Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Muunganiko wa Dk Tulia, Zungu gumzo

Muunganiko Pic Data (600 X 341) Muunganiko wa Dk Tulia, Zungu gumzo

Fri, 11 Feb 2022 Chanzo: mwananchidigital

Chama cha Mapinduzi (CCM), juzi kilimpitisha rasmi Mbunge wa Ilala, Mussa Azzan Zungu kugombea unaibu spika ulioachwa wazi na Dk Tulia Ackson ambaye Februari mosi, 2022 alichaguliwa kuwa Spika wa Bunge.

Dk Tulia alipata kura 376 (zote) akiwashinda wenzake wanane wa vyama pinzani waliowania kiti hicho kilichoachwa na aliyekuwa Spika, Job Ndugai ambaye alijiuzulu wadhifa huo Januari 6, mwaka huu.

ungu huenda akapata kura nyingi katika uchaguzi utakaofanyika kesho kwakuwa hakuna mbunge wa chama kingine aliyetangaza kuwania nafasi hiyo.

CCM ndicho chama chenye wabunge wengi bungeni na vikao vya Kamati Kuu kwa nyakati tofauti vilipitisha jina la Dk Tulia kuwania uspika na Zungu kuwania unaibu spika hivyo hata kama angetokea au atatokea mpinzani kuwania nafasi husika nafasi ya kushinda ni finyu .

Hivyo, baadhi ya wachambuzi, walisema kuchaguliwa kwa Zungu ambaye amekuwa Mwenyekiti wa Bunge kwa kipindi kirefu, kunakwenda kuifanya safu ya uongozi wa Bunge kukamilika rasmi kesho pale kura zitakapopigwa.

Kwa mujibu wa Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977, kazi kuu ya msingi ya Bunge ni kuwakilisha wananchi, kutunga sheria, kuishauri na kuisimamia Serikali kwa niaba ya wananchi ambao ndio wenye mamlaka yote yaliyokasimiwa kwa viongozi wa umma.

Hata hivyo, wachambuzi na wadau wa siasa nchini wanatofautiana katika mtizamo, baadhi wakiamini Dk Tulia na Zungu, wataleta mabadiliko chanya katika uongozi wao huku wengine wakisema hawatarajii mabadiliko yoyote.

“Kitaaluma, Dk Tulia ni mwanasheria, ana uzoefu wa kusimamia na kufuata kanuni na ameonyesha hivyo kwa miaka sita akiwa Naibu Spika. Ni dhahiri ataendelea hivyo,” alisema Dk Onesmo Kyauke, mchambuzi wa masuala ya kisiasa alipozungumza na Mwananchi jana.

Dk Kyauke ambaye ni wakili na mhadhiri wa zamani wa sheria Chuo Kikuu cha Dar es Saalam alisema ushirikiano wa wawili hao utaleta mabadiliko chanya yatakalipa Bunge uwezo wa kuisimamia na kuishauri vema Serikali.

“Alipokuwa Naibu Spika, yapo mambo na vitu ambavyo Dk Tulia alikuwa hawezi kufanya, sasa yeye ndiye mkuu wa mhimili wa Bunge, ni dhahiri ataleta mabadiliko chanya,” alisema Dk Kyauke akijibu swali kwanini mabadiliko anayoyatarajia kwa viongozi hao hayakuonekana wakati wakiwa kenye nyadhifa zao za awali

Kauli ya matumaini kwa uongozi mpya wa Bunge pia ilitolewa na Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (Saut), Profesa Costa-Ricky Mahalu aliyesema umahiri wa Spika Tulia katika masuala ya sheria na kanuni ukichanganywa na uzoefu wa Zungu katika uongozi kwenye ofisi za umma utaleta mabadiliko chanya katika uongozi wa Bunge.

“Zungu ni mzoefu wa uongozi katika ofisi za umma kuanzia ubunge, uwaziri na Mwenyekiti wa Bunge na Spika Tulia pia anao uzoefu wa miaka sita katika masuala ya uongozi wa Bunge. Mchanganyiko huu utaleta mabadiliko katika uendeshaji wa shughuli za Bunge,” alisema Profesa Mahalu, Balozi wa zamani wa Tanzania nchini Italia.

Mhadhiri na mkuu huyo wa zamani wa Kitivo cha Sheria cha Chuo Kikuu cha Dar es Salaam alitaja eneo jingine linaloongeza imani kuwa wawili hao wataongoza Bunge kwa weledi ni hulka na tabia yao ya kuhoji na kuwa na msimamo katika masuala ya msingi walipokuwa wasaidizi wa Spika Ndugai.

