Chadema ni miongoni mwa wadau wa kisiasa wanaoshiriki kuibua mawazo mbadala katika ujenzi wa Taifa kikiwa ni chama kikuu cha upinzani, hususani kukabiliana na shida ya ukosefu wa ajira kwa vijana.
Mwenyekiti wa Baraza la Vijana BAVICHA, John Pambalu, anazungumza na Nipashe katika mahojiano maalumu kueleza kuhusu juhudi za chama hicho chenye ushawishi mkubwa nchini miongoni mwa vile vya upinzani. Endelea…
SWALI: Unalizungumziaje tatizo la vijana kukosa ajira, ukiwa katika taasisi mojawapo ya kuongoza vijana?
JIBU: Dunia leo iko kibiashara na sisi CHADEMA tunaamini katika biashara. Mrengo wetu ni wa kati au ni kiliberali, huko soko linaamuliwa na mahitaji ya bidhaa na uzalishaji au upatikanaji. Kazi hizo zinahusisha rasilimali watu viwandani na kwenye huduma hivyo kwa sababu tumebadilika tunategemea soko liongoze uchumi.
Soko linaleta mabadiliko na namna ya kupata ajira, zamani tulikuwa na mpira wa kujitolea leo ni wa kulipwa kwa hiyo kila binadamu anastahili ujira kwa kazi anayoifanya na siyo kujitolea.
Kwenye sera yetu ya vijana, tutatumia sekta binafsi kutatua changamoto ya ukosefu wa ajira, kwa mfano tumeandaa namna ambavyo kijana anayeanza biashara hapaswi kutozwa kodi kwanza, yaani leo ndiyo anaanza na hapo hapo analipa kodi, ni lazima upewe muda maalum kujitafuta.
Lakini pia, tumeamua katika kila benki kutakuwa na dirisha maalum la kutoa mikopo kwa vijana. Aidha, benki zote za kibiashara zitatoa elimu ya biashara kwa vijana ili wawe na uwezo wa kurudisha mikopo na riba na kulipa kodi tofauti na sasa ambapo jukumu hilo sasa halijapewa kipaumbele.
SWALI: Tuambie BAVICHA mnapata wapi fedha za kufanyia harakati zenu?
JIBU: Chama kinatoa mchango wa fedha kwenye baraza, lakini pia tuna wanachama ndiyo wadau namba moja wa kuchangia kazi zetu, tumetengeneza wadau ambao ni vijana wenye umri wa chini ya miaka 35. Kwa ujumla vijana ndani na nje ya nchi ndiyo wahusika wakuu.
Wengine wapo katika taasisi binafsi, kuna diaspora hao wamekuwa na mchango mkubwa sana katika baraza letu. Tumelifanya kuwa la wanachama ili wajione wanamiliki. Matukio kama ya Siku ya Vijana Duniani yanagharimu mamilioni ya fedha na vijana ndiyo wanaoyafanikisha.
SWALI: Ni yapi mafanikio katika uongozi wako BAVICHA?
JIBU: Yako mengi, kwanza tumeandika sera ya vijana ya mwaka 2020 ambayo ina majibu ya matatizo mengi hasa ya kiuchumi yanayowakabili. Pia katika kipindi changu tumelifanya baraza kufanya harakati za kisiasa, bila kuegemea chama. Hapo zamani lilikuwa linafanya shughuli kwa kujificha kwenye chama, mfano kikienda sehemu fulani ndipo unawaona na BAVICHA.
Sisi tumeondokana na hali hiyo na katika mambo fulani tunaweza kusimama kupigania yale tunayoyaona yanahitaji kuzungumziwa na kupatiwa majibu kwa ajili ya jamii yetu. Kwa mfano, BAVICHA ilianzisha harakati ya kutembelea wafungwa magerezani na kupaza sauti ya kutaka kuachiwa kwa wafungwa wa kisiasa.
Ikumbukwe baada ya uchaguzi 2020 zaidi ya wanachama wetu 417 walikuwa wafungwa na mahabusu katika magereza mbalimbali.
Kwa hiyo kwenye harakati tuliweza kujipambanua wenyewe kwamba tunamudu kupigania haki bila kuegemea chama moja kwa moja. Katika oparesheni katiba mpya pamoja na kibano kikali cha uongozi wa hayati John Magufuli na kutuziba midomo, bado BAVICHA ilizunguka katika vijiji mbalimbali kuhamasisha na kutoa elimu ya katiba mpya. Aidha, tumehamasisha vijana kugombea nafasi mbalimbali za uongozi kwa mfano tumekuwa na wagombea vijana kwenye ngazi ya ubunge, kama Mwenyekiti nikiongoza kwa vitendo niligombea jimbo la Nyamagana, Julius Mwita aliyekuwa Katibu Mkuu wa baraza aligombea Musoma Mjini, Patrick Ole Sosopi alikuwa Isimani, Aisha Madoga Dodoma Mjini, Hadija Mwago Mbagala, na Neema Chozaile Geita Vijijini.
