Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwanzo mwisho wasaidizi wa Mnyika kukamatwa

90400 Mnyika2+pic Mwanzo mwisho wasaidizi wa Mnyika kukamatwa

Tue, 31 Dec 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. “Askari polisi waliotukamata walikuwa kwenye moja ya magari manne yaliyofuatilia msafara wa Katibu Mkuu (John Mnyika)kuanzia ofisi za Chadema Kanda ya Victoria eneo la Kitangiri.”

Hiyo ni kauli ya Ofisa Habari wa Chadema namsaidizi binafsi wa Mnyika, Abdulkarim Muro alipozungumza na Mwananchi kwa njia ya simu jana kuhusu tukio la yeye na dereva wa katibu mkuu huyo, Said Haidan kukamatwa, kuhojiwa, kushikiliwa kwa muda kabla ya kuachiwa na polisi.

Alisema kabla ya kuwafuatilia kutoka Kitangiri hadi Mahina, magari hayo awali yaliegeshwa jirani na ofisi za chama hicho wakati Mnyika alipofika kusalimiana na viongozi wa Kanda ya Victoria.

“Tulikamatwa tukiwa ndani ya eneo la hoteli ya Paradise muda mfupi tu baada ya Katibu Mkuu (John Mnyika) kuondoka na rafiki yake aliyemfuata pale hotelini tulikoenda kumsubiria mama mzazi wa Mnyika aliyekuwa kwenye shughuli ya kifamilia,” alisema Muro.

Pia, alisema kabla ya kuingia ndani ya hoteli na kuwakamata, maofisa hao wa polisi waliegesha gari lao nje ya geti na kusalia ndani ya gari kwa kipindi kirefu na baada ya kuwakamata, waliwahoji alipo Mnyika.

Alisema askari hao pia waliwahoji wameingia lini Mwanza na wamepanga kufanya shughuli gani.

“Licha ya kuwaeleza kuwa tuko Mwanza kwa ziara na shughuli binafsi ya kifamilia ya katibu mkuu; wao (polisi) walidai wana taarifa tumepanga kufanya vikao na mikutano ya kisiasa,” alisema.

Muro aliyedai walipigwa na askari hao kuwashinikiza kueleza alipokuwa Mnyika, alisema tukio hilo liliibua taharuki kwa wateja na uongozi wa hoteli uliokuwa ukihoji hatima ya gari na mali zao zilizokuwa eneo la hoteli hiyo, ndipo mmoja wa askari alipolazimika kuandikisha maelezo ya kukamatwa kwao kwenye kitabu cha kumbukumbu cha hoteli hiyo.

“Kama wanadai tulikamatwa nyumba jirani huo ni uongo. Nenda pale hotelini utapata ukweli wote kwa sababu tukio lile lilitokea hadharani watu wakishuhudia,” alisema Muro.

Pia, alisema licha ya polisi kuwakamata saa 10:30 jioni, askari hao walizunguka nao kwenye gari huku wakiegesha kwa muda katika nyumba moja kwenye eneo asilolifahamu kutokana na ugeni wake jijini Mwanza wakidai Mnyika alikuwemo ndani ya nyumba hiyo.

“Kuna wakati Mnyika alinipigia simu yangu ambayo walishaichukua nikawasihi wanipe nimjulishe kuwa wanamtafuta ili atoke nje kama yupo ndani ya nyumba ile au aende kituo cha polisi; lakini askari wale waligoma,” alisimulia Muro.

Alisema baada ya kuzunguka maeneo mbalimbali jijini Mwanza, askari hao waliwapeleka katika moja ya vituo vidogo vya polisi bila kuwaingiza kituoni, badala yake walisalia ndani ya gari iliyoegeshwa nyuma ya jengo la kituo hicho.

“Muda wote walikuwa wakiwasiliana kwa njia ya simu na watu wengine tusiowafahamu. Mwisho tulisikia wakielekezwa watupeleke Kituo Kikuu cha Polisi Mwanza tulikofikishwa saa 4:30 usiku na kuswekwa mahabusu bila kuandikishwa maelezo hadi saa 6:00 tulipotolewa, kuandika maelezo na kujidhamini,” alisema na kuongeza

“Tumeripoti leo asubuhi (jana) na kuelezwa kuwa upelelezi unaendelea na tutaitwa tukihitajika. Lakini tumepewa sharti la kutotoka nje ya Mwanza bila kutoa taarifa polisi,” alisema Muro.

Akizungumza na Mwananchi kwa simu jana, Mkurugenzi wa Mawasiliano, Itifaki na Mambo ya Nje ya Nje wa Chadema, John Mrema licha ya kupinga maelezo ya Polisi, pia alilaani kushikiliwa kwa maofisa hao huku akilisihi jeshi hilo kufanya kazi kwa weledi kwa kutojiingiza kwenye siasa kwa kuwadhibiti viongozi, wanachama na wafuasi wa vyama vya upinzani.

“Mbona katibu mkuu wa CCM (Chama Cha Mapinduzi) anazunguka kila sehemu nchini akifanya vikao vya ndani na kuhutubia mikutano ya hadhara bila kubughudhiwa na polisi. Maofisa wetu ambao wako Mwanza na katibu mkuu (John Mnyika) kwa mapumziko na shughuli ya kifamilia walikamatwa wakiwa ndani ya eneo la Hoteli ya Paradise.”

Chanzo: mwananchi.co.tz