Habari

Burudani

Michezo

Biashara

Afrika

Live Radio

Nchi

Kijamii

Lifestyle

SIL

Msigwa, Sugu wachuana kwa hoja

SUGU MSZA Mchungaji Msigwa kulia na Sugu wakishiriki kwenye mdahalo huo uliorushwa na Star TV.

Mon, 27 May 2024 Chanzo: www.tanzaniaweb.live

Wagombea wa Uenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Kanda ya Nyasa, Mchungaji Peter Msigwa na Joseph Mbilinyi 'Sugu' wameanza kuchuana kwa hoja nzito:

Sugu amedai amejitosa kwenye nafasi hiyo kutokana na msukumo wa wanachama ambao hawaridhishwi na uongozi wa sasa na hivyo kutaka mabadiliko.

Mch. Msigwa amesema hoja hiyo haina mashiko kwa kuwa kanda hiyo ndiyo inaongoza kwa kuandikisha wanachama wake kidigiti. Kama ingekuwa na migogoro, hilo lisingewezekana.

Mch. Msigwa anatetea nafasi yake kwa mara nyingine wakati Sugu ni mara ya kwanza kuingia kwenye kinyang`anyiro hicho.

Juzi wagombea hao walikutanishwa uso kwa uso katika mdahalo uliorushwa kupitia kipindi cha 'Medani za Siasa' cha kituo cha runinga cha Star Tv.

Sugu alisema aliamua kujitosa kwenye nafasi hiyo si kutokana na kuangalia mabaya au mazuri aliyoyafanya Mc. Msigwa bali vurugu za wanachama wenyewe ambao hawaridhishwi na mpinzani wake huyo wa sasa na hivyo kutaka mabadiliko.

Alimrushia lawama Mch. Msigwa kwamba ameshindwa kutatua migogoro iliyopo katika kanda hiyo, kutumia vibaya Katiba ya chama kuhalalisha mambo yake, kutengeneza vijana kuwa ‘machawa’ wake na kushindwa kujenga ofisi ya chama.

"Mimi nikichaguliwa, nitakuwa mwenyekiti wa kuleta umoja na kuweka watu pamoja, ili tuwe na CHADEMA Kanda ya Nyasa salama ambayo haina migogoro kama ilivyokuwa sasa hivi," Sugu alisema.

Naye Mch. Msigwa alijibu kwa kuhoji kwanini kanda hiyo iongoze kwa wanachama wake kujiandikisha kidigiti kama kweli ina migogoro anayoisema Sugu.

Alisema akichaguliwa kwa mara nyingine, atakuja kwa kasi kubwa zaidi kwa kutumia uzoefu wake aliopata katika kipindi chote akiwa kwenye nafasi hiyo.

"Nitakuwa mwenyekiti wa kuunganisha wanachama, kuongeza shauku, ari na hamu ya wanachama kukipenda chama chao zaidi, kukabiliana na CCM ambayo ndio mahasimu wetu kisiasa. Wanachama na wapenzi wa Kanda ya Nyasa wategemee kumpata Msigwa anayekuja kwa kasi kubwa zaidi," alisema Msigwa.

Alisema anaiona Nyasa kama jiwe la dhahabu ambalo ni tunu ya chama chao kukabiliana na CCM, hivyo wanahitaji kiongozi mwenye maono ya kuunganisha watu na anayefundisha.

Kuhusu migogoro kwenye kanda yake, Mch. Msigwa alisema, "Mwarobaini huwa hautupiwi mawe, unaotupiwa mawe ni mwembe, kwenye chama chetu tuna kanda 10, kwenye kanda hiyo, Nyasa inayoitwa ya migogoro ndiyo kinara wa kanda zote, sisi tumesajili wanachama wengi zaidi, migogoro yote inayojitokeza huwa tunaitatua kwa kuzingatia Katiba ya chama."

Kuhusu rushwa, Mch. Msigwa alisema haamini katika kutumia rushwa kupata uongozi, hahitaji kununua uongozi kwa sababu hata akikosa uongozi hatakufa.

Kwa mujibu wa CHADEMA, baada ya kufanyika uchaguzi katika Kanda ya Victoria juzi, uchaguzi mwingine katika kanda tatu za Nyasa, Serengeti na Magharibi utafanyika Mei 29 mwaka huu.

Chanzo: www.tanzaniaweb.live