Kadhalika, tumewahamasisha vijana kushika nafasi za juu za maamuzi ndani ya chama, kwa mfano Mkoa wa Simiyu aliyekuwa Mwenyekiti wa Vijana Mkoa ndiye Mwenyekiti wa CHADEMA na katibu wake ndiye Katibu wa chama. Katika mikoa ya Mwanza na Kagera, vijana wametoka kwenye uongozi wa vijana kwenda uongozi wa chama kwa kifupi wameiva na wanaaminika.
Aidha, BAVICHA ninayoiongoza imeweza kuwafikia vijana wasomi wa vyuo vikuu na sasa wameingia kwenye siasa kwa kiwango kikubwa. Kamati tendaji ya baraza ninayoiongoza imeacha woga. Zamani vijana wasomi wa vyuo vikuu katika mikoa yote tulikuwa si zaidi ya watano, leo mambo yamebadilika.
SWALI: Umefanikiwa vipi kukabiliana na changamoto BAVICHA?
JIBU: Bado kuna shida ya ushiriki mdogo wa vijana wasomi katika siasa kwa kuhofia hatma zao katika ajira na mustakabali kwenye maisha. Wakati sisi tunaingia madarakani vijana wa vyuo vikuu walioanzia uongozi katika CHASO (CHADEMA Students Organisation), tulikuwa wachache hatukuzidi watano.
Hata hivyo, hali imebadilika kwa kiasi kikubwa, mathalani, viongozi wapya waliochaguliwa sasa katika wilaya na mikoa asilimia 80 wanatokea CHASO.
Kwa hiyo, tumefanikiwa kushawishi vijana wa vyuo vikuu kufanya siasa. Ni wazi kwamba wale waliokuwa wanadhani wakiingia kwenye siasa hawataajiriwa huo woga umetoweka, katika wachache waliokuwepo walikuwa wanawaza kwenda kwenye ubunge na udiwani, lakini sasa wameona wanawajibu wa kujenga taasisi yetu CHADEMA.
SWALI: Ni upi mwelekeo wako kisiasa katika siku zijazo?
JIBU: Ni kuendelea kukitumikia chama na wananchi katika nafasi yoyote watakayonipa, lakini pia nina mpango wa kurejea kugombea ubunge katika jimbo la Nyamagana 2025. Nina uhakika nitashinda na kuongoza wananchi kutatua changamoto mbalimbali zilizopo Nyamagana kwa sasa.
SWALI: Una maoni gani kuhusu sheria mpya za uchaguzi zilizopitishwa karibuni?
JIBU: Hii tunaweza kuita kupaka rangi kuficha ukweli lakini kimsingi hakuna mabadiliko tuliyotarajia na kimsingi hatuziungi mkono. Wameandaa Sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi wakati katiba haiitambui inachokilinda ni Tume ya Taifa ya Uchaguzi. Tunaona ni kukinzana sheria na katiba. Ikumbukwe popote panapokuwa na ukinzani, katiba ndiyo inayotumika.
Jambo la pili, uhuru wa tume siyo jina ni muundo na sisi tumekuwa tukipinga tume ya uchaguzi kuwa na watumishi wa umma tunataka iwe na maofisa wake kuanzia ngazi ya chini mpaka za kitaifa kwa ajili ya uchaguzi ulio huru na haki. Wametoa jina wakurugenzi na kuandika Ofisa Mwandamizi wa Serikali hapo wanacheza na akili za watu.
Wakurugenzi ni maofisa waandamizi wa serikali ukweli unabaki kuwa matatizo ya tume si ya kisheria ni ya katiba. Watu wanataka kuwe na mgombea binafsi, katiba inakataa, wanataka haki ya kupinga matokeo ya urais mahakamani, sheria imekataza kwa hiyo vitu vingi bado haviko sawa.
Vilevile watu tuliamini kwamba itakapotungwa sheria ya Tume Huru ya Uchaguzi, itatumika uchaguzi wa mwaka 2025 lakini, inataka wajumbe wa tume waliopo sasa kuendelea kusimamia uchaguzi hadi utumishi wao utakapokoma.