Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwanzo mwisho alichochambua Lissu Ripoti ya Kikosi Kazi

Lissu Mwanzo mwisho alichochambua Lissu Ripoti ya Kikosi Kazi

Sat, 29 Oct 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wakati baadhi ya waliokuwa wajumbe wa kikosi kazi cha Rais cha kuchakata maoni ya demokrasia, wakitetea mapendekezo waliyotoa katika ripoti yao, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu amefichua udhaifu uliopo kwenye mapendekezo ya kikosi hicho.

Ripoti hiyo ilikabidhiwa kwa Rais Samia Suluhu Hassan Oktoba 21 jijini Dar es Salaam, ikiwa na mapendekezo 18 yaliyogusa mchakato wa mabadiliko ya Katiba, mfumo wa uchaguzi na mengineyo.

Kikosi hicho kilichotumia miezi tisa kuandaa ripoti hiyo kiliundwa baada ya kufanyika kwa mkutano ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa na kufunguliwa na Rais Samia Desemba 15 hadi 17 jijini Dodoma.

Hata hivyo, ripoti hiyo imeonyesha utata wa kupatikana kwa Katiba mpya na tume huru ya uchaguzi. Mchakato wa Katiba.

Akizungumza juzi usiku wakati wa mjadala wa ripoti ya kikosi kazi ulioandaliwa na Mwananchi kupitia jukwaa mtandao la Twitter Space, Makamu Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu alisema kikosi kazi kimerudia kosa la kihistoria tangu uhuru la kuweka mchakato wa Katiba kwenye mikono aliyosema siyo salama ya Rais.

Alitoa mfano wa mabadiliko ya Katiba yaliyofanyika miaka ya 1962, 1965, 1977, 1984 na 1992 akisema yalikosa uhalali kwa sababu Rais aliyekuwa madarakani, ndiye alikuwa mwenye uamuzi wa mwisho.

“Tunahitaji kuondokana na huo mzigo mzito wa kihistoria wa Rais kutawala mchakato wa Katiba. Kikosi hakitusaidii kwa hilo kabisa,” alisema Lissu.

Awali akichambua ripoti hiyo, Kiongozi wa ACT- Wazalendo, Zitto Kabwe aliyeanza kuchangia katika mjadala huo, alisema walipendekeza njia za kuukwamua mchakato huo.

“Kikosi kazi kimependekeza kwamba, hatua ya kwanza ni lazima kuwe na mkutano wa kitaifa ili tujadili mambo yaliyotukwamisha.

“Hatua ya pili ni kupeleka bungeni muswada wa sheria ya kufanya mabadiliko kwenye Sheria ya Mabadiliko ya Katiba.

Alitaja pia hatua ya kuhuisha Sheria ya Kura ya maoni kabla ya kuundwa kwa jopo la wataalamu, ambalo alisema wamependekeza liwe na watu watano tu kwa pande zote za Muungano.

“Muswada huo ukitoka hapo unakwenda kwenye kura ya maoni na tumependekeza hatua moja kabla ya kura za maoni, kuwe na kazi kubwa ya elimu kabla ya kupiga kura ya maoni,” alisema.

Lakini alipoulizwa kwa simu jana, aliyekuwa Makamu Mwenyekiti wa kikosi hicho, Hamad Rashid alisema walikubaliana kuwa rasimu hiyo isipelekwe kwenye Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

“Hao wataalamu wakishatoa taarifa yao ndiyo waipeleke kwenye Bunge na siyo kwa Rais na tukasema Bunge lililopo sasa hivi halifai kwa sababu ni la CCM, kwa hiyo lazima tupate Bunge lenye mjumuisho wa watu wengi,” alisema.

Hata hivyo, ukurasa wa 184 wa ripoti ya kikosi kazi umesema; “Baada ya jopo la wataalamu kukamilisha kazi ya kuandaa Rasimu ya Katiba, itawasilishwa katika Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa ajili ya kujadiliwa na kuipitisha kuwa Katiba Inayopendekezwa.”

