Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msigwa akemea ubinafsi ndani ya chama

FbeVyCeWAAIpWSF Baraza la uongozi kanda NYASA

Sat, 3 Sep 2022 Chanzo: Mwananchi

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) Kanda ya Nyasa, Peter Msigwa amekemea ubinafsi na migogoro ndani ya chama, akiwataka viongozi kujitafakari kwenye utendaji kazi katika maeneo yao.

Akizungumza kwenye kikao cha ndani cha kikatiba cha chama hicho kilichofanyika jijini hapa juzi, Msigwa alisema Uchaguzi Mkuu ujao, hawataki tena vilio vya kuibiwa kura.

Msigwa alisema Chadema haina hati miliki ya mtu, badala yake yeyote anaweza kuongoza na kuwataka viongozi kukubali kushauriwa.

Alisema kwa sasa imefika mwisho kwa chama hicho kila uchaguzi kulia kuibiwa kura na sasa kila mmoja ajipange kwa kuhakikisha anasajili wanachama wapya kidijitali na kuwa msemaji wa wananchi.

“Ukiwa kiongozi jitafakari unawafanyia nini wananchi wako, lazima tupate mabadiliko, mambo ya kulialia kila uchaguzi kuibiwa kura tutoke huko, tujipange; kwa sasa vipaumbele vyetu kitaifa ni kuwasemea wananchi na kujisajili kidigitali,” alisema Msigwa, aliyewahi kuwa mbunge wa Iringa Mjini.

Mjumbe wa Kamati Kuu ya chama hicho Taifa, Patrick Sosopi alisema kwa miaka sita nyuma walipitia kipindi kigumu na kwamba kwa sasa mazungumzo na maridhiano yanayoendelea baina ya vyama vya upinzani na chama, yanaenda kuponya maumivu.

Spika wa Bunge la Wananchi, Celestine Simba aliwataka viongozi wa chama hicho kujiandaa mapema kugombea nafasi mbalimbali kuanzia ngazi za chini tofauti na miaka iliyopita.

“Tunapoelekea kwenye uchaguzi wa Serikali za mitaa na ule mkuu tujipange mapema, suala hili ni mchakato, ule uliopita wagombea walikuja dakika za mwisho, hatutarajii lijirudie tena, tunataka kuona tunachukua majimbo mengi,” alisema Celestine.

Mwenyekiti wa chama hicho mkoani Mbeya, Joseph Mwasote alisema tangu 2019, mkoa huo umepitia kipindi kigumu kwa baadhi ya viongozi kukigawa chama kimakundi, lakini kwa sasa kimerejea kwenye hali yake.

“Nimpongeze mwenyekiti wetu kwa kazi aliyoifanya, wapo waliotengeneza makundi lakini tumesimama upya na sasa migogoro imeisha, leo tunakutana kwa pamoja, niwashukuru viongozi wenzangu,” alisema Mwasote.

Chanzo: Mwananchi