mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Manyoni ukiwasili  nyumbani kwake mtaa wa Majengo Mjini Manyoni ukiwa umebebwa na vijana wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini Tanzania huku wakiimba nyimbo mbalimbali.

Habari zinazohusiana na hii

Advertisement
"Tumechoka kuuawa, tutajilinda wenyewe, tumechoka kuuawa, tutajilinda wenyewe," wamesikika wakiimba vijana hao waliovalia sare za chama hicho.

Februari 27, 2020 Kamanda wa Polisi mkoani Singida, Sweetbert Njewike amesema Magubi ambaye kituo chake cha kazi kilikuwa Mwembeni mjini mwili wake uliokotwa mbugani mbali na barabara, ukiwa umechomwa chomwa sehemu mbalimbali za mwili ikiwemo kichwani na miguuni.

“Wakati mwili wa Alex ukiokotwa mbugani, pikipiki yake iliokotwa kanda ya barabara iendayo Dodoma. Baada ya mwili kukaguliwa alikutwa na vitu vyote isipokuwa simu. Chanzo cha mauaji hayo bado hakijafahamika, upelelezi unaendelea,” amesema.

“Tunaomba mwananchi yeyote mwenye taarifa sahihi juu ya tukio hilo atoe kwenye kituo chochote cha polisi kilicho karibu au mamlaka zingine ili watu\mtu aliyehusika aweze kukamatwa na kufikishwa mbele ya vyombo vya sheria,” amesema.

Kuhusu marehemu kuwa kiongozi wa Chadema wilayani Manyoni, Njewike alisema hilo wamelisikia lakini walipofanya utafiti imebainika kuwa alikuwa ni dereva wa bodaboda tu na sio kiongozi wa Chadema.

Wakati Kamanda Njewike akisema kuwa Magubi hakuwa kiongozi wa Chadema, Mwenyekiti CCM Halmashauri ya Itigi, Alli Minja akizungumza na Mwananchi amesema marehemu alikuwa mwenyekiti Chadema Wilaya ya Manyoni.

“Binafsi nasikitika kwamba sitohudhuria mazishi yake kutokana na kukosa usafiri. Alex alikuwa Chadema wa aina yake,” amesema na kuongeza;

“Alikuwa na utamaduni wa kuhudhuria vikao vya mabaraza ya madiwani katika Halmashauri ya Wilaya ya Manyoni na kwetu huku Itigi. Kwenye suala la miradi ya maendeleo, ulikuwa huwezi kujua kama ni wa upinzani. Alikuwa anatoa ushirikiano wa hali ya juu. Mungu aiweke roho yake mahali pema peponi,” amesema Minja.

Chanzo: mwananchi.co.tz