Dar es Salaam. Mkuu wa Wilaya ya Tunduru, Julius Mtatiro amesema kwa miaka 10 yote aliyokuwa kada na kiongozi wa Chama cha Wananchi (CUF) aliamini CCM ndiyo chama bora kuliko vyote.
Mtatiro aliyetangaza kujiunga na CCM Agosti 11, 2018 amesema katika mahojiano na Mwananchi jana Jumamosi Novemba 2, 2019, jijini Dar es Salaam kuwa ameachana na madai ya Mabadiliko ya Katiba aliyokuwa nayo awali na sasa amejikita kwenye maendeleo.
“Wakati najiunga CUF miaka 10 iliyopita, the best option (chaguo bora) ilikuwa CCM, lakini sikutaka kujiunga nacho kwa kuwa niliona ni chama kikubwa, kimejijenga kina kila kitu, nikawa natafuta chama ambacho nitakijenga kitakuwa kikubwa, ndivyo nilivyofanya,” amesema Mtatiro.
Mtatiro aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CUF (Bara) amesema alikiona chama hicho chama hicho kinaweza kuwa jukwaa zuri la kisiasa.
“Lakini wakati huo hata nikilinganisha vyama, hata leo unaona chama imara nchini CCM. Kina nguvu, kina ubora kuliko vyama vingine. Chama chenye hadhi ya uongozi wa nchi, chenye ubora, kilichokuwepo tangu wakati wa TANU,” amesema.
Akizungumzia madai na misimamo kuhusu Katiba aliyoshiriki kuhamasisha kupitia majukwaa ya siasa, Mtatiro aliyeteuliwa kuwa DC wa Tunduru Julai 14, 2019 amesema aliyatoa tu kwa sababu alikuwa upande wa upinzani. “Wewe ni mwanadamu lazima uwe na upande. I was living in Rome, unaishi Roma utaishi kama Waroma, ukienda China leo watu tangu asubuhi wanapika nyoka, huwezi kufa njaa, utakula nyoka, ukienda Israel wanapika viazi utakula viazi,” amesema.
Ameongeza, “Wale waliokuwa na madai ya Katiba nimewaacha waendelee na madai ya Katiba, mimi kwa sasa nadai maendeleo, nimekwambia kwa sasa focus kubwa ya kujiunga na siasa ilikuwa ni maendeleo.”
“Hayo mengine nilikutana nayo tu kwenye vyama vya siasa, chama kinakaa kikao kinaamua kwamba tuna msimamo wetu katika Katiba kwa mfano ni serikali tatu, wewe ni kiongozi, mkitoka hadharani mtasema Serikali tatu.
Ameendelea kusema licha ya nafsi yake kutokubaliana na baadhi ya mambo ya upinzani alikubaliana nayo kwa kuwa alikuwa kiongozi.
“Wewe unakuwa Mkristo unaamini Yesu ni Mungu, baadaye umeona Ukristo haukufai ukaukiri Uislamu unakuta Yesu ni nabii, utasema Yesu ni Mungu?” amehoji.