Siku chache baada ya kuchaguliwa kuwa Mwenyekiti wa Chama cha ACT- Wazalendo Mkoa wa Shinyanga, Chrisant Msipi ametangaza kukihama chama hicho na kujiunga CCM.
Msipi amejiunga CCM leo Januari 28, 2024 na kupokewa na Katibu wa Itikadi, Uenezi na Mafunzo wa chama hicho, Paul Makonda katika mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Sabasaba, Manispaa ya Shinyanga. Mkutano huo ulilenga kusikiliza kero za wananchi wa mkoa huo.
"Nimekaa nikafikiri, nikaona nirudi nyumbani si mkongwe kwenye siasa, nilikuwa askari polisi Mkoa wa Shinyanga, nilichaguliwa uenyekiti wa ACT-Wazalendo wiki moja iliyopita naomba kurudisha kadi," amesema Msipi.
Alipotafutwa Naibu Katibu wa Itikadi, Mawasiliano na Uenezi wa ACT- Wazalendo, Janeth Rithe, ameieleza Mwananchi Digital kuwa hana taarifa ya kiongozi wao kuhamia CCM.
Hata hivyo, amesema kama hilo ni kweli, ametumia haki yake ya kidemokrasia.
"Kachagua ndiyo uamuzi wake, demokrasia ndivyo ilivyo, mtu kaamua leo kuwa chama A, kesho chama B, tunamtakia kila la kheri. Huu ndiyo uhuru wa demokrasia, hatuna maelezo mengine," amesema Rithe.
Mbali ya hilo, Rithe amesema Shinyanga na Ruvuma ni miongoni mwa maeneo wanayotarajia kurudia uchaguzi kutokana na ujanjaujanja uliofanyika.
"Nadhani Msipi amenusa uamuzi wa Kamati Kuu iliyoketi jana Jumamosi Januari 27, 2024 katika Ofisi ya Makao Makuu Magomeni," amesema Rithe.
Makonda baada ya kumpokea Msipi amesema: "Kaka yangu Zitto Zubeir Kabwe (Kiongozi wa ACT-Wazalendo), si mimi ni kazi za Rais Samia Suluhu Hassan zimemvuta mwenyekiti wako wa mkoa, kama utakosa gharama za uchaguzi tuambie CCM tutakusaidia.
"Lakini ufahamu hizi ni salamu kabla ya mwaka 2025, kwa hiyo ACT- Wazalendo hawana mwenyekiti wa mkoa wa Shinyanga jamani pole. Nimesema si mimi ni Rais Samia, uongozi wote wa mkoa sasa mwenyekiti akiondoka mambo si yameharibika," amesema Makonda.