Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mvutano vyama vingi ulianza uchaguzi wa 1958

98584 UCHAGUZI+PIC Mvutano vyama vingi ulianza uchaguzi wa 1958

Tue, 10 Mar 2020 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Oktoba mwaka huu, Watanzania wenye sifa za kupiga kura watapata fursa ya kumchagua Rais, wabunge, wajumbe wa Baraza la Wawakilishi na madiwani ambao watawaongoza kwa miaka mitano ijayo.

Historia inatukumbusha kuwa Tanzania ilianza kufanya uchaguzi wake mkuu tangu enzi za ukoloni na kushirikisha vyama vingi.

Miongoni mwa vyama hivyo ni kile cha Tanganyika African National Union (Tanu) kilichoanzishwa Jumatano Julai 7, 1954.

Miaka minne baadaye, mwaka 1958, kulifanyika uchaguzi wa kwanza wa kitaifa uliohusisha vyama vingi vya siasa.

Serikali ya Gavana Edward Twining iliyokuwa ikiiongoza Tanganyika miaka hiyo, ilielemewa katika uchaguzi huo ambao Tanu, ikiongozwa na Mwalimu Julius Nyerere, ilielekea kupata ushindi mkubwa.

Baada ya Serikali ya kikoloni kuona inaelemewa katika uchaguzi huo, ilikubali ufanyike uchaguzi wa Baraza la Kutunga Sheria ambao viti vilikuwa vishindaniwe kwa misingi ya rangi ya ngozi ya mtu.

Pia Soma

Advertisement
Serikali ya Twining ililazimisha wapiga kura wapige kura tatu, moja kwa ajili ya wazungu, moja kwa wahindi na moja kwa waafrika.

Masharti mengine ya kumwezesha mwafrika kupiga kura yalimtaka awe na kipato cha paundi 400 za Kiingereza kwa mwaka, awe na kiwango cha elimu ya darasa la 12 na awe ameajiriwa katika kazi maalumu.

Akizungumza na Mwananchi hivi karibuni nyumbani kwake Ukerewe, Mwanza, Spika mstaafu Pius Msekwa alisema masharti hayo yalikuwa magumu na lengo lake lilikuwa ni kuikwaza Tanu katika uchaguzi huo.

Kufuatia masharti hayo, Tanu iliamua kufanya mkutano wake mkuu mwaka 1958 mjini Tabora kwa siku sita kuanzia Januari 21-26.

Alisema mkutano huo ulijadili iwapo kulikuwa na ulazima wa kushiriki katika uchaguzi chini ya masharti ya kibaguzi yaliyowekwa au isusie uchaguzi.

Hata hivyo, inaelezwa kuwa katika mkutano huo wa Tabora ziliibuka kambi mbili kubwa zilizoibua mvutano mkali uliotishia kuivunja Tanu vipande viwili.

Kambi moja ni ile ya wenye siasa za wastani waliopendelea kushiriki katika uchaguzi na ya pili ni ile ya wenye msimamo mkali waliotaka uchaguzi ususiwe kabisa.

Tanu ilinusurika na kile ambacho kingeweza kuwa mgogoro ndani ya chama ambao ungewafanya wale wenye msimamo mkali kama Sheikh Suleiman Takadir, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Tanu katika makao makuu, Zuberi Mtemvu, wakati huo katibu mwenezi wa Tanu, kufanya mapinduzi ambayo yangekigawa chama vipande mawili.

Kambi ya Mwalimu Julius Nyerere ambayo ilikuwa na viongozi akiwamo Abdallah Rashidi Sembe na Hamisi Heri, iliamua kuwa Tanu lazima itashiriki uchaguzi huo. Lakini kambi ya Mtemvu ambaye wakati huo alikuwa katibu mwenezi wa Tanu na Sheikh Suleiman Takadir, Mwenyekiti wa Baraza la Wazee wa Tanu katika makao makuu, ilikuwa na msimamo mkali. Waligoma kushiriki uchaguzi.

Kutokana na mvutano huo, Mtemvu na wafuasi wake walijiondoa Tanu wakikataa kushiriki uchaguzi wa ‘kura tatu’, wakaanzisha chama kingine cha siasa kupambana na Tanu.

Chama hicho kilijulikana kwa jina la African National Congress (ANC).

Uchaguzi wenyewe

Uchaguzi wa awamu ya kwanza ulifanyika Septemba 8 na 12, 1958, ulihusisha majimbo matano ya Tanganyika ukishirikisha vyama vingi.

Tanu ilishinda viti vyote vitano vya waafrika wakati ushindi wa viti vinane kati ya 10 vya wazungu na wahindi uliangukia kwa wagombea waliokuwa wapenzi wa Tanu.

Baada ya matokeo hayo, Julai ya mwaka huo, Gavana Twining aliondoka na badala yake akaja Gavana Richard Turnbull ambaye kwa kuona ushindi na kasi ya Tanu, aliamua kuanza kufanya kazi na chama hicho.

Mzunguko wa pili wa uchaguzi ulifanyika Februari 9 na 15, 1959. Katika uchaguzi huo Tanu ilishinda viti 28 kati ya 30 vilivyogombewa katika Baraza la Kutunga Sheria.

