Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Musukuma kuinadi CCM kwa helikopta Arusha

10235 MSUKUMA+PIC TanzaniaWeb

Mon, 6 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Monduli. Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Kasheku ‘Musukuma’ amesema ataanza kutumia helikopta wiki ya mwisho ya kampeni ili kuhakikisha ushindi katika kata zote za jimbo la Monduli na Arusha Mjini unakwenda CCM.

Akizungumza jana Jumamosi Agosti 4, 2018 katika mkutano wa kampeni kumnadi mgombea wa CCM kata ya Migungani wilayani Monduli, Benedict Mawala, Musukuma amesema lengo ni chama tawala kuibuka na ushindi.

Uchaguzi katika jimbo la Buyungu na kata 77 utafanyika Agosti 12 mwaka huu.

"Kuanzia wiki ijayo nitakuja na helikopta nitakuwa na Kalanga (Julius-aliyekuwa mbunge wa Monduli kwa tiketi ya Chadema) tutaruka na helikopta kufanya mikutano,” amesema.

Musukuma amewataka wakazi wa kata hiyo kutofanya makosa kwa kumchagua diwani wa Chadema kwa maelezo kuwa wengi waliobaini ukweli, wamerejea CCM kama ilivyo kwa Kalanga aliyejiuzulu uanachama wa Chadema na kujiunga na chama hicho tawala.

Kwa upande wake Mawala amewaomba wakazi wa kata hiyo kumchagua tena kuwa diwani kwa maelezo kuwa amerejea CCM chama kinachoongoza Serikali.

“Nimerejea nyumbani naomba mnichague nitashirikiana na Serikali kuwaletea maendeleo na kufanya yale niliyowaahidi wakati nikiwa upinzani,” amesema.

Katika jimbo la Monduli utafanyika uchaguzi  katika kata tatu baada ya wagombea wengine watatu wa CCM kupita bila kupingwa.

Katika jimbo la Arusha Mjini uchaguzi utafanyika katika kata  nne. Wagombea wote wa CCM awali walikuwa madiwani wa kata hizo kwa tiketi ya Chadema.

Chanzo: mwananchi.co.tz