Mbunge wa Geita Vijijini, Joseph Kasheku ‘Msukuma’ leo Ijumaa Aprili 8, 2022 ameeleza kuwa basi lake lililokamatwa kwa kosa la kuwa na samaki watatu linaozea kituoni lakini anashangaa aliyehusika na yeye analalamika.
Wakati Mpina akiwa Waziri wa Mifugo na Uvuvi, basi linalomilikiwa na Msukuma lilikamatwa likiwa na samaki na kutaifishwa. Wakati huo Serikali ilizuia uvuvi na usafirishaji wa samaki wadogo Ziwa Victoria.
Msukuma ametoa kauli hiyo wakati akichangia katika hotuba ya makadilio ya mapato na matumizi kwa Ofisi ya Waziri Mkuu na Wizara zilizochini yake ambapo amesema kuna watu huwa wanajisahaulisha wakisha kuwa nafasi za juu.
Hata hivyo Spika wa Bunge, Dk Tulia Akson amekea kauli hiyo akisema siyo sehemu ya mjadala ulio mbele ya bunge na kumtaka mbunge kujielekeza kwenye hoja mahususi huku akimsihi kufuta kauli yake aliyosema message delivery (ujumbe umefika).
Msukuma amemtaja moja kwa moja mbunge wa Kisesa, Luhwaga Mpina kwamba amekuwa mtu wa kulalamika huku akimhusisha yeye (Msukuma).
“Mimi sitaki kuangushiwa jumba bovu, nimeona katika moja ya mitandao nahusishwa na kauli yangu kuhusu ujenzi wa Bwawa la Mwalimu Nyerere, nililisema kweli na nikafuata taratibu zote, lakini tuliomba kibali cha kutembelea ambapo nakiri ujenzi wake umekwenda mara tatu ya alivyoacha Magufuli (Rais John Magufuli wa awamu ya tano),” amesema Msukuma.
Katika hatua nyingine ametaja hoja ya kupanda kwa bei ya mafuta Tanzania akitaka Serikali ichukue hatua za dharura kama ilivyofanya katika mazao ya wakulima, lakini ameonya bila kufanya hivyo wakati wowote mafuta yatapanda tena.