Mfumo wa uchaguzi

Akichambua mapendekezo kuhusu mfumo wa uchaguzi, Lissu alisema kikosi kazi hicho kimeendeleza mfumo uleule wa uchaguzi uliofeli.

“Tume inayopendekezwa na kikosi kazi itakuwa ni tume ya Rais ya uchaguzi kama ilivyo Tume ya Taifa ya Uchaguzi na Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, zimekuwa ni tume za Rais za uchaguzi.

“Rais ndiye atakayeteua makamishina wote. Anapelekewa majina ndiyo, makamishna wako saba, makamishna wanne ndio anaamua yeye mwenyewe,” alisema.

Hata hivyo, Hamad Rashid alipoulizwa kuhusu pendekezo hilo alisema: “Makamishna wanaomba, siyo kuteuliwa.

“Mwenyekiti na Makamu (wa tume huru ya uchaguzi) wote wataomba na majina yatapelekwa Rais,” alisema.

Lakini ukurasa wa 53 wa ripoti hiyo unasema: “Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi ambaye anapaswa kuwa ni jaji wa Mahakama Kuu au Mahakama ya Rufani aliye madarakani au mstaafu na makamu mwenyekiti ambaye anapaswa kuwa na sifa ya kuwa Jaji wa Mahakama Kuu au mstaafu, wateuliwe na Mheshimiwa Rais bila kufuata utaratibu wa kuomba na kusailiwa na kamati ya uteuzi.”

Watumishi wa umma kusimamia chaguzi

Huku akirejea ripoti za waangalizi wa uchaguzi wa kimataifa kwa chaguzi za Tanzania, Lissu alisema miongoni mwa changamoto zilizoorodheshwa, ni matumizi ya watumishi wa umma kusimamia chaguzi. “Ukisoma taarifa za watazamaji wa chaguzi zetu tangu mwaka 1995, wanazungumzia matatizo makubwa mawili ya tume kutokuwa huru.

“La kwanza ni Rais kuhodhi mamlaka ya kuteua makamishina na la pili ni watumishi kusimamia chaguzi. “Sisi tulioshiriki chaguzi tangu miaka hiyo, tunafahamu hao watumishi wa umma ni watu wa CCM asilimia 100 kwa 100 na ni tatizo kubwa, watazamaji wamesema miaka yote kwamba tume iwe na watumishi wake yenyewe,” alisema.

Kwa mujibu wa ripoti ya kikosi kazi ibara ya 5.6.5 (a) inasema, “Tume iendelee kutumia watumishi wa umma kusimamia uchaguzi; watumishi wa umma wawajibike moja kwa moja kwa Tume ya Uchaguzi kwa masuala yanayohusu shughuli za uchaguzi kwa mujibu wa sheria.”

Mbali na hayo, Lissu aligusia mapendekezo aliyoyaita ya hatari zaidi ya kumpa Msajili wa Vyama vya Siasa kuwa msimamizi wa ndani ya vyama. Hamad Rashid alisema wamependekeza hivyo, baada ya kubaini mfumo wa chaguzi ndani ya vyaama una upungufu.

Wakat huohuo, Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro alikosoa hatua Chadema kususia majadiliano. Alisema hatua ya vyama kususia majadiliano, imesababisha malalamiko zaidi hata baada ya ripoti kutoka. “Kwa maoni yangu ni muhimu vyama kukaa kwa pamoja tusipofanya hivyo yale yaliyotokea mwaka 2014 yatajirudia,” alisema.

Naye mwanahabari mkongwe, Absalom Kibanda alimpongeza Rais Samia kwa kuanzisha Kikosi Kazi akisema, “Ni halali kama taifa tutafika mbali, kikosi kazi ni mapendekezo sio amri kwa hiyo tusifungane sana.”

Alisema licha ya Chadema kususia kikosi hicho, wamekuwa na mazungumzo na Rais Samia aliyeamua kushirikisha vyama.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live