Mbali na Tanu pia vilikuwapo vyama vya All Muslim National Union of Tanganyika (AMNUT), United Tanganyika Party (UTP) na Chama cha African National Congress (ANC).

Vyama hivyo vilivaana katika Jimbo la Tanga ambako kina Mtemvu waligombea. Katika Jimbo hilo, John Keto wa Tanu (3,555), Petro Chambuya Mntambo wa Tanu (1,854), Zuberi Mtemvu wa ANC (53) na Paul Nkanyemka wa ANC (49).

John Keto alitangazwa kuwa mjumbe wa Baraza la Kutunga Sheria kwa Jimbo la Tanga.

Walikuwapo pia wagombea binafsi katika uchaguzi huo ambao walikuwa raia wenye asili ya India, Krishna Beldev (kura 3,550), Mohamed Hussain (1,435), Fazelabbas Sylemanji Khambalia (350), Mukhtar Ahmed Ayaz (76) na mzungu, Roderick Neville (3,439).

Chama cha UTP kilimsimamisha mzungu mmoja, David Lead kuwa mgombea wake na alipata kura 1,972.

Katika uchaguzi huo, Mwalimu Nyerere aliwahi kugombea kiti cha jimbo la Mashariki akishindana na Chifu George Kunambi ambaye alisimama kama mgombea binafsi. Nyerere alipata kura 2,628 dhidi ya kura 802 za Kunambi.

Kwa mujibu wa historia, majimbo yaliyofanya uchaguzi Septemba 1958 ni Kaskazini, Mashariki, Magharibi, Tanga na Nyanda za Juu Kusini. Majimbo yaliyobaki yalifanya uchaguzi Februari 1959.

Awali, Keto alikuwa mwalimu katika Shule ya Sekondari Minaki iliyofunguliwa Desemba 5, 1925, ikiwa moja ya shule tatu za sekondari kongwe, baada ya Shule ya Wavulana Tabora na St Marys. Keto alikuwa miongoni mwa walimu wa Minaki na alikuwa amefanya kazi kubwa walipoanza kufungua matawi ya Tanu maeneo ya Kisarawe kulikokuwa na matawi 173.

Kutokana na kazi yake nzuri, Tanu iliamua kumteua agombee kiti nyumbani kwao Tanga ambako alishinda.

Mwaka 1960 ulifanyika uchaguzi wa wabunge na Tanu ikaendeleza ushindi wake kwa kupata viti 70 kati ya 71 vilivyokuwa vikishindaniwa.

Baada ya ushindi huo, Desemba 9, 1961 Tanganyika ilipata uhuru na Mwalimu Nyerere akawa Waziri Mkuu, chini ya usimamizi wa Malkia Elizabeth wa Uingereza, wajumbe wengine 34 wa baraza hilo waliteuliwa na vyama vya siasa.

Januari mwaka 1962 Mwalimu Nyerere alijiuzulu wadhifa huo na Rashid Kawawa akachukua nafasi yake. Nchi ikawa Jamhuri na ilianza kujiandaa kwa ajili ya uchaguzi wa Rais Novemba 1962.

Katika uchaguzi huo, Tanu kilikabiliana na ANC na wapiga kura walikuwa milioni 1.8 waliojiandikisha. Tanu ilishinda kwa asilimia 98.15 na Nyerere akawa Rais wa Tanganyika. Na hapo ndipo mfumo wa vyama vingi ulifutwa na Tanganyika ikawa na mfumo wa chama kimoja.

Mwanzo wa chama cha Mtemvu

Tanganyika African National Congress (TANC) ni chama kilichoanzishwa na Mtemvu.

Chama hiki kilianzishwa wakati wa uchaguzi wa mwaka 1958 kwa jina la Tanganyika African Congress baada ya mwanasiasa huyo kujiengua Tanu.

Lakini kiliponyimwa usajili Mei 1958, kililazimika kubadili jina kutoka Tanganyika National Congress na kuitwa African National Congress.

Kilishiriki katika uchaguzi wa Septemba 1958 kwa kugombea kiti kimoja miongoni mwa vitano.

Katika kiti hicho, Mtemvu aligombea dhidi ya mgombea wa Tanu, Keto na mgombea wa UTP na Mntambo wa Jimbo la Tanga.

Katika kinyang’anyiro hicho, Mtemvu alishindwa vibaya baada ya kupata kura 53, Keto 3,455 na Mntambo 1,854.

Matokeo yake chama chake hakikushiriki mzunguko wa pili wa uchaguzi uliofanyika Septemba 1959.

Hata hivyo, katika uchaguzi huo enzi za ukoloni, kulikuwa na masharti mazito ya kukwamisha Waafrika kupata viti vingi.

Miongoni mwa masharti yaliyowekwa na serikali ya kikoloni ni sifa za kuandikishwa kuwa mpiga kura ambazo zilikwamisha watu wengi.

Mathalan, katika Wilaya ya Bagamoyo walioandikishwa kupiga kura walikuwa 630 wakati idadi ya wakazi ilikuwa 89,000.

Chanzo: mwananchi.co.tz