Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Muswada kudhibiti fedha haramu wapitishwa Bungeni

Bungeni Peji 11 Aprili 21, 2021 Muswada kudhibiti fedha haramu wapitishwa Bungeni

Wed, 9 Feb 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Bunge limepitisha Muswada wa Marekebisho ya Sheria ya Kudhibiti Utakatishaji Fedha Haramu wa mwaka 2022.

Muswada huo ulipitishwa jana bungeni Dodoma baada ya kujadiliwa na wabunge.

Wengi wao walimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa kufanikisha muswada huo kuwasilishwa bungeni kwa hati ya dharura, wakisema kumeiweka nchi katika nafasi nzuri kimataifa.

Walipongeza usikivu wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali na wizara yenye dhamana ya fedha kutokana na kukubaliana na mapendekezo mbalimbali kwenye vifungu na hivyo kurahisisha upitishwaji wake.

Akiwasilisha muswada huo, Waziri wa Fedha na Mipango, Dk Mwigulu Nchemba alisema una lengo la kuondoa changamoto na upungufu uliobainishwa katika Ripoti ya Tathmini ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mifumo ya nchi ya udhibiti wa utakatishaji wa fedha haramu, ufadhili wa ugaidi na ufadhili wa silaha za maangamizi.

Alisema tathmini ilifanywa na Umoja wa Nchi za Mashariki na Kusini mwa Afrika wa Kupambana na Utakatishaji wa Fedha Haramu mwaka 2021 na Tanzania ni mwanachama.

Alisema matokeo yalibainisha upungufu katika sheria hiyo unaotokana na mabadiliko ya viwango vya udhibiti wa utakatishaji wa fedha haramu, ufadhili wa ugaidi na ufadhili wa silaha za maangamizi pamoja na matumizi ya teknolojia mpya katika uhalifu.

Kwa mujibu wa Dk Mwigulu, matokeo hayo yamesababisha serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuwekwa chini ya uangalizi hadi pale itakaporekebisha upungufu huo.

"Endapo marekebisho ya sheria hii hayatafanyika ili kuondoa upungufu huo, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania itawekwa katika orodha ya nchi zenye mifumo ya fedha hatarishi na hivyo kuleta athari hasi kisiasa, kijamii na kiuchumi," alisema Mwigulu.

Alitaja athari nyingine ni kuathiri ushirikiano na uhusiano wa kibiashara na uwekezaji na jumuiya ya kimataifa na kupunguza fursa za misaada na mikopo kutoka kwa washirika wa maendeleo.

Alisema hali hiyo vile vile itadhoofisha ushirikiano wa kikanda na kimataifa.

“Tayari Umoja wa Ulaya umeijulisha Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kuhusu madhara yatakayojitokeza iwapo hatutatekeleza mapendekezo ya Ripoti ya Tathmini ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ndani ya muda uliowekwa," alisema.

Katika sheria ya utakatishaji fedha, marekebisho yamefanyika katika vifungu mbalimbali kikiwamo cha 14 kuwawajibisha viongozi wa kampuni wenye wadhifa wowote kwa makosa yanayofanywa na kampuni.

Kwenye Sheria ya Kuzuia Ugaidi, Sura ya 19, miongoni mwa marekebisho ni pamoja na kuweka kifungu kinachofafanua vitendo vya kigaidi kuwa ni pamoja na kutisha au kusababisha woga kwa umma au sehemu ya umma, kutisha au kulazimisha serikali au taasisi ya kimataifa kufanya au kutofanya kitendo chochote.

Vitendo vingine vya ugaidi ni kuvuruga utulivu au amani ya nchi au ya taasisi ya kimataifa kidini, kisiasa, kikatiba, kiuchumi au kijamii.

Vile vile waziri mwenye dhamana ya mambo ya ndani ya nchi amepewa uwezo kumtambua na kumtangaza mtu yeyote, kampuni au taasisi yoyote kuwa ni mshukiwa wa ugaidi wa ndani ya nchi kwa kuzingatia sifa au vigezo vilivyowekwa na Azimio Na. 1373 la Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa dhidi ya ugaidi.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live