Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwanzo Mwisho kesi ya kina Mdee ilivyokwenda…

MDEE NA WENZAKEEE Mwanzo Mwisho kesi ya kina Mdee ilivyokwenda…

Mon, 18 Dec 2023 Chanzo: Mwananchi

Desemba 14,2023, Mahakama Kuu ya Tanzania kupitia kwa Jaji Cyprian Mkeha ilibatilisha uamuzi wa Baraza Kuu la Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), lililobariki kuvuliwa uanachama Halima Mdee na wenzake 18.

Kamati Kuu ya Chadema, iliwavua uanachama kwa madai ya kuapishwa kuwa wabunge wa viti maalumu wakati kamati hiyo ilikuwa haijafanya uteuzi wowote wa nafasi hizo kwa mujibu wa ibara ya 7.7.16(a) ya katiba ya chama hicho.

Mdee na wenzake, walivuliwa uanachama wa chama hicho na Kamati Kuu ya Chadema, Novemba 27,2020, wakakata rufaa Baraza Kuu la chama hicho ambalo liliketi Mei 12,2022 kusikiliza rufaa hiyo na kubariki uamuzi ya Kamati Kuu.

Wengine waliovuliwa uanachama ni Grace Tendega, Ester Matiko, Ester Bulaya, Agnesta Kaiza, Anatropia Theonest, Asya Mohamed, Cecilia Paresso, Conchesta Rwamlaza, Felister Njau, Hawa Maifunga, Jesca Kishoa na Kunti Majala.

Katika orodha hiyo pia wamo Naghenjwa Kaboyoka, Nusrat Hanje, Salome Makamba, Sophia Mwakagenda, Stella Fiyao na Tunda Malapo ambao wote kwa pamoja hawakuridhika na uamuzi wa Baraza Kuu kubariki uamuzi ya Kamati Kuu.

Wanachama hao walifungua maombi namba 36/2022 Mahakama Kuu ya Tanzania dhidi ya wajibu maombi watatu, wakipinga uamuzi ya baraza hilo.

Wajibu maombi hao ni Bodi ya wadhamini ya Chadema kama mjibu maombi wa kwanza, Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) kama mjibu maombi wa pili na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG) kama mjibu maombi wa tatu katika kesi hiyo.

Suala la wabunge hao limekuwa likivuta hisia kutoka kwa wanachama wa Chadema na baadhi ya Watanzania, hivyo kesi hiyo ilikuwa ni moja ya kesi zilizokuwa zikifuatiliwa na makundi mbalimbali kujua ukweli wa kilichotokea.Kuanzia leo, tutawaletea hatua kwa hatua tangu ilipofunguliwa kesi hiyo, kusikilizwa na hatimaye kutolewa uamuzi. Katika kuwaletea simulizi hii ya kesi, tutaegemea katika hukumu ya Mahakama.

Jaji alivyoeleza kiini cha kesi

Katika hukumu hiyo, Jaji Mkeha alianza kutoa utangulizi wa kiini cha kesi hiyo ambapo alisema Oktoba 28, 2020 kulifanyika Uchaguzi Mkuu wa Rais na Wabunge ambapo Chadema, kilikuwa moja ya chama kilichoshiriki uchaguzi.

Kulingana na matokeo rasmi ya uchaguzi huo iliyotangazwa na Tume ya Taifa Uchaguzi (NEC) kwa kuzingatia ibara za 66(1(b), 67(1)(a) na (b) na 78(1) ya Katiba ya Tanzania, Jaji alisema Chadema walistahili kupata mgawo wa viti maalumu 19 katika Bunge la Tanzania.

Jaji alisema kulingana na vifungu 86(2), (6) na (7) vya Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, chama cha siasa kilicho na haki ya kupata idadi yoyote ya viti maalumu, kingewasilisha NEC majina ya wanawake wanaostahili kuteuliwa na tume.

