Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Musukuma: Nilitarajia kuikuta Machame kama ilivyo Marekani

15473 Pic+msukuma TanzaniaWeb

Tue, 4 Sep 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Hai. Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku maarufu ‘Musukuma’ amesema alitarajia kuikuta kata ya Machame Uroki kama Marekani kimaendeleo kumbe sivyo hivyo.

Kutokana na hali hiyo, mbunge huyo anayetamba ndiye pekee anayetetea wanyonge bungeni, alisema anawapa pole wakazi wa kata hiyo.

Musukuma aliyasema hayo juzi wakati akizungumza kwenye mkutano wa kampeni uliofanyika katika viwanja vya soko la Bwani, ambapo aliwataka wananchi wa kata hiyo wasirudie makosa ya mwaka 2015 ya kuchagua upinzani.

“Kwanza niwape pole sana, mimi nilitegemea huku nitapakuta kama Marekani, kumbe na nyie shida ni zilezile kama za usukumani, poleni sana,” alisema.

Alisema wananchi walifanya makosa na kutumika kwa muda mrefu na sasa Mungu amewapa maziwa ili kuondoa sumu na diwani amerudi CCM, hivyo wanapaswa kubadilika na kumchagua diwani anayetokana na CCM, Robson Kimaro awaletee maendeleo ya kweli.

Musukuma aliahidi kwamba wakichagua CCM, umeme utafika katika vijiji vyote ambavyo havijafikiwa na kwamba nguzo zitafika siku za karibuni.

“Tumekuja hapa kuwaomba, mchagueni diwani wa CCM, hamtajuta na hapa tutaweka lami eneo lililobaki la kilometa nne, kwani hela tunayo,” alisema.

Alisema pamoja na kata hiyo, pia wanalihitaji jimbo hilo la Hai linaloongozwa na Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe lirudi CCM kwa kuwa wananchi wameteseka kwa muda mrefu.

Mbunge wa Mbinga Mjini, Sixtus Mapunda alisema mwaka 2015 wananchi walimchagua mchezaji mzuri, lakini alikuwa kwenye timu mbovu na sasa amerudi kwenye timu nzuri hivyo wasifanye makosa.

Akiomba kura, Kimaro alisema kwa sasa ameingia kwenye eneo lenye matumaini ili kuwaletea wananchi maendeleo.

Chanzo: mwananchi.co.tz