Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

TV

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msimamizi aagiza walioandika R badala ya L kutoenguliwa

83209 Pic+msimamizi Msimamizi aagiza walioandika R badala ya L kutoenguliwa

Sat, 9 Nov 2019 Chanzo: mwananchi.co.tz

Mwanza. Msimamizi wa uchaguzi halmashauri ya wilaya ya Tarime, Peter Nyanja amewaagiza wasimamizi wasaidizi kutotumia makosa madogo ikiwemo kukosea sarufi kuwaengua wagombea wa nafasi mbalimbali katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa.

Akizungumza na Mwananchi kwa njia ya simu leo Novemba 6, 2019, Nyanja ametaja makosa ambayo ameagiza yasitumike kuengua wagombea kuwa ni pamoja na kuandika R badala ya L yaliyolalamikiwa na viongozi wa vyama vya siasa kutumika kuengua baadhi ya wagombea.

Makosa hayo kwa baadhi ya watu yanatokana na lugha za asili ambako hushindwa kutofautisha wapi L na R zinatumika kwa usahihi.

“Nimewaelekeza wasimamizi wasaidizi katika eneo langu kuepuka kutumia makosa madogo ya kibinadamu ikiwemo matatizo ya kushindwa kutofautisha kati ya R na L kuwaengua wagombea,” amesema Nyanja.

Kauli hiyo ya msimamizi inakuja baada ya viongozi wa vyama vya upinzani akiwemo katibu wa Chadema mkoani Mara, Heche Chacha kulalamikia baadhi ya wagombea wa chama hicho kikuu cha upinzani nchini kuenguliwa kwa kuandika R badala ya L walipokuwa wakiandika neno wilaya katika fomu zao.

Akifafanua zaidi kuhusu makosa aliyowaagiza wasimamizi wasaidizi kutoyatumia kuengua wagombea, Nyanja amesema “Wapo baadhi ya wagombea wameshindwa kuandika halmashauri ya Tarime vijijini badala ya halmashauri ya wilaya ya Tarime. Nimeagiza wasienguliwe kwa sababu hayo ni makosa yanayofanywa hata na baadhi ya watendaji, watumishi na wasomi,” Ametaja makosa ya msingi yanayoweza kusababisha mgombea kuenguliwa kuwa ni pamoja na kukosea kuandika kwa usahihi eneo analogombea, kutoonyesha kazi yake halali ya kumuingizia kipato, kushindwa kuthibitisha uraia wake na kutojaza nafasi anayoomba kugombea.

“Pia nimeagiza wasimamizi wasaidizi wajiridhishe kuwa wagombea wanajua kusoma na kuandika. Kuna baadhi yao tumebaini wamejaziwa fomu kutokana na miandiko yao kutofautiana na inayoonekana kwenye fomu zao. Ni lazima tujiridhishe,” amesema

Kuhusu pingamizi zilizosababisha wagombea wengi kuenguliwa, Msimamizi huyo amesema ofisi yake inaendelea kusikiliza majibu ya waliowekewa pingamizi na kuwasihi viongozi, wanachama na wafuasi wa vyama vyote kuwa na imani kwa sababu wote watatendewa haki kwa mujibu wa sheria, kanuni na taratibu za uchaguzi.

 “Changamoto ninayoiona ni baadhi ya vyama kutowaelimisha vya kutosha wagombea wao; binafsi nilikaa na viongozi wa vyama vyote vya siasa na kuelimishana kanuni kifungu kwa kifungu na kurasa kwa kurasa. Lakini inashangaza kuona baadhi ya wagombea kujaza fomu kuomba kuteuliwa kugombea ujumbe bila kubainisha ni kupitia viti maalum au kundi la jumla,” amesema Nyanja

Akizungumzia madai ya orodha ya walioteuliwa na kuenguliwa kutobandikwa kwenye mbao za matangazo, msimamizi huyo amesema kwenye eneo lake hilo lilifanyika kwa sababu ni moja ya hitaji na sharti kwa mujibu wa kanuni ya 18 (1) hadi (4), sura ya 287 ya kanuni ya uchaguzi.

Usuli:

Wagombea wa vyama vya siasa wilayani Tarime walioathiriwa na tatizo la lugha asili kwa kuandika herufi ‘R’ badala ya ‘L’ kwenye neno wilaya wamepata ahueni baada ya Msimamizi kuagiza kosa hilo lisitumike kuwaengua

Chanzo: mwananchi.co.tz