Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwenyekiti CCM Mara awalipua mafisadi

5e7abf73ff6202ad20252e0a8b8a97d3 Mwenyekiti CCM Mara awalipua mafisadi

Tue, 8 Feb 2022 Chanzo: www.habarileo.co.tz

Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Samuel Kiboye amewalipua watendaji wa vijiji na madiwani mkoani Mara akidai kuwa ni wala rushwa, wabadhirifu, wanatumia vibaya madaraka na yupo tayari kuwataja.

Kaboye aliyasema hayo jana wakati akizungumza kwenye sherehe za uwekaji jiwe la msingi, ujenzi wa chujio la maji katika mradi wa maji Bunda, mkoani Mara.

Alimuahidi Rais Samia kuwa atampelekea majina ya watu wote wanaopokea rushwa wakiwemo madiwani wanaochukua zabuni za halmashauri kinyume cha sheria.

“Mkoa wa Mara wanaopokea rushwa nitakuletea majina yao hata leo hii (jana) na wengine wako serikalini. Nakuambia ukweli wengine wanaweza kuniwekea sumu kwenye maji ili nife na wengine wameniambia siwezi kuwataja kwa kuwa mwaka huu kuna uchaguzi, mimi namtegemea Mungu tu,” alisema Kaboye.

Alisema sheria inakataza kuchukua zabuni kwenye halmashauri lakini kuna madiwani wanachukua zabuni hizo.

“Hizo halmashauri nitakuja nikuambie CCM haitamuonea mtu aibu, awe kiongozi yeyote katika Mkoa wa Mara anayevunja kanuni na katiba ya chama sisi tutamshughulikia,” alisema Kaboye.

Aliongeza: “Hatuwezi kumuacha mtu awe na kiburi au awe yuko juu kuliko chama. Maagizo yote uliyoyatoa tutayafanyia kazi na tutakuletea taarifa.”

Alitoa mfano kuwa kuna msaada ulitolewa na Shirika la Hifadhi za Taifa (Tanapa) katika Halmashauri ya Tarime Sh milioni 240 inunulie gari la kuchimba maji ya visima lakini hadi sasa gari hilo halijanunuliwa na akadai kuwa fedha hizo zimeliwa.

“Mheshimiwa Rais, mie nawashukuru watu wa Tanapa, wanafanya kazi vizuri hapa Bunda ndio maana walisema wasilipwe hata posho. Tanapa wanatoa msaada kwa vijiji vinavyowazunguka lakini hawataki kusema. Mheshimiwa Rais nakuambia pesa ya Tanapa inaliwa na hivi vijiji,” alisema Kaboye.

Alisema ana majina ya waliokula fedha hizo na atayawasilisha kwa Rais Samia akasema na akaomba kiongozi huyo wa nchi awachape viboko na awaweke ndani.

“Hatuwezi kukaa hapa Rais anachapa kazi halafu wengine wanachukua pesa, wanaweka matumboni mwao,” alisema Kaboye.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Mara, Ally Hapi alisema ameanza kutekeleza maagizo ya Rais Samia Suluhu Hassan kuwaweka pembeni watendaji wanaodaiwa kuhujumu miradi.

“Nataka kukuhakikishia tayari tumeanza kutekeleza maagizo yako. Jana hatujalala na wasaidizi wangu, tumekuwa na mashauriano na mazungumzo na waziri wetu na wakuu wa idara wale wote ulioagiza wakae pembeni tayari tumekwisha kufikisha maelekezo hayo,” alisema Hapi.

Alisema anafahamu kuwa muda si mrefu watapatikana wakuu wa idara kujaza nafasi za wale ambao wanadhaniwa wamehujumu Mkoa na hawajaweza kusaidia.

“Tumezungumza na waziri jana usiku na ametuambia mchakato wa kutuletea watu wapya, wazuri kwa ajili ya kuja kuendeleza kijiti cha mapambano kwenye mkoa wetu umeanza,” alisema.

Chanzo: www.habarileo.co.tz