Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtoto wa Lowassa ajiondoa kinyang’anyiro cha ubunge Monduli

12143 MTOTO+PIC TanzaniaWeb

Thu, 16 Aug 2018 Chanzo: mwananchi.co.tz

Arusha. Kada wa Chadema, Fred Lowassa amejiondoa kwenye kinyang’anyiro cha wanaowania kuteuliwa na chama hicho kugombea ubunge katika Jimbo la Monduli mkoani hapa.

Fred ambaye ni mtoto wa Waziri Mkuu wa zamani, Edward Lowassa, alionyesha nia ya kuwania ubunge katika jimbo hilo baada ya kuchukua fomu wiki iliyopita kufuatia Julius Kalanga kujiuzulu uanachama wa Chadema na ubunge, na kuhamia CCM.

Kalanga ameshateuliwa na Kamati Kuu ya CCM kugombea ubunge katika jimbo hilo.

Akizungumzia uamuzi wa Fred, Katibu wa Chadema Mkoa wa Arusha, Amani Golugwa alisema baada ya kushauriana, vikao vya uteuzi vilikubali kuondoa jina lake.

“Ni kweli nathibitisha kuwa ameomba kwa sasa siyo wakati muafaka licha ya kuwa alionyesha nia awali na wananchi wengi walimuunga mkono, hivyo chama kimekubali maombi yake na kimempitisha mgombea mwingine,” alisema Golugwa.

Alisema Chadema imempitisha diwani wa Lepurko, Yonas Masiaya Laizer kuwania ubunge wa jimbo hilo.

Wiki iliyopita makada wanne wa Chadema akiwamo Fred walichukua fomu za kuwania ubunge katika jimbo hilo.

Aliwataja wengine waliochukua fomu kuwa ni Cecilia Ndosi ambaye ni mwenyekiti Baraza la Wanawake wa Chadema (Bavicha) Mkoa wa Arusha ambaye pia ni diwani wa viti maalumu.

Wengine ni Laizer, Lobulu Kivuyo na Eric Ngwijo. Wanachama wengine waliochukuwa fomu lakini hawakurejesha hadi muda wa mwisho uliowekwa na chama hicho ni Aroan Mashuve na Dafi Dafi.

Chanzo: mwananchi.co.tz