Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mwanakotide wa Chadema afariki dunia

78838 Pic+chadema

Mon, 7 Oct 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Kada wa Chadema,  Fulgence Mapunda maarufu Mwanakotide amefariki dunia jana Jumapili Oktoba 6, 2019 katika Hospitali ya St Monica, Dar es Salaam.

Mwanakotide alikuwa mtunzi na mwimbaji wa nyimbo za hamasa za chama hicho, alijizolea umaarufu kupitia mikutano ya hadhara ya chama hicho, zikiwemo kampeni za uchaguzi mkuu wa mwaka 2010 na 2015.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Oktoba 7, 2019  Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano wa Chadema, Tumaini Makene imesema msiba upo  Mikocheni, nyumbani kwa kaka wa Mwanakotide.

“Chadema imepokea kwa masikitiko na majonzi makubwa taarifa za msiba Mwanakotide ambaye alianza kufanya kazi na chama tangu mwaka 2005.”

“Kupitia kipaji chake cha utungaji na uimbaji wa nyimbo za hamasa za mapambano ya siasa alifanya kazi ya kuieneza Chadema nchi nzima, kwa imani kubwa ya utumishi wa kisiasa,” amesema Makene.

Amesema tangu wakati huo Mwanakotide amejizolea sifa na umaarufu mkubwa kutokana na kutumia ipasavyo kipaji chake hicho, akiwakilisha itikadi, imani, falsafa na misimamo ya Chadema ndani na nje ya mipaka ya Tanzania, kupitia sanaa ya nyimbo.

Pia Soma

Advertisement

Makene amesema hadi mauti inamkuta, Mwanakotide  alikuwa mtumishi wa Makao Makuu ya Chadema kama ofisa anayeshughulikia masuala ya sanaa na wasanii tangu mwaka 2006.

“Chama kwa kushirikiana na familia kilikuwa kinagharamia matibabu yake hadi umauti ulipomkuta jana usiku,” amesema Makene.

Amesema Chadema kimepoteza mmoja wa wapiganaji wake mahiri wa mstari wa mbele katika mapambano.

“Tunatoa salaam za pole kwa familia ya Mwanakotide, viongozi, wanachama, wapiganaji wenzake na Watanzania wote wapenda mabadiliko ambao wameguswa na msiba huu ambao pia kwa namna moja au nyingine waliguswa na kazi za msanii huyu mahiri,” amesema.

Chanzo: mwananchi.co.tz