“Naamini hawataacha wala kufuata yote ya yaliyotokea katika uongozi uliopita. Ni lazima watataka kutengeneza na kuacha alama yao. Natarajia mabadiliko chanya kutoka kwao,” alisema Profesa Mahalu.

Heche na Bulendu waonyesha hofu

Akizungumzia uongozi wa Bunge chini ya Dk Tulia na Zungu, mbunge wa zamani wa Tarime Vijijini, John Heche (Chadema) alisema historia ya uongozi wa wawili hao unafifisha matumaini ya mabadiliko kulinganisha na Bunge lililopita.

“Dk Tulia na Zungu walikuwa wasaidizi wa Spika Ndugai katika kipindi ambacho Bunge lilipoteza hadhi ya kuaminika mbele ya umma kutokana na kuonekana kama muhuri wa kupitisha kila jambo la Serikali bila kuhoji hata kama inakinzana na mahitaji na maslahi ya umma. Sitarajii lolote jipya kutoka kwao,” alisema Heche

Kiongozi huyo wa zamani wa Baraza la Vijana wa Chadema (Bavicha) alisema “kiuhalisia, wawili hawa, Dk Tulia na Zungu wataendeleza mtindo wa uongozi ulioufanya Bunge kuonekana liko chini ya mamlaka ya Serikali,”

Akijibu swali la nini kifanyike ili Taifa lipate Bunge lenye viongozi mahiri watakaolinda hadhi kwa kuufanya mhimili huo kujisimamia na kujitegemea, Heche alitaja kupatikana kwa Katiba mpya itakayobadili mfumo wa uongozi unaoipa Serikali misuli dhidi ya mihimili mengine ya dola ya Bunge na Mahakama.

“Kwa katiba ya sasa, Rais ambaye pia ni Mwenyekiti wa CCM ndiye anayeongoza vikao vya kuwateua na kuwapitisha Spika na Naibu wake. Rais huyo huyo pia ndiye anamteua Jaji Mkuu. Ni wazi viongozi hao hawawezi kwenda kinyume kwa kupinga au kuhoji lolote linaloletwa na mteuzi wao,” alisema Heche

Naye Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino (Saut), Dotto Bulendu alisema Katiba, muundo na mfumo wa uongozi nchini kuwa sababu ya kutotarajia makubwa kutoka kwa Dk Tulia na naibu wake Zungu.

“Utayari wa dola (Serikali) kuiacha mihimili mengine ya Mahakama na Bunge kufanya kazi kwa uhuru na kwa kujitegemea haupo. Mahakama na Bunge hazifurukuti mbele ya Serikali, huo ndio ukweli unaotokana na mfumo wetu unaolindwa na Katiba Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977,” alisema Bulendu

Alisema japo Spika Tulia ni mwanasheria mwenye uwezo na uzoefu katika masuala ya kanuni na Zungu ni mzoefu katika uongozi wa umma, viongozi hao hawawezi kuleta mabadiliko kutokana na mfumo wa uongozi uliopo nchini.

“Moja ya tatizo letu ni kwamba tulichobadilisha wakati tunarejesha mfumo wa vyama vingi mwaka 1992 ni sentensi tu kuwa tunatoka mfumo wa chama kimoja kwenda vyama vingi; vitu vyote na mifumo yote imeendelea kusalia kama mwanzo. Sitarajii mabadiliko bila katiba mpya itakayobadilisha mfumo,” alisema Bulendu, ambaye ni mwandishi nguli wa habari

Matarajio ya umma

Akitoa maoni yake kuhusu Spika wa Bunge ambaye umma unamhitaji wakati wa mahojiano maalumu na Mwananchi mwezi uliopita, Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kirutheri Tanzania (KKKT), Askofu, Dk Fredrick Shoo alisema Spika wa Bunge anapaswa mtu jasiri mwenye uwezo wa kusimamia, kulinda, kuheshimu na kufuata kanuni bila hofu wale upendeleo.

“Spika wa Bunge lazima awe mtu anayeweza kulinda heshima ya Bunge katika mijadala, maamuzi na kazi ya kuisimamia na kuishauri Serikali bila kuingiliwa na mihimili mingine ya dola. Awe mtu anayeamini katika mihimili kuheshimiana na kushirikiana bila kuingiliana,” alisema Dk Shoo katika mahojiano hayo ya Januari 15.

Chanzo: mwananchidigital