Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtolea awatangazia neema wana Temeke

49497 Pic+mtolea

Mon, 1 Apr 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Halmashauri ya Temeke imepata ufadhili wa Sh265 bilioni kwa ajili ya ukarabati wa miundombinu ikiwamo barabara.

Hayo yalisemwa jana na Mbunge wa Temeke kupitia Chama Cha Mapinduzi (CCM), Abdallah Mtolea katika mkutano na wana CCM wa jimbo hilo.

Mbunge huyo alisema alijiunga CCM mwishoni mwa mwaka jana akitokea Chama cha Wananchi (CUF) baada ya kujiuzulu nafasi hiyo na Januari 2019 aliapishwa Dodoma baada ya kusimamishwa na chama hicho tawala na kupita bila kupingwa kuwa mbunge wa jimbo hilo.

Alisema wakati wa uchaguzi mdogo wa ubunge wa jimbo hilo hakukufanyika kampeni ambayo ingemfanya atambuane na wana CCM Temeke ndiyo sababu ameona ni busara kuitisha mkutano huo ili watambuane.

Alisema katika mkutano huo, amezialika kamati za siasa za kata 13 na matawi yote ya CCM jimbo la Temeke hivyo kufanya wajumbe waliohudhuria kuwa 1,600.

Kuhusu fedha hizo, Mtolea alisema miongoni mwa barabara zitakazokarabatiwa kwa kiwango cha lami ni za kata ya Kilakala, Makangarawe na mfereji wa Keko unaosababisha mafuriko utajengwa kwa kiwango bora.

Alisema fedha hizo pia zitajenga barabara za Yombo Vituka na Buza pamoja na zahanati na vituo vya afya.

Aidha, Mtolea alisema pamoja na fedha hizo, kuna Sh 2 bilioni kwa ajili ya kuwakopesha vijana, wenye ulemavu na wakina mama waliopo katika vikundi vinavyojishughulisha na shughuli za maendeleo kwa ajili ya kuinua vipato vyao.

Mbunge huyo aliwataka walengwa hao waonane na maofisa ustawi wa jamii waliopo katika maeneo yao ili waweze kukopa fedha hizo.

Kwa upande wake, katibu wa CCM kata ya Kurasini, Mwanavita Mbarouk alisema amefurahishwa na hatua hiyo ya maendeleo na kumpongeza mbunge huyo.

Alisema maboresho yatakayofanywa kupitia fedha hizo yatasaidia kuinua maendeleo ya Temeke kwa kiwango kikubwa tofauti na awali.



Chanzo: mwananchi.co.tz