Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Muliro aagiza uchunguzi muuza matunda anayedaiwa kubaka watoto

5401f55526c331d0c3023bd35cedd656.png Muliro aagiza uchunguzi muuza matunda anayedaiwa kubaka watoto

Mon, 13 Jun 2022 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema ameshatoa maelekezo ya kukamilishwa kwa uchunguzi kuhusu kesi inayomkabili Joshua Simangwe (66) anayetuhumiwa kuwafanyia ukatili wa kingono wanafunzi wa shule za msingi na chekechea za Airwing na Minazi mirefu mkoani Dar es Salaam.

Maelezo ya Kamanda Muliro yamekuja huku kukiwa na malalamiko ya wazazi na watoto wanaodaiwa kudhalilishwa kutaka Simangwe, maarufu kwa jina la Babu Chacha afikishwe mahakamani haraka.

Akizungumzia na HabariLEO kuhusu kadhia hiyo, Kamanda Muliro alisema: "Nimetoa maelekezo ya kukamilishwa haraka kwa uchunguzi wa suala hilo ili mtuhumiwa afikishwe mahakamani."

Simangwe alikamatwa na polisi Mei 27 mwaka huu kwa tuhuma za kuwafanyia ukatili wa kingono watoto wa shule hizo za msingi na chekechea.

Anadaiwa kuwapeleka watoto katika nyumba iliyo jirani na shule hizo inayotumika kwa ajili ya kufanyia mazoezi na yeye kukabidhiwa funguo kwa ajili ya kuhifadhi vifaa vyake vya biashara ya matunda anayoifanya jirani na shule hizo.

Wakizungumza na HabariLEO jana, wazazi hao wa watoto watatu ambao wamefungua jalada la kesi katika Kituo cha Polisi cha Sitakishari walisema ni takribani wiki mbili na siku kadhaa sasa tangu kukamatwa kwa mtuhumiwa huyo ambaye sasa yuko nje kwa dhamana.

"Siku ya tukio la kukamatwa tulienda polisi na tukaandika maelezo yote na taratibu zote tumefuata, sasa ni muda tunasubiri kesi iendelee lakini mtuhumiwa yuko mtaani, ameachiwa kwa dhamana. Tunaomba kesi ifikishwe mahakamani," alisema mmoja wa wazazi hao (jina linahifadhiwa).

Mzazi mwingine alisema kuwa wapo wazazi ambao watoto wao wemekumbana na vitendo hivyo vya kikatili lakini hawako tayari kuungana kutoa maelezo polisi wakidhani hawatapata haki.

"Wapo ambao ninawafahamu ambao watoto wao wamefanyiwa vitendo hivyo lakini hawako tayari kujihusisha na kesi kwa sababu ya woga na kudhani kwamba haki haitatendeka," alidai mzazi huyo ambaye mtoto wake anasoma Shule ya Msingi Minazi Mirefu.

Juni 10 ,2022 gazeti hili iliripoti tukio la wanafunzi katika shule hizo kudai kudhalilishwa kingono na muuza matunda anayefanya biashara katika eneo la shule hizo.

Imekuwa ikidaiwa kwamba wanafunzi zaidi ya 10 wa shule hizo wamefanyiwa vitendo hivyo na Simangwe anayeuza matunda katika eneo hilo kwa zaidi ya miaka 10.

Taarifa za Simangwe, Mkazi wa Kipunguni kudaiwa kufanya uovu huo ziliibuliwa mwezi uliopita baada ya mmoja wa mzazi wa watoto hao kuelezwa na mtoto wake alichofanyiwa.

Baadhi ya wazazi, uongozi wa Shule ya Msingi Airwing ulithibitisha kuwapo watoto wanaodai kufanyiwa vitendo hivyo. Mganga Mkuu wa Hospitali ya Rufaa wa Amana, Bryceson Kiwelu akithibitisha kuwapo wanafunzi wa shule hizo mbili waliofanyiwa vipimo na kugunduliwa kwamba wamedhalilishwa.

Mwalimu Msaidizi Shule ya Airwings, Fatihuba Karata alisema anazo taarifa za watoto wawili wanaodaiwa kufanyiwa vitendo hivyo waliopo shuleni hapo.

“Walikuja wazazi wawili ambao watoto wao wanasoma darasa la pili na darasa la awali wakasema kuwa watoto wao wamefanyiwa hivyo vitendo. Hivyo wazazi ndio walimkamata mtuhumiwa na kumpeleka polisi lakini sisi tulithibitisha kuwa ni kweli hao wanafunzi wawili wanasoma hapa,” alifafanua Karata.

Alisema walifanya kikao na wazazi ili kuwalinda watoto na wakakubaliana wawe wanawaleta hadi shuleni ambako hawawezi kutoka kwa sababu kuna uzio na kwenye lango yupo mlinzi.

Kwa upande wa Shule ya Msingi Minazi Mirefu, Mwalimu Mkuu, Brutu Msenga pia alithibitisha kuwapo kwa mwanafunzi aliyedai kufanyiwa kitendo hicho.

Wanafunzi waliohojiwa walisema walikuwa wakienda kwa mwanaume huyo ambaye walimrejelea kwa jina la ‘babu’ na kwamba alikuwa akiwapa matunda kabla ya kufanya vitendo hivyo huku akiwaonya wasimwambie mtu yeyote.

Mmoja wa watoto hao, huku akiwa na mzazi wake (majina yamehifadhiwa) alisema: “Rafiki yangu (jina limehifadhiwa) aliniambia twende kwa babu kwenye chumba cha mazoezi, akaniacha huko, babu akanifanyia kitendo kibaya halafu akanipa dawa nimeze na machungwa mawili, akasema nisimwambie mama wala mwalimu. Watoto wengi wanaenda ila mimi nimefanyiwa mara moja.”

Ilidaiwa kwamba mtoto mgeni aliyeenda kwa babu alikuwa akiambiwa kesho yake amlete rafiki yake ili naye ampatie matunda na juisi.

Hata hivyo, baadhi ya wafanyabiashara katika eneo hilo walisema hawana uhakika kama kweli ‘babu’ anaweza kufanya vitendo hivyo kwa namna wanavyomwona na kumfahamu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live