Baada ya kupokea majina hayo, tume itateua majina ya wabunge wa viti maalumu na baada ya kutangaza majina, NEC itapeleka majina hayo kwa Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na kwa katibu mkuu wa chama husika. Jaji alisema Novemba 24, 2020, waleta maombi yaani akina Mdee na wenzake 18, walionekana katika runinga ya TBC1 wakila viapo vya kuwa wabunge wa viti maalumu kwa udhamini wa Chadema ikimaanisha majina yalipelekwa na Chadema.

Jioni ya Novemba 25,2020, Katibu mkuu wa Chadema, John Mnyika, alitoa taarifa kwa umma akilaani kitendo cha Mdee na wenzake 18 kwamba kuapishwa kwao kulikiuka maelekezo ya chama ya kutoutambua uchaguzi mkuu wa 2020. Kupitia tangazo na jumbe kupitia kundi songozi (Whatsapp), Katibu Mkuu Chadema alitoa wito kwa waleta maombi kufika mbele ya Kamati Kuu asubuhi ya Novemba 2020 kujieleza kwa nini walichukua nafasi hizo na kuapishwa.

Kilichowafanya waitwe

Katika ujumbe huo, waleta maombi (Mdee na wenzake), walitakiwa kujieleza kwanini walichukua nafasi hizo na kuonyesha walikuwa wamedhaminiwa na Chadema bila kuzingatia taratibu za chama na msimamo wake kuhusu uchaguzi.

Baada ya kupokea wito huo, waleta maombi wote waliomba kikao hicho kilichokuwa kimepangwa kufanyika Novemba 27,2020 kiahirishwe na kwa bahati mbaya, wote walitoa sababu inayofanana ya kwanini wanataka kiahirishwe.

“Kila mleta maombi alimwandikia barua katibu mkuu akidai uwepo wa tishio la usalama wao. Wote waliomba ahirisho la siku 7 ili hali itulie, kupata eneo salama zaidi na muda wa kujiandaa na usikilizwaji ili watoe utetezi wao wa haki,”alisema.

Ombi la ahirisho lilikataliwa na Kamati Kuu ya Chadema kwa barua walizotumiwa na Katibu mkuu ambazo zinadaiwa kupokelewa na waleta maombi kwa wakati tofauti tofauti usiku wa manane wa Novemba 26 na asubuhi ya Novemba 28.

“Licha ya ahirisho lao kukataliwa, hakuna mleta maombi hata mmoja aliyehudhuria usikilizwaji wa shauri lao tarehe 27.11.2020 na Kamati Kuu (Ya Chadema) ikaendelea na kikao bila uwepo wa waleta maombi,” alisema Jaji.

“Kamati Kuu ikaamua kuwa Tume (NEC) iliwateau kimakosa waleta maombi ambao baadae waliapishwa kuwa wabunge wa viti maalumu wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kamati Kuu iliamua dhidi yao,” alieleza Jaji.

“Waleta maombi wote 19 walifukuzwa uanachama wa Chadema. Katika kupinga uamuzi wa kamati kuu, waleta maombi walikata rufaa baraza kuu la Chadema kwa mujibu wa Katiba ambacho ni chombo cha mwisho cha rufaa” Jaji alieleza kuwa Mei 11,2022, Baraza Kuu la chama hicho lilibariki maamuzi yaliyokuwa yamefanywa na Kamati Kuu, ya kuwafukuza uanachama.

Walichoiomba Mahakama

Jaji Mkeha alisema waleta maombi waliwasilisha maombi hayo kuiomba mahakama kutoa amri ya kubatilisha uamuzi uliopitishwa na Baraza Kuu la Chadema Mei 11,2022 na mchakato mzima wa kuwafukuza uanachama.

Pia waliomba mahakama kuwaamuru wajibu maombi kuwapa waleta maombi haki ya kusikilizwa na haki ya asili (natural justice) wakati wanashughulikia masuala yanayohusu haki zao na pia wasitekeleza uamuzi wa Baraza Kuu.

