Mwenyekiti wa Chama Cha Mapinduzi(CCM) Mkoa wa Dodoma Alhaj Adam Kimbisa amesema hatua aliyochukua Rais Samia Suluhu Hassan ya kutengua katazo la mikutano ya hadhara inathibitisha ukomavu alionao , weledi, uthubutu na nia nzuri ambayo kwa Watanzania.
Alhaj Kimbisa ameyasema hayo leo Januari 5,2023 jijini Dar es Salaam alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hatua iliyochukuwa na Rais Dk.Samia kuruhusu mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa nchini.
“Rais Dk.Samia Suluhu Hassan alikutana na viongozi wa vyama vyote vya siasa ikiwa ni sehemu ya muendelezo wa jitihada ambazo amekuwa akizifanya tangu aingie madarakani za kuhakikisha mazingira ya ufanyaji siasa yanaboreshwa ikiwa ni pamoja na kuimarisha hali ya demokrasia , uhuru wa vyombo vya habari , uhusiano na vyama vya siasa pamoja na uhuru wa kujieleza.
“Ni ukweli kuwa jitihada , nia na uthubutu wake sit u umekuwa nguzo muhimu ya kuchochea kasi ya mariadhiano ya kisiasa nchini bali zimechangia pakubwa kuondoa mkwamo wa kisiasa ulioshuhudiwa kwa miaka sita sasa.Hatua iliyochukuliwa na Rais Samia kuruhusu mikutano ya hadhara kwa vyama vya siasa inathibitisha ukomavu alionao,”amesema Kimbisa.
Amesema CCM Mkoa wa Dodoma kinaamini kuruhusiwa kwa mikutano ya hadhara kutaimarisha nguvu za kisiasa za Chama hicho, kutapanua wigo kwa wanachama wengi zaidi kutoa mawazo chanya kuhusu masuala yanayohusu Taifa lao na kufungua fursa kwa viongozi wa ngazi wa Chama wa ngazi zote kunadi na kutangaza hadharani mazuri yote yanayotekelezwa na Serikali.