Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Mtifuano bungeni kukatika umeme, Musukuma, Kishoa waja juu, Makamba atoa majibu

Bunge La Tz Musukuma asema sababu za kukatika umeme hazina msingi

Wed, 16 Feb 2022 Chanzo: www.mwananchi.co.tz

Mbunge wa Geita Vijijini (CCM), Joseph Musukuma amesema sababu zinazotolewa na Serikali kuhusu kukatika kwa umeme mara kwa mara hazina msingi na ni ubabaishaji tu.

Musukuma ameyasema hayo jana Jumanne Februari 15, 2022 wakati akichangia taarifa ya Kamati ya Bunge ya Nishati na Madini kwa kipindi cha Januari 2021 hadi Februari 2022.

Amesema wakati umeme unaanza kukatika Watanzania walimuona Waziri wa Nishati, January Makamba akipaa na helkopta kuyaeleza mataifa kuwa kuna upungufu wa maji vyanzo vya maji na kwamba vimekauka.

“Chifu Hangaya akaomba tukapata mvua, tumerudi tena kwenye mashine (sababu za kukatika umeme). Sasa hii mitambo inaendeshwa kwa saa. Ndio maana kamati imewataka Tanesco (Shirika la Umeme Nchini) walete schedule (ratiba) ya miaka mitano service ilikuwa inafanyikaje, sio kuwtuambia sio kutuambia mitambo haikufanyiwa service,”amesema.

Amesema kutofanyiwa kwa ukarabati kwa mitambo  ya kuzalisha umeme ya kisasa kutasababisha kupiga honi na kwamba kama ikiwa ni ndani ya ukumbi wa Bunge hakuna mtu atakaa ndani.

“Kama ubabaishaji tu hakuna sababu za msingi za kutukatia umeme mara kwa mara. Ifanyike service za kimkoa mkoa au kipande sio kukaa kwenye giza nchi nzima na Serikali imehamasisha wakiingie kwenye viwanda vidogo vidogo na vya kati sasa hii inazua taharuki kubwa sana,”amesema.

Amesema kamati hiyo imeitaka Tanesco ije na sababu maalum inayofanya nchi ikose umeme sehemu nyingi za biashara.

Kuhusu Bwawa la umeme la kuzalisha Mwalimu Nyerere, Musukuma amesema haoni sababu ya  swaga zinazoendelea kuhusu ucheleweshaji wa ujenzi wa bwawa hilo. Amesema Rais Samia Suluhu Hassan wakati anaingia madarakani alikuta fedha Sh2 trilioni zimelipwa na yeye mwenyewe ameshalipa Sh1 trilioni na hivyo hakuna mkandarasi anayedai.

Ametaka Serikali kueleza tatizo liko wapi kuhusu kupungua kasi ya ujenzi wa mradi huo.

Kishoa asema ni aibu Kwa upande wake Mbunge wa Viti Maalum, Jesca Kishoa amesema mwenendo wa kukatika kwa umeme mara kwa mara nchini ni aibu kwa nchi na kutaka changamoto hiyo itatuliwe. Jesca Kishoa amesema hayo wakati akichangia taarifa ya shughuli za Kamati ya Nishati na Madini kwa kipindi cha kuanzia Januari 2021 hadi Februari 2022.

Amesema kumekuwepo na changamoto kubwa ya mwenendo wa hali ya umeme nchini na hata lile lengo la Taifa la kufikia megawati 5000 ifikapo mwaka 2025 litakuwa ni jambo ambalo lisilowezekana kwa sababu ya namna Taifa linavyokwenda.

“Kivutio kikubwa kwa wawekezaji ni umeme wa uhakika na namna tunavyokwenda tunapoteza wawekezaji wengi hakuna mwekezaji ambaye anaweza kuwekeza katika nchi ambayo umeme unakuwa wa kusuasua na kukatika katika mara,”amesema. Amesema hali ya kukatika umeme mara kwa mara inasababisha kuwaharibia mitambo. Jesca amesema sababu zinazotolewa na Serikali za kukatika umeme mara kwa mara kimsingi si sababu zinazotakiwa kuwaeleza.

“Tunaambiwa kuwa mitambo imechoka, tuna wahandisi wanazunguka kutafuta kazi kwanini wasiifanyie ukarabati? Kama sasa hivi tuna megawati 1,600 halafu tunashindwa kufanya marekebisho vipi lile dude la Mwalimu Nyerere likikamilika ambalo tunakwenda kuwekeza kwenye megawati zaidi ya 2000, tunakwenda kulipua nchi,”amesema.

Amehoji miongoni mwa sababu za kukatika kwa umeme mara kwa mara ni kuwa mitambo imezidiwa.

“Swali la kujiuliza hivi vinapokwenda kuagizwa kwenye wizara hakuna specification. Ni kama unachukua oksijeni kwa mgonjwa mmoja unakwenda kumwekea mwingine. Ni muhimu haya mambo yakafanyiwa kazi ni aibu sana,” amesema.

Makamba atoa majibu haya Waziri wa Nishati, January Makamba akijibu hoja hiyo amesema hakuna mtu kwenye wizara au Tanesco anapenda umeme ukatike na hakuna mtu anayefanya makusudi kukata umeme kwani hata sasa hivi watu wa Tanesco usiku wanashughulikia suala hilo linapotokea.

Amesema wanakuja na mradi mkubwa wa gharama ya Dola 1.9 bilioni untakaosaidia kuboresha vituo vya uzalishaji umeme na njia za umeme zilizopo. “Tunaomba wabunge mtu-support.”

Amesema nchi nzima kuna sub-stations 67 wakati kimuundo Tanesco ina wilaya 132 na kati ya sub-stations 67 Dar es Salaam ziko 37 hivyo stability ya umeme haiwezi kupatikana wakati hakuna sub-station nchini.

“Na katika hizo sub-station hizo zilizochakaa ni majority. Sasa tumetafuta hela tumetenga za ku-reffubish (kuboresha) sub-station 19 na kujenga nyingine mpya 59,” amesema na kuongeza “Tumeyakuta matatizo na tunayashughulikia kwa hakika.”

Chanzo: www.mwananchi.co.tz