Maombi hayo yaliungwa mkono na maelezo ya waleta maombi hao, viapo 19 vya waleta maombi na kiapo cha pamoja (joint affidavit) cha waleta maombi kujibu kiapo cha mjibu maombi wa kwanza ambaye ni Baraza la Wadhamini Chadema.

Kwa upande wa pili, Jaji alisema maombi hayo yalipata upinzani kupitia majibu wa mjibu maombi wa kwanza ambaye ni Baraza la wadhamini Chadema na pia viapo kinzani (counter affidavit) vya mjibu maombi huyo wa kwanza katika kesi hiyo. Mjibu maombi wa pili na wa tatu hawakuwasilisha kiapo chochote kinzani.

Mawakili waliochuana

Waleta maombi waliwakilishwa na mawakili Ipilinga Panya, Aliko Mwamanenge, Edson Kilatu, Emmanuel Ukashu, Humphrey Malenga, Matinde Waissaka na Joyce Mwakapila wakati mjibu maombi wa kwanza alitetewa na mawakili watatu.

Mawakili Peter Kibatala akisaidiana na Jeremiah Mtobesya na Hekima Mwasipu wakati mjibu maombi wa pili na watatu walitetewa na jopo la mawakili mawakili wa Serikali 10, wakiongozwa na wakili wa Serikali mkuu, Jeska Shengena.

Mawakili waliosaidiana na wakili Shengena kuchuana kortini na wakili Kibatala na wenzake ni Stanley Kalokola, Boaz Msoffe, Ayoub Sanga, Mathew Fuko, Masunga Kamihanda, Leonia Maneno, Kause Kilonzo, Lilian Mirumbe na Frida Mollel.

Kwa nini Jaji alikubali mashahidi

Jaji Mkeha alisema maombi hayo yalishughulikiwa si tu kwa kuzingatia utaratibu wa kushughulikia kesi za maombi ya marejeo (Judicial review cases) unavyotaka, lakini pia ilipokea majibu ya baadhi ya viapo vya waleta maombi wa kesi hiyo.

Halikadhalika ilipokea majibu ya viapo kutoka upande wa wajibu maombi wa kwanza ambao katika mazingira nadra, walifika mahakamani na kuulizwa maswali ya dodoso kuhusiana na kile walichokiapa katika viapo walivyoviwasilisha.

Jaji alisema hiyo ilitokea baada ya wakili Kibatala kuwasilisha ombi la kupata nafasi ya kuwauliza maswali ya dodoso mleta maombi wa 1 (Halima), 2 (Tendega), 3 (Matiko), 4 (Bulaya), 8 (Paresso), 11 (Mwaifunga), 12 (Kishoa) na 15 (Hanje). Wakili Kibatala alijenga hoja kuwa kuna taarifa muhimu zitakazotumika kuamua maombi hayo zimefichwa na waleta maombi hao, ombi ambalo halikupingwa na upande wa waleta maombi lakini nao wakatoa tuhuma kama hizo hizo.

Kwa hiyo upande wa waleta maombi nao wakawasilisha ombi kama hilo la kutaka mahakama iwape nafasi ya kuwauliza maswali ya dodoso wote waliotoa viapo kwa wajibu maombi, ombi ambalo nalo halikupngwa na wajibu maombi.

Jaji alisema katika kulikubali ombi hilo, maana yake mahakama inahama kutoka utaratibu uliozoeleka wa kushughulikia maombi ya marejeo kwa maana ya mashahidi kuhojiwa maswali ya dodoso, utaratibu ambao ni nadra kutokea.

“Hata hivyo kwa kuzingatia maslahi ya umma (public interest) katika mgogoro huu na haja ya kuamua kwa uwazi na haki, nilikubali maombi hayo,”alisema Jaji akiruhusu utaratibu huo aliosema ni nadra.

Usikose mwendelezo wa kesi hii kesho

Chanzo: Mwananchi