Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msimamizi wa uchaguzi amjibu Mrema

86014 Pic+mrema Msimamizi wa uchaguzi amjibu Mrema

Thu, 28 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Moshi. Msimamizi wa uchaguzi halmashauri ya Moshi vijijini mkoani Kilimanjaro, Juma Tukosa amewaonya wanasiasa  wanaoeneza taarifa kuwa uchaguzi katika kijiji cha Kiraracha haukuwa huru na haki.

Ameeleza hayo leo Jumanne Novemba 26, 2019 katika mkutano wake na waandishi wa habari kuhusu uchaguzi wa Serikali za mitaa ambao katika halmashauri hiyo ulifanyika katika kijiji hicho pekee. Wagombea walioshiriki ni wa CCM na TLP.

Mgombea wa CCM, Thomas Mrema alipata kura 518, dhidi ya mpinzani wake wa TLP, Adrea Lekule aliyepata kura 101.

Ametoa ufafanuzi kutokana na malalamiko yaliyotolewa na mwenyekiti wa TLP, Augustino Mrema kwamba chama hicho hakikutendewa haki katika uchaguzi huo.

Mrema aliyewahi kuwa naibu Waziri Mkuu, Waziri wa Mambo ya Ndani na mbunge wa Vunjo anaishi katika kijiji hicho.

Katika maelezo yake Mrema alilalamikia hujuma, kutotendewa haki licha ya kushiriki uchaguzi huo kwa nia njema ya kumuunga mkono Rais wa Tanzania, John Magufuli.

Tukosa amesema Mrema anapaswa kuacha kupotosha umma, ikiwa ataendelea atachukuliwa hatua.

“Wanasiasa  wanaopotosha umma waache, wakikaidi vyombo vya usalama vitawachukulia hatua mara moja kwa kuwa uchaguzi ulikuwa huru na haki.”

“Wanasema kuna Meya alikwenda ulipofanyika uchaguzi jambo ambalo si sahihi kwa sababu Halmashauri ya Moshi haina Meya, inaongozwa na mwenyekiti wa halmashauri,  Michael Kilawila ambaye ni mwanachama wa Chadema na hakuwahi kufika eneo la uchaguzi,” amesema msimamizi huyo.

Amemtaka Mrema kutambua kuwa uchaguzi ni maandalizi  na ushindi hautolewi mkononi na kumtaka akubali matokeo.

“Baadhi ya vyama vilidhani vitapewa ushindi mkononi, watambue ushindi haupatikani kwa kupewa, ushindi ni kushindana na katika kushindana lazima apatikane mshindi, ”alisema Tukosa.

Ofisa uchaguzi halmashauri ya Moshi, Patrick Nyavanga amesema uchaguzi unaendeshwa kwa kanuni na sheria na kuwataka wagombea ambao hawakuridhishwa na uchaguzi huo kufuata utaratibu.

Chanzo: mwananchi.co.tz